Kumlipia Mama Aliyefariki Deni La Swawm Ya Ramadhaan
SWALI:
Asalam alaykum naomba kuuliza suala ambalo linanitatiza katika akili yangu mimi ni msichana ambae mama yangu amefariki kabla ya kifo chake alikuwa akidaiwa mwezi mzima wa ramadhani ambayo ilipitiwa na miaka kumi na tatu bila ya kuilipa suala langu ni tumlipie vipi naomba mnifahamishe na ikiwa ni kuwalisha masikini naomba mniambie ni kiasi gani au tunaweza kumlipa mtu amfungie au sisi watoto wake tunaweza kumfungia inshala M/mugu awape nguvu na awaongezee elimu ili muzidi kutusaidia ammin.
JIBU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani kwa swali lako
Suala hili wamekhitilafiana Wanachuoni, kuna waliosema deni la Swawm ya nadhiri tu ndio inayopaswa kulipwa. Na wengine wameonelea kuwa Swawm hata za Ramadhaan zinafaa kulipwa. Waliosema zinazolipwa ni Swawm za nadhiri wanatoa dalili hii:
Kulikuwa na mwanamke mmoja wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa safarini, na humo akaweka nadhiri kuwa lau Allaah Atamuokoa basi yeye atafunga miezi miwili. Lakini mwanamke huyo hakuwahi kufunga mpaka akaaga dunia. Jamaa yake wa karibu alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza kuhusu ile nadhiri ya funga ya huyo jamaa yake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Je, unaonaje, angekuwa anadaiwa na mtu si ungelimlipia deni lake?” Akajibu: “Ndio”. Kisha Mtume akamwambia, “Basi mlipie funga yake” (al-Bukhaariy na Muslim).
Na wanaonelea kuwa Swawm hata za Ramadhaan mtu anaweza kulipiwa deni lake, wanatoa dalili ifuatayo:
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema tena: “Atakayekufa ilhali kaacha deni la funga basi na alipiwe na walii wake” (al-Bukhaariy na Muslim).
Na Allaah Anajua zaidi