10-Swabrun Jamiyl: Yanayosahilisha Kuvumilia Mitihani

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

10 - Yanayosahilisha Kuvumilia Mitihani

 

 

‘Amali zifuatazo, zitaweza kumsaidia kwa idhini ya Allaah, anayesibiwa na mitihani na huenda zikamfanyia hafifu huzuni zake au maumivu na kila aina ya dhiki zake, na juu ya hivyo akathibitika mtu katika iymaan. Ila yapasa mtu atekeleze kwa yakini na matarijio kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ‘Amali zenyewe zimegawika katika sehemu mbili: (i) ‘Amali Za Kimatendo (ii) ‘Amali za Kimoyo.

 

 

I) ‘Amali Za Kimatendo

 

Ni ‘amali anazotenda mtu kutumia viungo vyake vya mwili kwa kila aina za ‘ibaadah.

 

 

1- Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Asome Qur-aan Kwa Wingi:

 

 Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatueleza kwamba Qur-aan ni shifaa (poza) na rahmah kwa Waumini. Na imethibiti katika Sunnah kwamba Suwrah kadhaa zinatumika kwa Ruqya (kinga na tiba) ya magonjwa, kusahilisha huzuni za misiba, maafa n.k.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَنُنَزِّلُ مِنَ الْقُرْآنِ مَا هُوَ شِفَاءٌ وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ﴿٨٢﴾

Na Tunateremsha katika Qur-aan ambayo ni shifaa na rahmah kwa Waumini; [Al-Israa: 82]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ﴿٤٤﴾

Sema: “Hiyo ni kwa walioamini ni mwongozo na shifaa. [Fusswilat: 44]

 

 

 

2 – Aiyepatwa Mitihani Na Masaibu Azidishie Du’aa

 

Du’aa ni ‘ibaadah pekee inayoweza kugeuza majaaliwa ya Muislamu yanayoandikwa na Malaika Wawili katika Kitabu cha matendo, kama ilivyothibiti katika Hadiyth:

 

عَنْ ثَوْبَانَ (رضي الله عنه)  أن النبي (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((لاَ يَرُدُّ الْقَدَرَ إلاَّ الدُّعَاءُ وَلاَ يَزِيدُ فِي الْعُمُرِ إلاَّ الْبِرُّ وَإِنَّ الْعَبْدَ لَيُحْرَمُ الرِّزْقَ بِالذَّنْبِ يُصِيبُهُ))

 

Kutoka kwa Thawbaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hairudishwi Qadar ila kwa du’aa, wala hauzidishwi umri ila kwa wema, na hakika mja anaharamishiwa rizki kutokana na dhambi aitendayo)) [At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ahmad]

 

Du’aa pia inaondosha kila aina ya shari na balaa:

 

عَنْ مُعَاذٍ (رضي الله عنه) عَنْ رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لَنْ يَنْفَعَ حَذَرٌ مِنْ قَدَرٍ وَلَكِنَّ الدُّعَاءَ يَنْفَعُ مِمَّا نَزَلَ وَمِمَّا لَمْ يَنْزِلْ فَعَلَيْكُمْ بِالدُّعَاءِ عِبَادَ اللَّهِ))

 

 Kutoka kwa Mu’aadh (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Haifai hadhari kutokana na Qadar lakini du’aa inasaidia katika yaliyoteremka na yasiyoteremka, basi juu yenu [jitahidini] kwa du’aa enyi waja wa Allaah))  [Ahmad]

 

 Na Du’aa kadhaa zimethibiti katika Sunnah ambazo Muislamu akizisoma zinamuondoshea huzuni na dhiki, mojawapo ni:

 

 اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي ، وَنُورَ صَدْرِي، وَجلاَءَ حُزْنِي ، وَذَهَابَ هَمِّي

 

 Allaahumma inniy ‘abduka wabnu-‘abdika, wabnu-amatika, naaswiyaatiy biyadika, maadhwin fiyya hukmuka, ‘adlun fiyya qadhwaauka, as-aluka bikullismin huwa Laka, sammayta bihi Nafsaka aw-anzaltahu fiy Kitaabika, aw ‘allamtahu ahadan min khalqika, awis-staatharta bihi fiy ‘ilmil-ghaybi  ‘indaka, an-taj’alal-Qur-aana rabiy’a qalbiy, wanuwra swadriy, wajalaa huzniy, wadhahaaba hammiy

