21-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - Nusaybah Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu 'Anhaa)
21 - Subira Za Swahaabiyaat - Nusaybah Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)
Nusaybah bint Ka’ab Al-Answaariyyah, alijukana pia kwa jina la Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Alisilimu aliposikia tu Uislaam. Na alijaaliwa kuwa katika fungamano la kumlinda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa hali na mali lilojuliakna kwa ‘Bay’atul-‘Aqabah’ (Fungamano la Al-‘Aqabah) la Pili’. Ujumbe upatao wanaume sabiini na wanawake wawili akiwemo yeye kutoka Madiynah walikwenda Makkah kwa siri kukutana na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufungamana na ahadi zake. Alishiriki katika vita vingi vikiwemo vita vya Uhud, Hudaybiyah, Khaybar, vita vya Al-Yamaamah na Hunayn. Alihudhuria pia siku ya ‘Bay’atur-Ridhwaan’ (Fungamano la Radhi] pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba wengineo chini ya mti, akaingia katika miongoni mwa wale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliowateremshia kauli Yake:
لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ فَعَلِمَ مَا فِي قُلُوبِهِمْ فَأَنزَلَ السَّكِينَةَ عَلَيْهِمْ وَأَثَابَهُمْ فَتْحًا قَرِيبًا﴿١٨﴾
Kwa yakini Allaah Amewawia radhi Waumini walipofungamana nawe ahadi ya utiifu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) chini ya mti, (Allaah) Alijua yale yaliyomo nyoyoni mwao; basi Akawateremshia utulivu, na Akawalipa ushindi wa karibu. [Al-Fat-h: 18]
Alibashiriwa Jannah pia pamoja na kuwa karibu na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Alikuwa na mapenzi makubwa mno ya Dini yake na akimpenda mno Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa mwanamke shujaa aliyependa jihaad katika njia ya Allaah na kusaidia waliokuwa wakijeruhiwa vitani. Aliposhiriki vita vya Uhud alionyesha ushujaa wake na mapenzi yake ya ajabu ya kumhami Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Alipatwa majeraha kumi na mbili. Kisa chake amekisimulia mwenyewe:
“Nilitoka wakati wa asubuhi siku hiyo nikiwa nimebeba birika la maji na kuelekea moja kwa moja penye uwanja wa vita nikajionee mwenyewe yanayotendeka huko. Nikamuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa kati ya Swahaba zake na wakati huo Waislamu walikuwa wakiwashambulia makafiri na kuwashinda. Ghafla mambo yakabadilika na Waislam wakaanza kushindwa, na kurudi nyuma. Nilipomuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezungukwa na maadui, nikautoa upanga wangu na kusimama mbele yake na kuanza kupigana huku na kule. Akatangulia kafiri mmoja anayeitwa Abuu Qamiy-ah huku akisema kwa sauti kubwa: “Nionesheni alipo Muhammad! hatosalimika leo ikiwa mimi nitakuwa salama”. Anasema Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) “Alipomfikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakati huo alikuwa keshaanguka chini akiwa amejeruhiwa, mimi nikamkabili kafiri huyo akiwa na upanga mkononi nami nikiwa nimesimama baina yake na baina ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) huku akinichoma kwa upanga wake mara nyingi. Nami nikampiga kwa upanga wangu mara nyingi pia, lakini adui wa Allaah yule alikuwa amevaa nguo mbili za chuma.” Mwanawe Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye ni ‘Abdullaah bin Zayd (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema: “Baada ya vita vya Uhud kumalizika niliona majeraha mengi juu ya mwili wa mama yangu Nusaybah, na majeraha mengine yalikuwa makubwa hata ilikuwa ukiweza kuiingiza kiganja cha mkono ndani yake kutazama.”
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipozungumza juu ya ushujaa wake siku ya Uhud alisema: ((Daraja ya Nusaybah binti Ka’ab leo ni kubwa kuliko fulani na fulani)) Na alikuwa akisema kumwambia Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): ((Nani atakayeweza kustahamili ulivyostahamilia wewe ee Ummu ‘Ammaarah?)) Na Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akawa anamjibu: “Mimi niko tayari kustahamili chochote ee Rasuli wa Allaah, isipokuwa nataka tu uniombee niwe pamoja nawe siku ya Qiyaamah.” Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: ((Bali utakuwa pamoja nami, tena si peke yako, wewe na wanao na familia yako yote. Ee Rabb wangu! mjaalie yeye na familia yake yote wawe pamoja nami Peponi)). Pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ((Nilikuwa ninapogeuka kushoto au kulia namuona yeye akipigana kwa ajili yangu)).
Nusaybah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alidhihirisha subira yake mara nyingine katika vita vya Al-Yamaamah alipokatwa mkono wake. Vilikuwa ni vita baina ya majeshi ya Kiislamu na majeshi ya Musaylimah Al-Kadh-dhaab wakati wa ukhalifa wa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu). Ummu ‘Ammaarah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipomtaka Khalifa wa Waislam ruhusa ili ashiriki vita hivyo, Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimwambia: “Tunaulewa vizuri ushujaa wako na usatahamilivu wako ee Ummu ‘Aamaarah, ingia vitani ukitaka kwa baraka za Allaah” Ummu Sa’ad bin Ar-Rabiy’ amesema: “Nilimuona Nusaybah bint Ka’ab mkono wake ukiwa umekatika, nikamuuliza: “Lini umekatika mkono wako?” Akanambia: “Siku ya (vita vya) Al-Yamaamah nilikuwa pamoja na watu wa Madiynah, tulipofika katika bustani ya Musaylimah, vita vikali vikapiganwa kwa muda hivi kwa ajili ya kupateka mahali hapo, na Abuu Dujaanah aliuliwa mahali hapo. Kisha nikaingia mimi ndani ya qasri nikimtafuta adui wa Allaah, Musaylimah al-Kadh-dhaab, akanitokea mmoja katika watu wake. Nikapambana naye, akanipiga na kunikata mkono wangu. Basi wa-Allaahi sijauendea kuuokota, nilisonga mbele kumtafuta mpaka nikamuona khabithi yule (Musaylimah) akiwa amekufa, na mwanangu (‘Abdullaah bin Zayd) akiwa karibu yake huku akiufuta upanga wake juu ya mwili wa Musaylimah, Nikamuuliza: “Wewe ndiye uliyemuua?” Akanijibu: “Ndiyo ee mama yangu.” Nikasujudu kumshukuru Allaah.”
Riwaayah nyingine imesemekana kwamba aliyemuua Musaylimah ni Wahsh bin Harb Al-Habashiyyi na kwa hiyo imesemekana kwamba wote wawli walihusika kumuua adui huyo wa Allaah.