07-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Da'wah (Ulinganiaji Wa Dini)
07-Subira Katika Da’wah (Ulinganiaji Wa Dini)
Da’wah katika Dini hii tukufu ina fadhila nyingi mno kama zilivvyothibiti dalili zake katika Qur-aan na Sunnah. Daa’iyah (mlinganiaji) atakapoweza kuitekeleza kazi hii ipasavyo basi hakika atakuwa amebahatika kutekeleza kazi tukufu kabisa na ya hadhi kwake, kwani huko ni kuendeleza majukumu ya Rusuli na Manabii waliowalingania watu wao kufuata haki. Na da’wah ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kila Muislamu na kwa hivyo ni jukumu la kila mmoja kulifanyia kazi kwa kuwaita watu katika Tawhiyd (kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuwakumbusha watu maneno na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili watu wabakie katika taqwa, iymaan, usalama na amani ya dunia na Aakhirah yao. Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaiambatanisha amri hiyo pamoja na mafaniko ya hakika. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ وَيَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ ۚ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفلِحُونَ ﴿١٠٤﴾
Na watokeze kutoka kwenu umati wa watu unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu. [Aal-‘Imraan: 104]
Akabainisha pia kwamba bila ya kulingania haki na kuusina na subira ni mambo yatakayomfanya mwana Aadam awe katika khasara [Suwrah Al-Aswr]
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliusia kazi hii pale aliposimama katika Jabali la ‘Arafah katika Hijjah yake ya mwisho baada ya kuwapa Maswahaba mawaidha na nasaha zake akahakikisha nao kuwaliza kama alitimizia risalah aliyotumwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa); wakakiri Maswahaba hilo, kisha akawaamrisha:
(( أَلا فَلْيُبَلِّغِ الشَّاهِدُ مِنْكُمُ الْغَائِبَ))
((…basi abalighishe (afikishe ujumbe) aliyekuweko shahidi hapa miongoni mwenu kwa asiyekuweko)) [Al-Bukhaariy]
Kwa maana kila mmoja wao aendelee kubalighisha risala na mafunzo yake, kizazi baada ya kizazi mpaka kitakaposimama Qiyaamah. Na akausia pia katika kauli yake nyingine:
((بَلِّغُوا عَنِّي وَلَوْ آيَةً))
((Fikisheni kutoka kwangu (ujumbe) japo Aayah moja)) [Al-Bukhaariy]
Kauli hiyo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inadhihirisha umuhimu mkubwa wa kila Muislamu kuamrisha mema na kukatazana maovu hata ikiwa ni Aayah au Hadiyth moja aliyojifunza kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Kulingania huko kuwe kwa baswiyra (nuru za elimu, dalili, hoja na umaizi) kama Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyomuamrisha Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي﴿١٠٨﴾
Sema: “Hii ndio njia yangu nalingania kwa Allaah, juu ya nuru za elimu na umaizi, mimi na anayenifuata. [Yuwsuf: 108]
Na baswiyrah ni elimu sahihi inayopatikana katika vyanzo vya kuaminika na kutoka kwa ‘Ulamaa wenye manhaj ya Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia). Baswiyra pia ni hikma kama vile vile Alivyoamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ﴿١٢٥﴾
Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi [An-Nahl: 125]
Na da’wah ndio inayotengeneza Ummah kwa kuwatoa watu kutoka katika kiza kuingia katika Nuru, na kutoka katika upotofu kuelekea hidaaya, na kugeuza ubatilifu kwa haki, na kugeuza shari kwa kheri, na ndio maana imeambatinishwa na ukamilifu wa iymaan.
كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ﴿١١٠﴾
Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah [Aal-‘Imraan: 110]
Sharti kuu la da’wah ni kuweko ikhlaas kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na inahitaji daa’iy (mlinganiaji) awe mnyenyekevu kwa watu anaowalingania ili kusiweko alama ya kiburi, riyaa au aina yoyote ya kujifakharisha. Bali daa’iy awe mwenye tabia njema katika kauli zake na matendo yake: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٣٣﴾
Na nani mwenye kauli nzuri zaidi kuliko yule anayelingania kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa Waislamu.” [Fusw-Swilat: 33]
Na pia inahitaji subira ya hali ya juu kwani daa’iy wa mambo ya haki hataacha kukumbwa na mitihani mbali mbali. Na hiyo ndio jihadi ya kweli kwa kujirekebisha mtu tabia zake, kutumia wakati wake, mali yake na kila neema aliyoruzukiwa na Rabb wake katika kazi hii tukufu. Pia aweze kuvumilia maudhi ya watu, jambo ambalo haliepukani kwa kila daa’iy. Na hapo inahitaji azimio kubwa la kuendeleza da’wah kama walivyovumilia Rusuli na Manabii. Luqmaan alipompa nasaha mwanawe alimkumbusha kuvuta subira katika kazi hii tukufu:
يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ وَأْمُرْ بِالْمَعْرُوفِ وَانْهَ عَنِ الْمُنكَرِ وَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا أَصَابَكَ ۖ إِنَّ ذَٰلِكَ مِنْ عَزْمِ الْأُمُورِ ﴿١٧﴾
“Ee mwanangu! Simamisha Swalaah, na amrisha mema na kataza ya munkari, na subiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa. [Luqmaan: 17]
Kwa hiyo daa’iy inampasa afuate nyendo za Rusuli na Manabii anaposibiwa na mitihani ya da’wah khasa kutokana na maudhi ya watu, kwani Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivumilia mateso na maudhi ya Makafiri, Mayahudi na wanafiki waliomkadhibisha, wakamfanyia kila aina ya istihzai kwa kumwita mwendawazimu, mtungaji mashairi, kahini, mchawi, hata kufika kumpiga mawe lakini alivumilia na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamlinda hadi Akaleta nusra Yake mpaka akasimamisha na kuineza Dini ya Kiislamu. Basi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awe ni kigezo bora kwa daa’iy wa Dini hii tukufu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Haendi kinyume na ahadi Yake Anaposema:
إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ﴿٥١﴾
Hakika Sisi Tutawanusuru Rusuli Wetu, na wale walioamini katika uhai wa dunia na Siku watakayosimama mashahidi. [Ghaafir: 51]
Kwa ahadi hiyo na nyinginezo za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), ziwe ni matumaini makubwa kwa Muislamu anayelingania watu katika haki na atawakali kwa Rabb wake akitarajia pia malipo mazuri kabisa ya Jannah ambako ndiko kwenye maisha ya milele. Wala hakutakuwa na usalama, amani, furaha wala mafaniko yoyote ila kwa kufuata maamrisho ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ya kubalighisha risala ya Dini hii tukufu kwa watu wote kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
هَـٰذَا بَلَاغٌ لِّلنَّاسِ وَلِيُنذَرُوا بِهِ وَلِيَعْلَمُوا أَنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ وَلِيَذَّكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ﴿٥٢﴾
Hii (Qur-aan) ni ubalighisho wa risala kwa watu, na ili wawaonye kwayo, na ili wapate kujua kwamba hakika Yeye ni Muabudiwa wa haki Mmoja Pekee na ili wakumbuke (na wawaidhike) wenye akili. [Ibraahiym: 52]
Maonyo makali yamethibiti katika Qur-aan na Sunnah kwa kutokuitimiza kazi hii tukufu ya kuamrisha mema na kukatazana mema, japokuwa kutakuweko mitihani mbali mbali, na kwa hivyo hapana budi kuvuta subira na kutaraji malipo yake mazuri yasiyokuwa na hesabu.