14-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Maryam Bint ‘Imraan Mama Yake Nabiy 'Iysaa
14 - Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Maryam Bint ‘Imraan Mama Yake Nabiy ‘Iysaa
Subira yake ilikuwa ni katika utiifu ambayo ni subira ngumu kabisa kama tulivyotangulia kutaja. Mama yake Hannah bint Faaqudhw alitamani apate mwana wa kiume ili awe msimamizi wa Baytul-Maqdis [Msikiti ulioko Quds, Palestina]. Lakini alijaaliwa mtoto wa kike, akamwita ‘Maryam’. Akalelewa na mjomba wake Nabiy Zakariyyah ('Alayhis-Salaam). Maryam akawa mtiifu, mwenye taqwa ya hali ya juu, mwenye kufanya ‘ibaadah mchana na usiku.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akawatuma Malaika wambashirie:
وَإِذْ قَالَتِ الْمَلَائِكَةُ يَا مَرْيَمُ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَاكِ وَطَهَّرَكِ وَاصْطَفَاكِ عَلَىٰ نِسَاءِ الْعَالَمِينَ ﴿٤٢﴾
Na pale Malaika waliposema: “Ee Maryam! Hakika Allaah Amekuteua na Amekutakasa na Amekukhitari juu ya wanawake wa walimwengu.” [Aal-‘Imraan: 42]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemteua Maryam kwa sababu ya kumtumikia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kwa sababu ya sitara, heshima na umaasumu wake. Pia kwa sababu ya kuthibitika kwake katika yakini. Akapata fadhila za kuwa ni miongoni mwa wanawake wanne walio bora kabisa ulimwenguni Taz. Hadiyth katika Subira ya Aasiyah.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema kuwa Malaika walimuamrisha Maryam akithirishe ‘ibaadah zake na azidishe unyenyekevu, na azidishe kujisalimisha, kusujudu na kurukuu n.k.
يَا مَرْيَمُ اقْنُتِي لِرَبِّكِ وَاسْجُدِي وَارْكَعِي مَعَ الرَّاكِعِينَ ﴿٤٣﴾
“Ee Maryam! Kuwa mtiifu kwa Rabb wako, na sujudu, na rukuu pamoja na wanaorukuu.” [Aal-‘Imraan: 43]
Maryam aliipokea amri hiyo akazidi kuwa katika subira ya utiifu ili adiriki jambo Alilohukumiwa na Allaah lie ni mtihani wake. Ulikuwa ni mtihani mkubwa mno, lakini ulimpatia daraja tukufu duniani na Aakhirah kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alionyesha Miujiza Yake na Uwezo Wake wa kumuumba mwana tumboni mwake bila ya kuingiliwa na mwanamume. Akashika mimba baada ya kubashiriwa na Jibriyl ('Alayhis-Salaam) akaridhika na majaaliwa hayo. Ila alitambua kuwa utakuwa ni mtihani mkubwa kwake kumzaa mtoto bila ya kuolewa. Akahofia maudhi ya watu kwa maneno na dhana zao mbaya, jambo ambalo lilihitajia pia subira ya hali ya juu. Aliposhikwa na uchungu uliompeleka katika shina la mtende, alisema:
يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَـٰذَا وَكُنتُ نَسْيًا مَّنسِيًّا ﴿٢٣﴾
“Laiti ningelikufa kabla ya haya na nikawa wa kusahauliwa, aliyesahauliwa kabisa!” [Maryam: 23]
Kwa maana: “Natamani nisingelikuwa nimeumbwa nikawa si chochote” [Kauli ya Ibn ‘Abbaas katika tafsiyr ya Ibn Kathiyr]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamtuliza khofu yake na sikitiko lake na Akampooza:
فَنَادَاهَا مِن تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا ﴿٢٤﴾
Lakini (muitaji) akamwita kutoka chini yake kwamba: “Usihuzunike! Rabb wako Amekwishakufanyia kijito cha maji.”
وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا ﴿٢٥﴾
“Na tingisha kwako shina na mtende, litakuangushia tende ziloiva zilizotayari kuchumwa.”
فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا ۖ فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا﴿٢٦﴾
“Basi kula na kunywa na litue jicho lako. Na utakapokutana na mtu yeyote basi sema: Hakika mimi nimeweka nadhiri ya swawm kwa Ar-Rahmaan hivyo leo sitomsemesha mtu yeyote.” [Maryam: 24-26]
Khofu yake ilihakiki baada ya kumzaa ‘Iysaa ('Alayhis-Salaam) na alipokuwa amembeba mbele ya watu wake wakadhihirisha dhana zao alizozikhofia:
فَأَتَتْ بِهِ قَوْمَهَا تَحْمِلُهُ ۖ قَالُوا يَا مَرْيَمُ لَقَدْ جِئْتِ شَيْئًا فَرِيًّا ﴿٢٧﴾
Akawafikia watu wake akiwa amembeba (mtoto); wakasema: “Ee Maryam! Kwa yakini umeleta jambo lisilopata kusikika, kuu na ovu mno.
يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا ﴿٢٨﴾
“Ee dada wa Haaruwn! Hakuwa baba yako mtu muovu, na wala hakuwa mama yako kahaba.” [Maryam: 27-28]
Hali ikawa kama zinavyoendelea Aayah:
فَأَشَارَتْ إِلَيْهِ ۖ قَالُوا كَيْفَ نُكَلِّمُ مَن كَانَ فِي الْمَهْدِ صَبِيًّا ﴿٢٩﴾
Akamuashiria. Wakasema: “Vipi tuseme na aliye kwenye susu, bado mtoto?”
قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾
(Mtoto) Akasema: “Hakika mimi ni mja wa Allaah; Amenipa Kitabu (Injiyl) na Amenijaalia kuwa Nabiy.”
وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾
“Na Amenijaalia kuwa mwenye kubarikiwa popote nitakapokuweko, na Ameniusia Swalaah na Zakaah madamu niko hai.”
وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾
“Na niwe mtiifu kwa mama yangu na wala Hakunijaalia kuwa jabari, muovu.”
وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا ﴿٣٣﴾
“Na amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa hai.” [Maryam: 29-33]
Juu ya hivyo, dhana, tuhuma na uzushi wa watu wake uliendelea, lakini Maryam aliendelea kuvuta subira akamlea mwanawe ambaye alikuwa ni fadhila kuu juu yake kwamba alikuwa ni miongoni mwa Manabii na Rusuli Watukufu. Na subira hiyo aliihitaji pia mwanawe Nabiy ‘Iyssa ('Alayhis-Salaam) ambaye naye alizuliwa ya kuzuliwa. Lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anathibitisha ukweli wake kuwa ‘Iysaa ni mja Wake:
ذَٰلِكَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ ۚ قَوْلَ الْحَقِّ الَّذِي فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٣٤﴾
Huyo ndiye ‘Iysaa mwana wa Maryam! Kauli ya haki ambayo wanaitilia shaka.
مَا كَانَ لِلَّـهِ أَن يَتَّخِذَ مِن وَلَدٍ ۖ سُبْحَانَهُ ۚ إِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٣٥﴾
Haiwi kwa Allaah kamwe Ajichukulie mwana yeyote. Subhaanah! (Utakasifu ni Wake). Anapokidhia jambo basi huliambia: “Kun” (Kuwa!) nalo linakuwa!
وَإِنَّ اللَّـهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٣٦﴾
(Nabiy ‘Iysaa akasema): “Na kwamba hakika Allaah ni Rabb wangu, na Rabb wenu, basi mwabuduni Yeye (Pekee). Hii ndio njia iliyonyooka.” [Maryam: 34-36]