09-Swabrun Jamiyl: Yapasayo Na Yasiyopasa Wakati Wa Mitihani

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

09 - Yapasayo Na Yasiyopasa Wakati Wa Mitihani

 

 

 

Swabrun Jamiyl (subira njema) ni kuzuia ulimi usinene yasiyopasa wala kumshtakia yeyote isipokuwa kumshtakia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na pia moyo uvumilie asimahanike mtu na kukata tamaa, na viungo visitende yaliyoharamishwa kama kujipigia mashavu na kuchana nguo n.k., basi Muumini anapaswa  kuzingatia na kutekeleza au kujiepusha yafuatayo:

 

 

 1-Kuridhika Na Majaaliwa Na Kusalimu Amri:

 

 

Muumini atambue kwamba kila linalomfika ni majaaliwa yaliyokwishahukumiwa katika Lawhum-Mahfuudhw (Ubao Uliohifadhiwa), kwa hiyo hana budi nayo, bali aridhike nayo apate radhi za Rabb wake na ujira wa kuvumilia. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴿٢٢﴾

Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.

 

لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ ﴿٢٣﴾

Ili msisononeke juu ya yale yaliyokuondokeeni na wala msifurahie kwa yale Aliyokupeni (Allaah); na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha. [Al-Hadiyd: 22-23]

 

 

Bali Muumini anapaswa kuwa na tawakuli na Allaah na akumbuke kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿٥١﴾

Sema: “Halitusibu (lolote) isipokuwa lile Alilotukidhia Allaah. Yeye ni Maulaa wetu.” Basi kwa Allaah watawakali Waumini. [At-Tawbah: 51]

 

 

Na huko ndiko kuthitibisha iymaan ya Muumini kwa  kuridhika na majaaliwa kama Anavosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

 مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿١١﴾

Hausibu msiba wowote isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Na yeyote   anayemuamini Allaah, (Allaah) Huuongoza moyo wake. Na Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi. [At-Taghaabun: 11]

 

 

 

2- Kutokushitaki Au Kumlalamikia Kwa Watu Masaibu Na Mitihani Bali Kumuomba Allaah:

 

 

Kulalamika au kushitaki kwa watu kunaharibu subira na kumkosesha mtu fadhila zake, kwani anayeshtaki mitihani ya Rabb wake kwa kiumbe huwa amemshtakia ambaye hawezi kumnufaisha au kumuokoa katika mitihani yake. Lililo la busara ni amshtakie Rabb wake Ambaye ni Pekee Mwenye uwezo wa kumteremshia rahamh Akampa faraja.  Mmoja miongoni mwa Salafus-Swaalih alipomuona mtu anamshtakia mwenziwe alimwambia:

 

Vipi unamshtaki Anayekurehemu kwa asiyekuwa na uwezo wa kukurehemu?”

 

Tumepta fundisho bora kutoka kwa Nabiy Ya'aquwb ('Alayhis-Salaam) pale alipojazwa na huzuni kwa kumkumbuka mwanawe mpenzi Yuwsuf na kisha kupotelewa na mwanawe wa pili bin Yamiyn pindi aliposema:

 

 إِنَّمَا أَشْكُو بَثِّي وَحُزْنِي إِلَى اللَّـهِ﴿٨٦﴾

 “Hakika mimi nashitakia dhiki ya majonzi yangu na huzuni zangu kwa Allaah  [Yuwsuf: 86]

 

Lakini inafaa kumshtakia mtu pale anapofikwa na hali ya kuhitaji msaada wa mtu aliojaaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na si msaada ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Pekee Ndiye Mwenye uwezo nao. Mfano, kulalamika dhulma anayotendewa na mwenzake inayoendelea ikiwa anayeshtakiwa ana mamlaka ya kumwepusha na anayemdhulumu, au anapotafuta msaada wa gharama za matibabu ya maradhi yake, au kuomba msaada wa kutatua jambo fulani gumu n.k. kwa kuitikadi kwamba uwezo huo unatokana na Nguvu na Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Aliomjaalia huyo msaidizi.  

 

 

 

 3- Kuomba Maghfirah Na Toba

 

 

 Huenda ikawa mitihani inayomsibu mtu ni kutokana na madhambi aliyoyatenda hivyo ni vyema arudi kwa Rabb wake kuomba maghfirah na toba. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٤١﴾

Ufisadi umedhihiri katika nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale iliyochuma mikono ya watu ili (Allaah) Awaonjeshe baadhi ya ambayo wameyatenda ili wapate kurejea. [Ar-Ruwm: 41]

 

Na Anasema pia:

 

وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ﴿٣٠﴾

Na haukusibuni katika msiba wowote basi ni kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono yenu, na Anasamehe mengi.  [Ash-Shuwraa: 30]

 

 

 

 4-Kumdhukuru Na Kumshukuru Mno Allaah

 

 

 Kila unapomdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Naye Hukukumbuka. Kauli nzuri iliyoje Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:

 

 فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ﴿١٥٢﴾

Basi nidhukuruni na Mimi Nitakukumbukeni; na nishukuruni wala msinikufuru.  [Al-Baqarah: 152]

 

 

Tunajua kwamba kila kheri na shari ni mtihani kwetu, na katika hali zote inatupasa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ili kudhihirisha yakini ya kuamini Qadhwaa na Qadar  Rejea Mlango Wa ‘Maana Na Aina Za Subira’. Na hivo ndivyo ilivyo sifa ya Muumini bali huwa ni jambo la kuwastaajibsha wengineo kwa sifa yake hiyo ya ukamilifu wa iymaan:

 

))عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ، وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ، وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ)) مسلم

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lake ni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake))  [Muslim]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ameahidi kwamba kila mara mja Wake anapomshukuru, Humzidishia neema, na anapokanusha basi ametoa onyo la adhabu kali.

