20-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - Ummu Haarithah (Radhwiya Allaahu 'Anhaa)

 

Swabrun Jamiyl (Subira Njema)

 

20- - Subira Za Swahaabiyaat - Ummu Haarithah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)

 

 

Naye ni Ar-Rabiy’ bint Nadhwr bin Dhwamdhwam bin Zayd, shangazi yake Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Mama mzee aliyevuta subira kwa ajili ya kutaka Jannah baada ya kuuliwa mwanawe mpenzi katika vita vya Badr. Waliporudi watu vitani aliangaza huku na kule akimtafuta mwanawe. Waume walirudi kwa wake zao, watoto walirudi kwa wazazi wao. Yeye akangojea na kungojea amuone kipenzi cha moyo wake, lakini Haarithah hakutokea. Akamwendea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akiwa machozi yamemlenga machoni. Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesimulia: “Ummu Haarithah alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  baada ya Haarithah kufa shahidi katika vita vya Badr kwa mshale aliodungwa moyoni na mtu asiyejulikana. Akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Unajua mahali pa Haarithah moyoni mwangu (jinsi alivyo kipenzi kwangu), kwa hiyo ikiwa yuko Jannah, sitomlilia, au sivyo unaona nifanye nini? Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika hizo ni Jannaat nyingi si Jannah [moja] na mwanao amefikia Jannah ya Al-Firdaws ya juu))”.

 

Mama mzee huyo aliposikia jibu hilo, machozi yake yakamkauka akarudi nyumbani kwake akiwa na matumaini ya kuondoka duniani ajumuike na mwanawe huko Peponi. Hakutaka ngawira wala mali, wala lolote bali aliridhika na Jannah. Madamu mwanawe yupo Jannah amestarehe kwa mema waliyobashiriwa mashahidi, basi kumkosa mwanawe duniani hakukuwa na umuhimu tena. Akaendelea kuvuta subira kupata mema yanayodumu milele.

 

 

Share