 

 ((Ee Allaah hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako Ulilojiita kwa Nafsi Yako au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe [na kujihusisha kulijua] katika ilimu iliofichika Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu, na sababu ya kuondoka wahka wangu.  [Ahmad (1/391, 452), Al-Haakim (1/509) na ameipa daraja Swahiyh Al-Albaaniy]

 

 

 

 3 – Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Akimbilie Kuomba Maghfirah Na Toba

 

Kwa vile huenda ikawa sababu mojawapo ya mitihani na shari inatokana na madhambi ya mtu anayoyatenda, inahitajika kuomba maghfirah na toba ili kujikinga nayo, kwani kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):    

 

وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿٣٣﴾

Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu hali wao wanaomba maghfirah. [Al-Anfaal: 33]

 

Juu ya hivyo kuomba maghfirah na toba kuna faida nyingi kwa Muislamu kama zilivyothibiti katika Qur-aan na Sunnah. Manabii walipowalingania watu wao waliwanasihi waombe maghfirah na toba ili Allaah   Awajaalie maisha mazuri yenye manufaa, na Awaruzuku neema Zake, na Awazidishie nguvu [Huwd: 2-3, 50-52, Nuwh: 10-12]

 

 

  4- Aliyepatwa Na Mitihani Na Masaibu Akimbilie Swalaah

 

Imepokelewa kutoka kwa Hudhayfah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba:

 

 ((كاَنَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وآله وسلم إِذا حَزَبَهُ أمْر فَزِعَ إِلى الصَّلاَة)) أخرجه أبو داود وحسنه الألباني في صحيح أبي داود 1319 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akizidiwa na jambo la dhiki hukimbilia kuswali.”  [Abu Daawuwd na ameipa daraja ya Hasan Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Abi Daawuwd (1319)]

 

 Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaamrisha kutafuata msaada kutokana na Swalaah na subira:

 

 وَاسْتَعِينُوا بِالصَّبْرِ وَالصَّلَاةِ ۚ وَإِنَّهَا لَكَبِيرَةٌ إِلَّا عَلَى الْخَاشِعِينَ ﴿٤٥﴾

Na tafuteni msaada kupitia subira na Swalaah; na hakika hilo ni kubwa isipokuwa kwa wanyenyekevu.  [Al-Baqarah: 45]

 

 

Imesemakana kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) alipokuwa safarini akapata habari ya kifo cha kaka yake, alisema neno la istirjaa’ (Innaa-liLLaahi wa innaa Ilyahi Raaji’wn) kisha akaswali rakaa mbili akakaa kitako kirefu, kisha akainuka kuendelea safari yake huku akisoma Aayah hiyo tukufu.

 

 

 

 5 – Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Amdhukuru Allaah Hususan Kwa Tasbiyh

 

 

 Kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kila aina ya dhikru-Allaah ambazo zimethibiti katika Qur-aan na Sunnah. Mfano kumdhukuru kwa Adhkaar ambazo pindi Muislamu anapopatwa janga na balaa, wahka na huzuni; adkhaar hizo zinapatikana katika kitabu cha Hiswnul-Muslim.  Mfano mojawapo ni du’aa ya Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam):

 

 لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ 

Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako), hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.  [At-Tirmidhiy, Ahmad, Al-Haakim (Du’aa ya Dhan-Nuwn na pia imo katika Qur-aan Al-Anbiyaa: (87)]

 

 Du’aa hiyo imethibiti kwamba anayeisoma hutakabaliwa haja yake, na pia huondokewa na dhiki au shida zake kwani hivyo ndivyo alivyoomba Nabiy Yuwnus kwa muda masiku au miezi au miaka mpaka akatolewa kwenye dhiki pindi alipokuwa katika kiza tumboni mwa samaki:

 

 وَذَا النُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَاضِبًا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقْدِرَ عَلَيْهِ فَنَادَىٰ فِي الظُّلُمَاتِ أَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾

Na Dhan-Nuwn (Yuwnus) alipoondoka akiwa ameghadhibika, akadhani kwamba Hatutamdhikisha; akaita katika kiza kwamba: “Hapana muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako), hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.”