 

 وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

 

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: “Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu); na mkikufuru, basi hakika adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym: 7]

 

 

Na Muislamuu kutokuridhika na majaaliwa ya Allaah, ni aina mojawapo ya kukanusha au kukufuru hukmu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwani hakuna mtihani au msiba unaomsibu mtu isipokuwa kwa amri Yake. Lililo la muhimu kwa mja ni kusalimu amri, kuridhika na kutegemea malipo mema ya duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  baada ya kauli Yake kuhusu kifo cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  wakati walipofadhaika Maswahaba hata wakafikia kutokuamini kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amefariki:

 

 وَمَا مُحَمَّدٌ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ ۚ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ ۚ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللَّـهَ شَيْئًا ۗ وَسَيَجْزِي اللَّـهُ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

Na Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) si yeyote isipokuwa ni Rasuli tu. Wamekwishapita kabla yake Rusuli. Je, akifa au akiuawa mtageuka nyuma ya visigino vyenu (mrudi ukafirini)? Na atakayegeuka nyuma ya visigino vyake, basi hatomdhuru Allaah kitu chochote. Na Allaah Atawalipa wenye kushukuru.

 

  

وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَن تَمُوتَ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ كِتَابًا مُّؤَجَّلًا ۗ وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الْآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا ۚ وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٥﴾ 

Na haiwi kwa nafsi yeyote kufa isipokuwa kwa idhini ya Allaah, imeandikwa muda wake maalumu. Na yeyote anayetaka thawabu za dunia Tutampa katika hizo. Na yeyote anayetaka thawabu za Aakhirah Tutampa katika hizo; na Tutawalipa wanaoshukuru.  [Aal-‘Imraan: 144-145]

 

 

5- Kutokuva Mipaka Ya Shariy’aha Katika Kuombeleza:  

 

 

 Kuombeleza kwa kujipiga mashavuni na kuchana nguo au kulaani wakati, au kupandisha sauti ya kilio na kusema maneno tele na kuojiombea maangamizi n.k. ni miongoni mwa mambo yaliyoharamishwa katika misiba.  

 

 عَنْ عَبْدُ الله ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((لَيْسَ مِنَّا مَنْ ضَرَبَ الْخُدُودَ وَشَقَّ الْجُيُوبَ وَدَعَا بِدَعْوَى الْجَاهِلِيَّةِ)) متفق عليه

 

 Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullahi bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  ((Si miongoni mwetu anayejipiga mashavu, akachana nguo na akaomba maombi ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 Muislamu ana haki ya kubakia katika huzuni isiyozidi siku tatu. Baada ya hapo inampasa kujirudisha katika hali yake ya kawaida ya kimaisha na si kujiwekea masiku ya kuombeleza. Imekatazwa hayo katika masimulizi yafuatayo:

 

 

عَنْ زَيْنَبَ بِنْتِ أَبِي سَلَمَةَ (رضي الله عنهما) قَالَتْ: دَخَلْتُ عَلَى أُمِّ حَبِيبَةَ (رضي الله عنها) زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حِينَ تُوُفِّيَ أَبُوهَا أَبُو سُفْيَانَ بْنُ حَرْبٍ، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فِيهِ صُفْرَةُ خَلُوقٍ، أَوْ غَيْرِهِ،  فَدَهَنَتْ مِنْهُ جَارِيَةً، ثُمَّ مَسَّتْ بِعَارِضَيْهَا . ثُمَّ قَالَتْ: وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ، إِلا عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) قَالَتْ زَيْنَبُ: فَدَخَلْتُ عَلَى زَيْنَبَ بِنْتِ جَحْشٍ (رضي الله عنها) حِينَ تُوُفِّيَ أَخُوهَا، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فَمَسَّتْ مِنْهُ ثُمَّ قَالَتْ: أَمَا وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ إِلاَّ عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Zaynab bint Abi Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: “Niliingia kwa Ummu Habiybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mkewe Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipofiliwa na baba yake Abuu Sufyaan bin Harb. Akaitisha manukato manjano na manukato ya aina nyingine. Akampaka mjakazi wake na akajipaka mashavuni. Kisha akasema: “WaLLaahi sikuwa nina haja ya kujipaka manukato isipokuwa nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema juu ya mimbar: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kumkalia maiti matanga zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe miezi minne na siku kumi)). Zaynab akasema: Kisha nikamwendea Zaynab bint Jahsh (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipofiliwa na ndugu yake. Akaitisha manukato, akajipaka kisha akasema: “WaLLaahi sikuwa nina haja ya manukato, isipokuwa nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho kumkalia maiti matanga zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe miezi mine na siku kum]i)) [Al-Bukhaariy na Muslim

 

 Hayo ni mafunzo bora ya kufuata na tuchukue mfano wa Nabiy Ya’quwb ('Alayhis-Salaam)

 

Pindi ilipomzidi huzuni yake baada ya kupotelewa na mwanawe Yuwsuf kwa miaka mingi:

 

 وَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَىٰ عَلَىٰ يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٨٤﴾

Akajitenga nao, na akasema: “Ee majonzi yangu juu ya Yuwsuf.” Na macho yake yakageuka meupe kutokana na huzuni, naye huku akiwa amezuia ghaidhi za huzuni. [Yuwsuf: 84]

 

 

 

Share