Zingatio: Mwenye Kujiua Si Miongoni Mwetu
Zingatio: Mwenye Kujiua Si Miongoni Mwetu
Naaswir Haamid
Hayajawa haya maisha ya duniani isipokuwa ni mtihani tu, na matokeo ya mtihani huu iwapo umepasi au umefeli yatajulikana baada ya kukata roho na kuthibitishwa baada ya kupokea Kitabu siku ya Qiyaamah.
Hivyo, kila mwanadamu na zaidi kwa Muislamu anawajibika kujipinda kuufanya vyema mtihani huu. Na ni hasara ya nani iwapo mtahiniwa ataanza kudai kwamba mtihani ni mgumu na kuwa ndio chanzo cha yeye kujitoa roho? Bila ya shaka yoyote itakuwa ni hasara kwa nafsi yake.
Ndio mtihani huu ambao tunapambana nao hapa duniani; na kwa bahati mbaya, ndugu zetu wengine wa Kiislamu wamekuwa na papara hadi kufikia kujitoa roho zao kwa makusudi, lengo kuu likiwa ni kukimbia matatizo au kashfa walizokumbana nazo.
Hapa tunaona mlolongo mkubwa wa wanaozidhulumu nafsi zao, wapo wanaojitundika vitanzi, wanaomeza sumu, wanaojitupa kwenye majumba marefu na kadhalika.
Na ni kwasababu gani hadi kufikia kuzitoa roho hizi? Si nyengine zaidi ya mitihani ya maisha, maradhi, familia, ndoa, watoto, fitina, kukosa kazi na kadhalika. Lakini kuna wengine mitihani hii wameitengeneza kwa mikono yao wenyewe kama vile kufumaniwa katika uzinifu, kubeba mimba nje ya ndoa, madeni yasiyokuwa na ulazima na kadhalika.
Kutokana na ukosefu wa elimu ya Tawhiyd juu ya namna ya kujikwamua na mitihani hii, kundi hilo hapo juu huamua kuwa njia ya kujikwamua na mitihani ni moja tu; nayo ni kujidhulumu nafsi zao kwa kujiua kwa makusudi.
Basi ee mwenye kufikiria kujidhulumu nafsi yako kwa kujitoa roho kutokana na mashaakil ya dunia haya, hujayapitia yale maneno ya Rabb Mtukufu Aliyoyanadi kwako?
قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾
Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu. [Az-Zumar: 53]
Na kutokana na Hadiyth aliyoisumulia Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Yeyote atakayejitupa kutoka mlimani na kujiua ataingia motoni akiuangukia ambako ataishi humo milele. Na yeyote atakayekunywa sumu na kujiua nafsi yake, atabeba sumu yake mkononi mwake huku anainywa motoni ambako ataishi milele. Na yeyote atakayejiua kwa silaha ya chuma, atabeba silaha yake mkononi mwake na huku anajichinja tumbo lake motoni ambako ataishi milele. [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Hivyo tunawanasihi wale ambao wamegubikwa na mitihani hii ya dunia wenye kufikiria kujidhulumu nafsi zao, waachane na mawazo hayo potofu, kwani hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuikutia mitihani ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Naye katu hakuwa miongoni mwa wenye kujidhulumu nafsi yake. Na iwapo unaona mitihani yako ni mikubwa zaidi, basi yupo aliyekuzidi maradufu.
Tunamuomba Rabb Mtukufu Atujaalie haki tuweze kuiona tukaifuata, na baatwil kuitambua tuweze kuikimbia. Twakuomba Manani utujaalie khatima njema na utujaalie kuwa miongoni mwa waja wako wema watakaoruzukiwa bustani zako za Jannatul-Firdaws; Aamiyn.