11-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Haajar Mama Yake Nabiy Ismaa'iyl
11 - Subira Za Wanawake Wema Wa Awali: Haajar Mama Yake Nabiy Ismaa’iyl
Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) alihama Shaam kuelekea Makkah akiwa pamoja na mkewe Haajar na mwanawe Ismaa’iyl. Walipofika aliwaacha katika bonde kame, kavu, na lisilokuwa tambarare. Hapakuwa na chakula wala maji, na hapakuwa na watu wanoishi.
Haajar alitawakali kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na akavuta subira juu ya kwamba alikuwa na mtoto mchanga aliyekuwa bado akimnyonyesha. Pindi Nabiy Ibraahiym alipoondoka na kuwaacha bondeni Makkah, Haajar alimuuliza: “Ee Ibraahiym, unakwenda wapi na kutuacha katika bonde lisokuwa na watu au chochote (cha kutuwezesha kuishi)?” Akakariri swali lake mara kadhaa, lakini Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) hakumjibu wala hakutazama nyuma kwani hivyo ndivyo alivyoamrishwa na Rabb Wake, na hakutaka kufanya kinyume chake. Haajar mwishowe akamuuliza: “Je Allaah Amekuamrisha kufanya hivyo?” Akajibu: “Ndio”. Jibu hilo lilimtosheleza Haajar kwani alijua kwamba ni hukmu ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akasema: “Basi nenda, hakika Allaah Hatatutekeleza” [Al-Bukhaariy]
Nabiy Ibraahiym alimuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
رَّبَّنَا إِنِّي أَسْكَنتُ مِن ذُرِّيَّتِي بِوَادٍ غَيْرِ ذِي زَرْعٍ عِندَ بَيْتِكَ الْمُحَرَّمِ رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَشْكُرُونَ ﴿٣٧﴾
“Rabb wetu! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria wangu katika bonde lisilokuwa na mmea wowote, kwenye Nyumba Yako Tukufu. Rabb wetu, ili wasimamishe Swalaah na Ujaalie nyoyo za watu zielekee kwao na Uwaruzuku mazao ili wapate kushukuru.” [Ibraahiym: 37]
Baada ya Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) kuondoka, haukupita muda Ismaa’iyl akaanza kulia kwa njaa na kiu, hapo Haajar akaanza kutafuta maji mara akitembea kwa kasi, mara akikimbia baina ya majabali mawili ya Swafaa na Marwah huku akiomba du’aa na kumdhukuru Rabb wake. Alikaribia kukata tamaa kupata chakula au maji, mara akasikia sauti inayovumavuma. Hapo ndipo alipokuja Jibriyl ('Alayhis-Salaam) akabubujiwa maji ya zamzam kwa amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Ndege wakaanza kuzunguka katika dimbwi la Zamzam, na watu wa msafara wakatambua kwamba kuna maji, wakayafuata na ndipo wakaweka makazi yao. Hao waliokuwa ni watu katika kabila ya Jurhum waliokuwa safarini kutoka Yemen. Wakabakia hapo, na Haajar na mwanawe wakawa ni wamiliki wa maji hayo katika mji huo mtukufu wa Makkah. Wakaishi nao hadi Ismaa’iyl alipokuwa mkubwa akaoa mwanamke kutoka kabila hilo. Na hapo ndipo kizazi cha Nabiy Ismaa’iyl kilipochipuka hadi kufikia kuzaliwa kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Hizo ni miongoni mwa fadhila kuu kabisa za subira ya Haajar. Juu ya hivyo, ‘ibaadah ya Sa’y baina ya Swafaah na Marwah inatekelezwa na idadi isiyohesabika ya Waislamu tokea zama za kale mpaka leo na itaendelea mpaka Siku ya Qiyaamah, na thawabu zake zikimfikia Haajar.