13-Swabrun Jamiyl: Subira Za Wanawake Wema Wa Awali - Aasiyah Aliyekuwa Mke Wa Fir’awn
13- Subira Za Wanawake Wema Wa Awali: Aasiyah Aliyekuwa Mke Wa Fir’awn
Aasiyah aliishi katika Qasri la fakhari, lilojaa kila aina ya starehe, wakiwemo watumishi tele, na alipata kila alichokitamani. Alikuwa mke wa Fir’awn, Fir’awn aliyejivuna na kutakabari na akavuka mipaka kujifanya yeye ni muabudiwa. Aliwaamrisha watu wake wamwabudu na akawaekea vitisho pindi wakimuasi.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alimtia ilhamu Aasiyah ampende Muwsa pale alipoletewa kisanduku kilichopatikana katika mto wa Nile ambacho ndani yake alikuwemo Muwsaa akiwa mtoto mchanga. Mtoto huyo alikuwa na nuru usoni mwake, na alimuathiri mno hadi akamuomba Fir’awn asimuue bali wamfanye mwana wao. Akamlea malezi mema yakajengeka mapenzi ya mama na mwana.
Muwsaa alipopewa risala (ujumbe) wa kumlingania Fir’awn katika Tawhiyd, Aasiyah alimwamini hapo hapo. Lakini alificha kwanza iymaan yake kwa kumkhofu Fir’awn. Haukufika muda alidhihirisha Uislamu wake. Fir’awn alimtaka arudi katika dini yake ya kumwabudu yeye, akamwekea vitisho na kumtahadharisha adhabu kali. Lakini alithibitika katika iymaan yake ya kufuata haki. Fir’awn akataka ushauri kwa Haamaan (mawaziri wake) wakamshauri amuue Aasiyah. Wakamfunga mikono na miguu yake wakamweka juani. Fir’awn akaamrisha liletwe jiwe kubwa kabisa. Kisha aulizwe Aasiyah akiwa katika adhabu ya jua na kiu kikali, kwamba nani mwabudiwa wake? Atakapomkubali yeye basi yu angali mke wake, laa sivyo wampige nalo jiwe kumuulia mbali. Aasiyah alithibitika katika iymaan yake, hakujali kuyaacha maisha ya ufalme aliyokuwa akiishi katika Qasri ambako kulijaa kila aina za starehe. Alilojali zaidi ni kupokea haki aliyokuja nayo Muwsaa na ndugye Haaruwn ya kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee, na kupata radhi Zake atakapokutana Naye Peponi. Katika hali hiyo ya kuadhibiwa na kukaribia mauti, hakutaharuki wala kuhamanika wala kupapatika bali alivuta subira huku akiomba:
رَبِّ ابْنِ لِي عِندَكَ بَيْتًا فِي الْجَنَّةِ وَنَجِّنِي مِن فِرْعَوْنَ وَعَمَلِهِ وَنَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ﴿١١﴾
“Rabb wangu! Nijengee nyuma Kwako kwenye Jannah na niokoe na Fir’awn na vitendo vyake na niokoe na watu madhalimu.” [At-Tahriym: 11]
Watu wa Fir’awn walipomjia Aasiyah, macho yake yalikuwa yakitazama nyumba yake ya Peponi aliyokwishaahidiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Akapigwa jiwe, roho yake ikatoka akiwa katika Tawhiyd ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Iymaan na subira yake ya hali ya juu imemstahiki kuwa ni miongoni mwa wanawake wanne waliobashiriwa Jannah kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((أَفْضَلُ نِسَاءِ أَهْلِ الْجَنَّةِ خَدِيجَةُ بِنْتُ خُوَيْلِدٍ وَفَاطِمَةُ بِنْتُ مُحَمَّدٍ وَمَرْيَمُ بِنْتُ عِمْرَانَ وَآسِيَةُ بِنْتُ مُزَاحِمٍ امْرَأَةُ فِرْعَوْنَ))
((Wanawake bora wa Jannah ni Khadiyjah bint Khuwaylid na Faatwimah bint Muhammad, na Maryam bint ‘Imraan, na Aasiyah bint Muzaahim)) [Musnad Ahmad, ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (1135)]