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akasema:  

 

فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْغَمِّ ۚ وَكَذَٰلِكَ نُنجِي الْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾

Basi Tukamuitikia na Tukamuokoa kutokana na ghamu. Na hivyo ndivyo Tuwaokowavyo Waumini. [Al-Anbiyaa: 87-88]

 

Na pindi makafiri wa Makkah walimpotia mtihanini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumkanusha na kumfanyia kila aina ya maudhi, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimuamrisha kuswali na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mchana na usiku kwa kuomba maghfirah, kumsabihi, kumhimidi, kumpwekesha, kumtukuza n.k. ili imhafifishie dhiki zake.

 

Ametaja hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah zifuatazo:

 

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ﴿٩٧﴾

Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema.

  

فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ﴿٩٨﴾

Basi Sabbih kwa Himidi za Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu.

   

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr: 97-99]

 

Na pia:

 

 فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ ﴿١٣٠﴾

Basi subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla kukuchwa kwake. Na katika nyakati za usiku pia sabbih na katikati ya mchana huenda ukapata ya kukuridhisha.  [Twahaa: 130]

 

Na pia:

 

فَاصْبِرْ إِنَّ وَعْدَ اللَّـهِ حَقٌّ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ بِالْعَشِيِّ وَالْإِبْكَارِ﴿٥٥﴾

Basi vuta subira (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), hakika ahadi ya Allaah ni haki, na omba maghfirah kwa dhambi zako, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako jioni na asubuhi.  [Ghaafir: 55]

 

Na:

 

 فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ الْغُرُوبِ﴿٣٩﴾

Subiri juu ya yale wanayoyasema, na sabbih kwa Himidi za Rabb wako kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa.

 

 

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَأَدْبَارَ السُّجُودِ﴿٤٠﴾

Na katika usiku Msabbih na baada ya kusujudu. [Qaaf: 39-40]

 

Na pia:

 

وَاصْبِرْ لِحُكْمِ رَبِّكَ فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٤٨﴾

Na subiri (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa hukumu ya Rabb wako, kwani hakika wewe uko chini ya Macho Yetu. Na sabbih kwa Himidi za Rabb wako, wakati unapoinuka.

  

وَمِنَ اللَّيْلِ فَسَبِّحْهُ وَإِدْبَارَ النُّجُومِ ﴿٤٩﴾

Na katika usiku Msabbih na zinapokuchwa nyota. [At-Twuur: 48-49]

 

 

 

Kumtakasa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa tasbiyh ni kusema:

 سُـبْحانَ الله 

 

Subhaana-Allaah

 

au

سُبْحانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ سُبْحَانَ اللهِ العَظِيمِ

Subhaana Allaahi Wabihamdihi Subhaana Allaahil-’Adhwiym

Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake, Utakasifu ni wa Allaah Aliye Mtukufu

 

 

Na Kumhimidi ni:

الْحَمْدُ لِلّه

AlhamduliLlaah

 

 au

 

سُبْحَانَ اللهِ، والحَمْدُ للهِ، وَ لاَ إِلَهَ إلاَّ اللهُ واللهُ أَكْبَرُ

Subhaana Allaah, WalhamduliLLaah, wa laa ilaaha illa Allaah, wa Allaahu Akbar

Utakasifu ni wa Allaah na Himdi Anastahiki Allaah, na hapana muabudiwa wa haki  ila ni Allaah, na Allaah ni Mkubwa.

 

 

6 – Aliyepatwa Mitihani Na Masaibu Atoe Sadaka

 

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Umaamah Al-Baahiliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

   دَاوَوُا مَرْضَاكُمْ بِالصَّدَقَة

 

 ((Watibuni wagonjwa wenu kwa sadaka)) [Hadiyth Hasan -  Swahiyh Al-Jaami’ (3358)]

 

Na kutoa sadaka ni ‘amali inayohitaji subira kwa kutegemea pia malipo mema duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ ۗ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٩٦﴾

Mlivyo navyo nyinyi vinatoweka, na vilioko kwa Allaah ni vya kubakia. Na kwa yakini Tutawalipa wale waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda. [An-Nahl: 96]

 

 

 

II) ‘Amali Za Kimoyo

 

 

Ni ‘amali za kutafakari, kuzingatia na kushukuru, ambazo zitamliwaza aliyefikwa na mitihani kwa kutaraji malipo mema.

