15-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maswahaba - Familia Ya Yaasir (Radhwiya Allaahu 'anhum)
15- Subira Za Maswahaba - Familia Ya Yaasir (Radhwiya Allaahu ‘anhum)
Yaasir na ndugu yake ‘Abdullaah (ambao asili yao ni kutoka Yemen), na Summayyah ambaye ni mke wa Yaasir, na mtoto wao ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kuingia katika Dini ya Kiislamu. Walianza kupata kila aina ya mateso na adhabu lakini nuru ya Uislamu iliyoingia katika nyoyo zao, iliwafanya wastahamili mitihani yote iliyowasibu. Walikuwa wote watatu; Yaasir, ‘Ammaar na Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhum) wakitolewa nje wakati wa jua kali sana, wakipelekwa jangwani na kupewa kila aina ya adhabu. Wakati huo Waislam walikuwa bado wachache sana na hawakuwa na nguvu za kuweza kujitetea. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akipita chini ya nyumba yao na kuwasikia wakiadhibiwa, alikuwa akiwaombea du’aa. Siku moja ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Ee Rasuli wa Allaah, adhabu tunayoipata hivi sasa imepindukia mipaka." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Kuweni na subira enyi familia ya Yaasir, hakika ahadi yenu [jazaa yenu] ni Jannah)) ‘Amru bin Maymun (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Washirikina walikuwa wakiuunguza mkono wa Yaasir, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akipita kila siku na kuushika mkono huo huku akisema: ((Ee moto kuwa baridi na salama juu ya ‘Ammaar, kama ulivyokuwa baridi na salama juu ya Ibraahiym)).
Bibi Sumayyah (Radhhwiya Allaahu ‘anhaa) pamoja na mumewe, mtoto wao na Waislamu wengi wa mwanzo waliweza kuvumilia tabu nyingi na mateso mengi sana kwa sababu tu walitegemea malipo mema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kutokana na iymaan zilizothibiti ndani ya nyoyo zao na baada ya kutambua kuwa hiyo ndiyo njia ya pekee itakayomletea mtu maisha matukufu hapa duniani na kesho Aakhirah, waliridhika kuzipoteza roho zao kwa ajili ya kupata radhi za Rabb wao.
Sumayyah bint Khubat alijulikana kwa umaarufu wake (Ummu ‘Ammaar) ni mtu wa mwanzo kufa shahidi kwa ajili ya Uislamu. Siku moja Abuu Jahal alimuingilia Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kuanza kumpiga kwa mateke na magumi huku akimtaka amtukane Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na awatukuze miungu ya washirikina wa ki-Quraysh. Lakini Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alistahamili adhabu yote hiyo huku akisema: “Ahadun Ahad”. Neno hilo lilizidi kumtia uchungu Abuu Jahl akawa anaendelea kumpiga Bi Sumayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) mpaka akafariki. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposikia hayo alisikia uchungu sana, lakini hakuwa na uwezo wa kufanya lolote mbele ya nguvu za makafiri hao, na kwa ajili hiyo akawataka watu wake wahamie nchi ya Uhabeshi (Ethiopia).
Ama ‘Ammaar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) siku moja aliteswa sana na makafiri wakamtaka amtukane Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na walimwekea kitisho kuwa watamuua. Ikambidi awadanganye kwamba amerudi katika dini yao akamtukana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili wasimtese zaidi. Aliporudi kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea juu ya yote hayo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza: ((Lakini vipi ndani ya nafsi yako unajionaje?)) ‘Ammaar akamwambia: “Iymaan imetulia ndani yake”. Hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Kama watarudia tena basi na wewe rudia)).
Ndipo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipoteremesha kauli Yake:
مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿١٠٦﴾
Atakayemkufuru Allaah baada ya iymaan yake - isipokuwa yule aliyekirihishwa (kukanusha) na huku moyo wake umetua juu ya iymaan - lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu. [An-Nahl: 106]