06-Swabrun Jamiyl: Subira Katika Kutafuta Elimu
06 - Subira Katika Kutafuta Elimu
Kutafuta elimu ni waajib kwa kila Muislamu. Na kuifanyia kazi kwa kufuata mafunzo yake, na kuitumia elimu kwa kufunza wengineo yote inahitaji subira; na subira zaidi inahitajika kwa kutokuharakiza kupata matokeo au kutokuchoka au kukata tamaa inapokuwa hali ngumu ambayo mtu hakuitegemea.
Kuchuma elimu ni jambo tukufu kabisa kwa Muislamu kwani inafikisha kumtambua Rabb wake na kuyatambua yampasayo kutenda na yanayopasa kuepukana nayo. Kufanya hivyo ni alama ya kutakiwa kheri na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما)، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ يُرِدِ اللَّهُ بِهِ خَيْرًا، يُفَقِّهْهُ فِي الدِّينِ)) أخرجه الترمذي وغيره وقال: حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anayekusudiwa kheri na Allaah, [Allaah] Humpa ufaqihi [ujuzi] katika Dini)) [At-Tirmidhiy na wengineo na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]
Kheri hiyo ya kupata ujuzi wa Dini inampelekea Muislamu katika kheri kubwa zaidi ya kumfikisha kwenye makazi ya kudumu milele. Kwa hiyo ni dhahiri kuwa elimu ni ufunguo wa Jannah. Amethibitisha hilo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عن أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((مَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَبْتَغِي فِيهِ عِلْمًا، سَلَكَ اللَّهُ بِهِ طَرِيقًا إِلَى الْجَنَّةِ)) مسلم
Imepokelewa toka kwa Abuu Ad-Dardaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Anayetafuta njia ya kutaka elimu humo, Allaah Humpatia njia ya Jannah [Peponi])) [Muslim]
Fadhila nyingi mno za mwenye kutafuta elimu zimethibiti katika Qur-aan na Sunnah, ila Muislamu hawezi kuzidiriki bila ya kuwa na subira kwani anahitaji kuwa na uvumilivu katika kila hali atakapokuwa katika safari yake ndefu ya kutafuta elimu hata aweze kuifahamu kwa kina na akamilishe masomo yake. Ndipo tukawa tunahitaji kuomba Du’aa:
((الَّلهُمَّ انْفَعْنِي بِمَا عَلَّمْتَنِي وَعَلِّمْنِي مَا يَنْفَعُنِي وَزِدْنِيعِلْمًا))
Allaahumma Anfa’niy bimaa ‘Allamtaniy, wa ‘Allimniy maa yanfa’uniy wa-Zidniy ‘ilmaa.
((Ee Allaah, Ninufaishe kwa Unayonifunza, na nielimishe yatakayoninufaisha na nizidishie elimu)) [Swahiyh Ibn Maajah]
Yafuatayo ni mambo ambayo mtafutaji elimu (mwanafunzi), hana budi nayo na anapaswa kuyavumilia:
1-Kujifunza Qur-aan Na Hadiyth Pamoja Na Kuzihifadhi
Qur-aan ni somo linalohitaji subira kwani kuna mashaka ya kujifunza kuzitamka herufi za Qur-aan zipasavyo, kuihifadhi moyoni, na kuifanyia kazi maamrisho yake:
عَنْ عَائِشَةَ قَالَتْ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((الْمَاهِرُ بِالْقُرْآنِ مَعَ السَّفَرَةِ الْكِرَامِ الْبَرَرَةِ وَالَّذِي يَقْرَأُ الْقُرْآنَ وَيَتَتَعْتَعُ فِيهِ وَهُوَ عَلَيْهِ شَاقٌّ لَهُ أَجْرَانِ))
Imetoka kwa mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yule aliyekuwa hodari wa kusoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika Waandishi wa Allaah watukufu wema, na yule ambaye anaisoma Qur-aan kwa mashaka na huku anajitahidi kwa kudodosa atapata ujira mara mbili)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hali kadhalika kujifunza na kuhifadhi Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwani atazihitaji kuzifundisha kwa wengineo; jambo litakalompatia fadhila na malipo mema:
عن إبْنِ مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) ِ قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولُ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: (( نَضَّرَ اللَّهُ امْرَأً سَمِعَ مِنَّا شَيْئًا فَبَلَّغَهُ كَمَا سَمِعَه، فَرُبَّ مُبَلِّغٍ أَوْعَى مِنْ سَامِعٍ)) وراوه الترمذي وقَالَ : حَدِيثٌ حَسَنٌ صَحِيحٌ