 

 

 1- Aliyepatwa Na Mitihani Na Masaibu Hulipwa Malipo ya ‘Ibaadah Alizokuwa Akizitenda Pindi Alipokuwa Katika Siha:

 

Muumini atafakari kwamba anapofikwa na maradhi akawa hawezi kutekeleza ‘ibaadah zake kama alivyokuwa katika hali ya uzima, hupata thawabu zake vile vile kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Muadilifu kwa kuwa Anajua kwamba lau si kusibiwa na maradhi, Muislamu huyo angeliendeleza ‘ibaadah zake, basi Humpa ujira wake vile vile na juu ya hivyo hupata ujira zaidi wa subira duniani na Aakhirah.

 

 عن أبي موسى الأشعري  (رضي الله عنه)  عن النَّبي (صلى الله عليه وآله وسلم) قال: (( إِذَا مَرِضَ الْعَبْدُ أَوْ سَافَرَ كُتِبَ لَهُ مِثْلُ مَا كَانَ يَعْمَلُ مُقِيمًا صَحِيحًا)) البخاري

 

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja anapopatwa maradhi, au akiwa safarini, huandikiwa (thawabu) kama alivyokuwa akitenda akiwa mkaazi na mwenye afya)) [Al-Bukhaariy]

 

وعَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه)  أَنَّ رَسُولَ (صلى الله عليه وآله وسلم) قال: إِذَا ابْتَلَى اللَّهُ الْعَبْدَ الْمُسْلِمَ بِبَلاَءٍ فِي جَسَدِهِ قَالَ لِلْمَلَكِ : اكْتُبْ لَهُ صَالِحَ عَمَلِهِ الَّذِي كَانَ يَعْمَلُ، فَإِنْ شَفَاهُ غَسَلَهُ وَطَهَّرَهُ، وَإِنْ قَبَضَهُ غَفَرَ لَهُ وَرَحِمَهُ)  رواه أحمد في "المسند" (21/268) قال الألباني: حسن صحيح .

 

 Na Imepokelewa kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Akimjaribu mja Muislamu kwa kumpa mtihani katika mwili wake, Humwambia Malaika: “Mwandikie amali zake njema alizokuwa akizitenda.”  Akimpa shifaa (Akimponyesha) Humwosha na kumtakasa, na Akichukua roho yake, Humghufuria na Akamrehemu)) [Ahmad katika Musnad na amesema Al-Albaani: Hasan Swahiyh]

 

 

2 – Mwenye Kupatwa Mitihani Na Masaibu Ategemee Malipo Ya Aakhirah:

 

Fadhila tele zimethibiti kwa anayevumilia mitihani kwamba malipo yake ni mema yasiyohesabika duniani na Aakhirah [Rejea Mlango Wa: ‘Fadhila Za Subira Katika Qur-aan’ na pia, ‘Subira Katika Mitihani Kwa Ujumla’] Juu ya hayo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameahidi Jannah (Pepo) ya kudumu iliyojaa neema:

 

 أُولَـٰئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا وَيُلَقَّوْنَ فِيهَا تَحِيَّةً وَسَلَامًا ﴿٧٥﴾

Hao ndio watakaolipwa maghorofa ya juu (Jannah) kwa kuwa walisubiri, na watapokelewa humo kwa maamkizi na amani.

 

خَالِدِينَ فِيهَا ۚ حَسُنَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴿٧٦﴾

Ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje wa mahali pa kustakiri na makazi ya kushi daima. [Al-Furqaan: 75-76]

 

 

 

3 – ‘Ibaadah Za Aliyepatwa Na Mitihani Na Masaibu Huwa Za Dhati:

 

Muumini wa kweli anaposibiwa na mitihani na janga, hujikurubisha zaidi kwa Rabb wake kwa kila aina ya ‘ibaadah, na hapo hata du’aa zake huwa ni zile za dhati ndani ya moyo wake uliokuwa na huzuni na dhiki. Na hapo ndipo inapothibiti kumuabudu na kumtaka msaada Pekee Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

 Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada. [Al-Faatihah: 5]

 

 

 

4 - Mitihani Na Masaibu Ni Kupendwa Na Allaah Kwa Kutanguliziwa Adhabu

 

Tafakari ndugu Muislamu uliyefikwa na mitihani, na shukuru kwamba masaibu yamekufikia ukiwa katika maisha ya dunia; basi omba upasi mtihani wa Aakhirah kwani huko kuna shida na dhiki zaidi.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

 وَلَنُذِيقَنَّهُم مِّنَ الْعَذَابِ الْأَدْنَىٰ دُونَ الْعَذَابِ الْأَكْبَرِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٢١﴾

Na bila shaka Tutawaonjesha adhabu ndogo kabla ya adhabu kubwa huenda wakarejea (kutubia). [As-Sajdah: 21]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametubashiria hilo:

 

عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) قَال:َ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم): َ(( إِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الْخَيْرَ عَجَّلَ لَهُ الْعُقُوبَةَ فِي الدُّنْيَا وَإِذَا أَرَادَ اللَّهُ بِعَبْدِهِ الشَّرَّ أَمْسَكَ عَنْهُ بِذَنْبِهِ حَتَّى يُوَافِيَ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) وَ قال النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ عِظَمَ الْجَزَاءِ مَعَ عِظَمِ الْبَلاَءِ وَإِنَّ اللَّهَ إِذَا أَحَبَّ قَوْمًا ابْتَلاَهُمْ فَمَنْ رَضِيَ فَلَهُ الرِّضَا وَمَنْ سَخِطَ فَلَهُ السَّخَطُ)) رواه الترمذي وقال حديث حسن

 

Kutoka kwa Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anapompendelea mja Wake kheri, Humharakishia adhabu duniani. Na Allaah Anapomtakia mja Wake shari Humzuilia dhambi zake hata Amlipe Siku ya Qiyaamah)). Na amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hakika malipo makubwa kabisa yapo pamoja na mtihani mkubwa, na hakika Allaah Anapopenda watu Huwapa mtihani. Basi atakayeridhika atapata radhi (za Allaah) na atakayechukia atapata ghadhabu)) [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]

 

 

 

5 – Katika Mitihani na Masaibu, Mtazame Aliye Chini Yako

 

Wana Aadam hawalingani sawa katika neema walizojaaliwa. Basi katika hali ya mitihani na masaibu, Muumini amtazame mwenzake aliye na shida au hali mbaya zaidi kuliko yeye. Kufanya hivyo kutamkumbusha kuwa yeye yuko katika hali bora zaidi na yuko katika neema kuliko nduguye aliye na hali ngumu zaidi. Mfano mgonjwa anapokwenda hospitali kutibiwa, huenda akakuta huko wagonjwa walio na maradhi zaidi kuliko maradhi yake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha hayo: 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صلى الله عليه وآله وسلم):  ((انْظُرُوا إِلَى مَنْ هُوَ أَسْفَلَ مِنْكُمْ، وَلاَ تَنْظُرُوا إِلَى مَنْ هُوَ فَوْقَكُمْ فَإِنَّهُ أَجْدَرُ أَنْ لاَ تَزْدَرُوا نِعْمَةَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ)) متفق عليه وهذا لفظ مسلم.

 وفي رواية البخاري: ((إِذَا نَظَرَ أَحَدُكُمْ إِلَى مَنْ فُضِّلَ عَلَيْهِ فِي الْمَالِ وَالْخَلْقِ فَلْيَنْظُرْ إِلَى مَنْ هُوَ أَسْفَلَ مِنْهُ))

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mtazameni aliye chini yenu wala msimtazame aliye juu yenu kwani (kufanya hivyo) ni haki zaidi msije mkazidharau neema za Allaah juu yenu)) [Al-Bukhaariy na Muslim], hii lafdh ya Muslim.

