Mwanamke Mja Mzito Afunge Ramadhwaan?

SWALI:

Assalamu alaykum warahmatullahi wabakatuh

Je mwanamke mja mzito anaweza kufunga wakati wa ramadhani? Kwasababu kuna ubishani baina yangu na mume wangu. Inshaallah mwenyezi mungu atawazidishia ‘ilm.

Wassalamu alaykum

 


 

JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Mwanamke mja mzito ana khiari katika kufunga Swawm ya Ramadhaan. Ikiwa ataweza kufunga bila ya kuathirika siha yake na ya mtoto anaweza kufunga. Lakini ikiwa anahisi hawezi kufunga kwa sababu hawezi kukaa na njaa  na khofu kuwa mtoto tumboni ataathirika basi ameruhusiwa kutokufunga, kwani atakuwa ameingia katika hukmu ya mgonjwa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

((أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ)) 

 

((Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyingine)) [Al-Baqarah: 184]

Kisha anatakiwa alipe deni lake baada ya Ramadhaan. Na kwa kauli ya Wanachuoni wengine ni kuwa anatakiwa alipe kafara ikiwa aliacha kufunga kwa kuhofia nafsi yake au nafsi ya mtoto aliye tumboni.

Tafadhali ingia katika viungo vifuatavyo vyenye mas-ala kama hayo upate maelezo zaidi:

 

Mke Mje Mzito Hawezi Kulipa Siku Zilizobakia Za Ramadhaan

 

Nini Hukmu Ya Swawm na Mwenye Kunyonyesha?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share