Imepokelewa toka kwa ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Allaah Amneemeshe mtu aliyesikia kitu kutoka kwetu naye akakifikisha kama alivyosikia. Huenda anayefikishiwa akawa mwenye kufahamu zaidi kuliko aliyesikia)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan Swahiyh]
Masomo ya Dini yanahitaji uvumilivu na si pupa ili yathibitike na yafahamike vilivyo. Inahitaji pia kudurusiwa mara kwa mara ili isipotee moyoni baada ya kuthibitika kwani itakapopotea moyoni itakuwa ni khasara kubwa ya kupoteza muda wake wote, na pengine hata kupoteza mali aliyoitumia kwa ajili ya kuichuma elimu hiyo. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ametunasihi:
عَنْ أَبِي مُوسَى عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((تَعَاهَدُوا الْقُرْآنَ فَوَالَّذِي نَفْسِي بِيَدِهِ لَهُوَ أَشَدُّ تَفَصِّيًا مِنْ الْإِبِلِ فِي عُقُلِهَا))
Kutoka kwa Abuu Muwsa (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Shikameni (dumisheni kuisoma) na Qur-aan, kwa hakika naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, ni wepesi zaidi kukimbia (kupotea akilini) kuliko ngamia anavyochopoka katika kamba yake)) [Al-Bukhariy na Muslim]
Amesema ‘Umar ibn Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) “Tulikuwa tunahifadhi Aayah kumi na hatukuziendea nyingine mpaka tumezifanyia kazi (hizo kumi)”. Imesimuliwa pia kwamba alihifadhi Suwratul-Al-Baqarah katika muda wa miaka tisa, na hivyo si kwa ajili ya kuhifadhi au kuzijua maana yake tu, bali kuzifahamu kwa bayana na kwa kina na kutekeleza maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake. Na hivyo ndivyo inavyompasa mwanafunzi au mtafutaji elimu kwani ni miongoni mwa mambo manne yanayowajibika kwa kila Muislamu kujifunza kama alivyoyaasisi Al-Imaam Muhammad ibn Al-Wahhaab katika Kitabu chake ‘Al-Uswuul Ath-Thalaathah’.
2- Mwanafunzi Kujifunza Na Kutekeleza Adabu Za Kiuanafunzi:
Inampasa kwanza mwanafunzi ajifunze adabu za kiuanafunzi na kuwa na subira pale anapokuwa hakufahamu anayoyaelezea mwalimu wake, na hivyo kwa kutokuuliza maswali mengi wakati mwalimu anaposomesha au kusherehesha darsa, bali asubiri hadi atakapomaliza. Pia awe na heshima mbele ya mwalimu kwa kumkabili kwa upole na adabu, kutimizia anayomwamrisha yanayohusiana na masomo yake. Kadhalika mwanafunzi anapaswa kutekeleza na kufuata taratibu za utafutaji elimu na kuwa na uvumilivu mkubwa katika hilo.
3-Kuamka Usiku Wa Manane:
Kufanya juhudi kuamka usiku hakuna budi kwa anayetafuta elimu kwa sababu ndio wakati wenye utulivu na muwafaka zaidi kwa masomo kwani Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ نَاشِئَةَ اللَّيْلِ هِيَ أَشَدُّ وَطْئًا وَأَقْوَمُ قِيلًا﴿٦﴾
Hakika kuamka usiku (kuswali) ni uthibiti zaidi wa kuathiri moyo na kuifahamu na unyofu zaidi wa maneno kutua. [Al-Muzzammil: 6]
Lakini kunahitaji subira kwani kuna mashaka ya kukata mtu usingizi wake wakati watu wamelala. Avute subira kwa kuachilia mbali kitanda chake akaamka na akajiamsha zaidi kwa kutia wudhuu akasimama kuswali kisha akadurusu masomo yake. Anayetafuta elimu hana budi kukosa raha kwani hawezi mtu kuichuma elimu akiwa ameshuhgulishwa na raha za dunia. Imepokelewa kutoka kwa Yahyaa bin Yahyaa At-Tamiymiy amesema: “Abdullaahi bin Yahyaa bin Abi Kathiyr amesema: Nimemsikia baba yangu akisema: “Elimu haiwezekani kwa raha ya mwili” [Imesimuliwa na Muslim katika ‘Kitabu cha Misikiti Na Sehemu Za Swalaah - Mlango wa Swalaah Tano]
4- Kudurusu Masomo Na Kufanya Utafiti:
Subira katika kufanya utafiti na kufuatilia elimu japokuwa ni mbali mno pa kuipatia. Maswahaba na waja wema walisafiri maelfu na maelfu ya maili kwa ajili ya kutafuta elimu.
Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amekusanya maelfu ya Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Swahibu zangu katika watu wa Makkah walikuwa wakijishughulisha na biashara masokoni, na swahibu zangu katika watu wa Madiynah walikuwa wakijishughulisha na kilimo, lakini mimi nilikuwa masikini niliyetumia muda wangu mwingi kukaa pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nilikuwa nikihudhuria wasipohudhuria, na nikihifadhi wanaposahau.”
Imaam Ahmad bin Hanbal alitembea maili thelathini elfu kutafuta Hadiyth na akahifadhi maelfu ya Hadiyth, na akaacha nyuma yake hazina ya Vitabu.
Na Jaabir bin ‘Abdillaah alisafiri muda wa mwezi mmoja kwenda Misr kutafuta Hadiyth moja.
Imaam An-Nawawy ambaye aliishi muda wa miaka 45 lakini kwa muda huo wa maisha yake mafupi, alikuwa akitumia muda wake wote kutafuta elimu na kuifunza, hata hakuwa akila chakula kizuri na wala hakutamani kuoa.
5-Kuwa na Taqwa Na Utiifu;
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾
Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 200]
Huo ni wito kwa Waumini wote, na inawahusu zaidi watafutao elimu kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameihusisha Aayah na mafanikio ya dunia na Aakhirah kwa mambo manne; subira, kuzidi kuvuta subira, kubakia imara na taqwa. Subira hiyo inajumuisha aina zote za subira; subira katika utiifu, kuacha maasi, kukubali Qadhwaa na Qadar (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa), kuvumilia maudhi ya watu. Na kutafuta elimu kunampeleka mtu kwenye taqwa kwa kuwa atakuwa akitumia wakati wake wote katika kutafuta elimu, kujifunza, kutekeleza ‘ibaadah kusubiri Swalaah baada ya Swalaah, na kila aina ya ‘amali njema.Pia itamwongoza mtu katika tabia za upole, ukarimu n.k. ambazo humkurubisha mja kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Inahitaji pia kujiepusha na maasi kwani atakapoiendekeza mtu nafsi yake atatumbukia kwayo na kushughulishwa nayo hata asiweze tena kuwa na muda wa kutafuta elimu au akose kuwa na taqwa na utiifu. Yote hayo yanahitaji subira.
6-Kuhudhuria Vikao Vya Darasa, Mihaadhara Na Kusikiliza Kwa Makini”
Kuvuta subira katika kuhudhuria vikao vya darasa na mihadhara ya Dini hata kama si wakati muwafaka au uliouzoea kama alfajiri au usiku baada ya Swalaah ya ‘Ishaa, kwa makini japokuwa akili imeshughulishwa na mengineyo. Kubakia hadi mwisho wa darsa ili ufaidikie na yote anayoyafundisha mwalimu japokuwa umechoka au una usingizi. Aghlabu baadhi ya wanafunzi huanza masomo yao kwa hamu na juhudi kubwa lakini hawafiki hata robo yake huchoka na kukata tamaa kutokana na mashaka wanayokumbana nayo.