 

Na katika riwaayah ya Al-Bukhaariy: ((Anapomtazama mmoja wenu aliyefadhilishwa zaidi kwa mali na umbo basi amtazame aliye chini yake))

 

 

 

6 – Mitihani Na Masaibu Humtoa Mtu Kutoka Kwenye Kughafilika Na Huwa Ni Sababu Ya Kuhidika:

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuhusu walioghafilika na dunia wakasahau Aakhirah:

 

إِنَّ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا وَرَضُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَاطْمَأَنُّوا بِهَا وَالَّذِينَ هُمْ عَنْ آيَاتِنَا غَافِلُونَ﴿٧﴾

Hakika wale wasiotaraji kukutana Nasi, na wakaridhika na uhai wa dunia na wakakinaika nayo, na wale ambao wanaghafilika na Aayaat Zetu   [Yuwnus: 7]

 

Anawaonya kwamba hao watakuwa katika maisha ya dhiki na shida na Atawasahaulia mbali kama wao walivyomsahau.

 

 وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾

 “Na atakayejitenga na ukumbusho Wangu basi hakika atapata maisha ya dhiki, na Tutamfufua Siku ya Qiyaamah hali akiwa kipofu.”

 

قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾

Atasema: “Rabb   wangu! Kwa nini Umenifufua kipofu, na hali nilikuwa naona?”

 

 قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا ۖ وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾

 (Allaah) Atasema: “Hivyo ndivyo, zilikufikia Aayaat Zetu ukazisahau   na kadhaalika leo umesahauliwa.”

  

وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي مَنْ أَسْرَفَ وَلَمْ يُؤْمِن بِآيَاتِ رَبِّهِ ۚ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَدُّ وَأَبْقَىٰ ﴿١٢٧﴾

Na kadhaalika Tutakavyomlipa yule anayevuka mipaka na asiamini Aayaat za Rabb wake. Na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni kali zaidi na ni ya kudumu zaidi.  [Twaahaa: 124-127]

 

 

Aghlabu Muislamu anayekuwa katika kughafilika kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kushughulishwa na anasa na starehe za dunia, kisha pindi akipatwa na masaibu, huwa ni sababu ya kumrudisha kwa Rabb wake akatanabahi kwamba yaliyokuwa yakimshughulisha hayatomfaa lolote. Kisha hutekeleza ‘ibaadah zake ipasavyo na hapo basi ndipo hujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akatambua ladha ya ‘ibaadah hizo na zikamzidishia iymaan   na mapenzi ya Rabb wake, na kumpenda zaidi Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini Yake tukufu. Lakini nasaha kwa kila Muislamu aliyeghafilika akawa mbali na kumdhukuru Allaah kwamba leo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekupa fursa ya kukutanabahisha ukarudi Kwake baada ya mitihani na misiba. Basi tahadhari usije kurudi katika hali ya mwanzo. Kumbuka kwamba wengine walioaga dunia wakiwa katika mighafiliko ya dunia wameondoka patupu bila ya kuchuma ‘amali za kumtosheleza kwenye safari ndefu ya Aakhiray isiyoepukika.

 

Wewe bado una fursa kwa kuwa umo katika makazi ya kutubia na kutenda ‘amali njema. Kwa hiyo mshukuru Rabb wako kwa kukujaalia mitihani iliyokuzindua kutoka kizani na sasa umo katika mwamko na nuru. Zingatia hayo ndugu Muislamu yasije kukufikia mauti ukatamani kurudishwa duniani ujirekebishe. Majuto utakayoyadhihirisha wakati huo hayatafaa kitu bali utajibiwa:

 

كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾

 

 “Laa hasha!” Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu.  Na nyuma yao kuna barzakh mpaka Siku watakayofufuliwa. [Al-Muuminuwn: 100]

 

 

7 – Mitihani Na Masaibu Ni Hikma Ya Allaah

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mwenye Hikma na Mjuzi. Anapomsibu mja Wake mitihani huenda ikawa ni kheri yake (mja) kama Anavyosema:

 

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ ۗ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٢١٦﴾

 

Na asaa mkachukia jambo na hali lenyewe ni kheri kwenu. Na asaa mkapenda jambo na hali lenyewe ni la shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui. [Al-Baqarah: 216]

 

 

Rejea kisa cha Nabiy Muwsa ('Alayhis-Salaam)  na Khidhr katika Suwratul-Kahf ambacho kimejaa Hikma za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)    [Al-Kahf: 60-82]

 

 

 

Share