7-Kuwa na Zuhd (Kuipa dunia mgongo):
Mwenye kutafuta elimu anapaswa pia kuwa na sifa ya zuhd ambayo inahitaji subira kwa sababu ni kukinaisha nafsi yake na matamanio ya dunia. Na kuipa mgongo dunia si jambo jepesi ila kwa ambaye Allaah Amemrehemu. Zuhd pia inamfanya mtu awe mnyenyekevu na inamjaza mapenzi ya kutangamana na masikini na walio dhaifu wenye taqwa na kuepukana na matajiri ambao wanaoshughulika na starehe za dunia badala ya kushughulika na mambo ya Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَاصْبِرْ نَفْسَكَ مَعَ الَّذِينَ يَدْعُونَ رَبَّهُم بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ يُرِيدُونَ وَجْهَهُ ۖ وَلَا تَعْدُ عَيْنَاكَ عَنْهُمْ تُرِيدُ زِينَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَا تُطِعْ مَنْ أَغْفَلْنَا قَلْبَهُ عَن ذِكْرِنَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ وَكَانَ أَمْرُهُ فُرُطًا ﴿٢٨﴾
Na isubirishe nafsi yako pamoja na wale wanaomuomba Rabb wao asubuhi kabla jua kucha na jioni, wanataka Wajihi Wake. Na wala macho yako yasiwavuke kwa kutaka pambo la uhai wa dunia. Na wala usimtii Tuliyemghafilisha moyo wake na Ukumbusho Wetu akakafuata hawaa zake, na jambo lake limekuwa la kuzidi kuvuka mipaka. [Al-Kahf: 28]
Kupata mapenzi ya watu atakaowafanyia da’wah ni muhimu kwani kutawajengea imani na mlinganiaji au mwalimu; na hivyo itasababisha kumsikiliza na kumfuata kwa sababu ya unyenyekevu wake kwao ambao unadhihirisha ikhlaas yake kwao kwa kutokujali manufaa ya kidunia. Juu ya hivyo ni kupata mapenzi ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Ameusia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa Ummah wake:
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ السَّاعِدِيِّ (رضي الله عنه) قَالَ: أَتَى النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَجُلٌ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ ، دُلَّنِي عَلَى عَمَلٍ إِذَا أَنَا عَمِلْتُهُ أَحَبَّنِي اللَّهُ وَأَحَبَّنِي النَّاسُ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((ازْهَدْ فِي الدُّنْيَا يُحِبَّكَ اللَّهُ وَازْهَدْ فِيمَا فِي أَيْدِي النَّاسِ يُحِبُّوكَ)) إبن ماجه وغيره بأسانيد حسنة
Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’iyd As-Saa’idiyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Nijulishe amali ambayo nikiifanya Allaah Atanipenda na watu pia watanipenda” Akasema: ((Ipe mgongo dunia Allaah Atakupenda, na uvipe mgongo vilivyomo kwa watu, watu watakupenda)) [Ibn Maajah na wengineo kwa isnaad Hasan]
Basi kuwa na zuhd ee mwanafuzi na daa’iy (mlinganiaji Dini] wakupende watu. Na kuwa na zuhd akupende Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwani Yeye Hapendi mwenye kuifadhilisha dunia kabla ya Aakhirah, bali Ameilaani hiyo dunia na wakaazi wake isipokuwa watatu:
عن أبي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: (( أَلاَ إِنَّ الدُّنْيَا مَلْعُونَةٌ مَلْعُونٌ مَا فِيهَا إِلاَّ ذِكْرُ اللَّهِ ، وَمَا وَالاَهُ ، وَعَالِمٌ أَوْ مُتَعَلِّمٌ)) الترمذي وقال: حَدِيثٌ حَسَنٌ
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Zindukeni! Dunia imelaaniwa, kimelaaniwa kilichomo humo isipokuwa kumtaja Allaah na jambo linalokaribiana na hilo (la kumtii Allaah), Mwanachuoni na anayejifunza [Dini])) [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]
Kwa hiyo ukiwa ni mwenye zuhd, ukashughulika kutafuta elimu na moyo wako ukawa umeelemea kwayo na ukajazwa mapenzi yake, shaytwaan hataweza kukughafilisha na dunia. Hutofikiria mali, wala kupata pato lolote kwa kazi yako ya da’awah, wala hutojikalifisha kuishi maisha ya raha, wala hutotamani starehe yoyote, kwani hakuna kitakachokushughulisha ila mambo matatu hayo ambayo yanamhusu mtafutaji elimu, kwa vile muda wako wote utakuwa ni kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kutafuta elimu na kuifunza au kuibalighisha kwa wengineo, na hayo ni utiifu na ambayo yanahitaji subira ya kweli.