Wanaopinga (Ahlul-Bid'ah) Kuwa Allaah Yuko Juu Hawana Dalili Za Msingi
Wanaopinga (Ahlul-Bid'ah) Kuwa Allaah Yuko Juu Hawana Dalili Za Msingi
Shaykh-ul-Islam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah)
[Al-Fataawaa al-Hamaawiyyah, ukurasa 19]
Kuna kauli tele kutoka kwa Salaf kuhusiana na suala hili*
Kwa upande mwingine, hakuna herufi hata moja kwenye Kitabu cha Allaah (’Azza wa Jalla), wala Sunnah ya Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au Maswahaba wake, au waliokuja baada yao na Maimaam wa Ummah; kauli zao hazikwenda kinyume. Hakuna maandishi kutoka kwao, au hata mfano wa kitu kinachoashiria hilo.
- Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah Hayupo juu mbinguni.
- Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah Hayupo juu ya kiti Chake cha enzi.
- Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah Yupo kila mahali.
- Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kuwa kila mahali [popote] ni sawa na Allaah.
- Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba Allaah Hayupo ndani ya uumbaji, nje ya uumbaji.
- Kamwe hata mmoja hakuwahi kusema kwamba ni makosa kuashiria kwa kidole juu kwa Allaah, na kadhalika.
Ukweli ni kuwa imepokelewa Hadiyth kutoka kwa Jaabiyr bin 'Abdillaah (Radhwiya Allaahu ’anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kasema wakati wa khutbah yake ya mwisho:
"Je, nimefikisha?” Wakasema: "Ndiyo." Kisha [baada ya hapo] akapandisha kidole chake akikielekeza mbinguni kisha akakiteremsha na kusema: ”Allaahumm Shuhudia.” [Muslim 1218]
*Yaani ni kauli ambayo inathibitisha Majina na Sifa za Allaah. Hapa chini kunafuatia baadhi ya kauli za Salaf ambazo zinaonesha wazi kabisa na dhahiri kuwa Muumbaji wa viumbe yupo juu mbinguni:
1 - Imaam Muhammad bin Is-haaq (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Juu ya kiti cha enzi yupo Yule ambaye ana Ukuu na Utukufu.” [Al-'Uluww, Uk. 150., kutoka kwa Imaam Adh-Dhahabiy]
2 - Imaam 'Abdur-Rahmaan al-Awzaa'iy (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Yupo juu ya kiti Chake cha enzi kwa namna ileile ambayo Yeye Mwenyewe kaieleza.” [Uk. 138)]
3 - Imaam Hammaad bin Zayd (Rahimahu-Allaah) kasema kuhusu Jahmiyyah:
“Hoja yao ni kwamba hakuna ilaah yeyote juu ya mbingu.” [Uk. 146]
4 - Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Allaah Yuko juu ya mbingu. Elimu (maarifa) Yake yapo kila mahali na hakuna kitu kinachoepuka (pinga) hilo.” [Uk. 140]
5 - Kulisemwa kwa Imaam ’Abdullaah bin al-Mubaarak (Rahimahu-Allaah):
“ Vipi tutajifunza kumjua Rabb wetu?” Akasema:
“Kwa kujua kwamba yupo juu ya mbingu saba na juu ya kiti Chake cha enzi. Hatusemi kama jinsi Jahmiyyah wanavyosema kuwa Yupo hapa duniani.”
6 - Imaam Jariyr adh-Dhabbiy (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Kauli ya Jahmiyyah inaanza kwa asali na inakwisha kwa sumu. Wanajaribu kusema kwamba hakuna ilaah yeyote juu ya mbingu.” [Uk. 151]
7 - Imaam 'Aliy al-Madiyniy (Rahimahu-Allaah ) kasema:
“Jahmiyyah wanataka kukataa kwamba Allaah Aliongea na Muwsaa, na kwamba Yupo juu ya kiti Chake cha enzi. Naonelea kuwa wanatakiwa kufanya tawbah. Ima watubie au wanyongwe.“ [Uk 169]
8 - Imaam Wahb bin Jariyr (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Jitengeni mbali na fikra za Jahmiyyah. Wanataka kusema kwamba hakuna ilaah yeyote juu ya mbingu. Hakuna la zaidi isipokuwa Ibliys ndio kawateremshia wahyi (kuhusu hili). Si kitu kingine bali ni Ukafiri” (Uk. 170]
9 - Imaam Abuu Zur'ah ar-Raaziy (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Yupo juu ya kiti Chake cha enzi na elimu Yake ipo mahali pote. Laana ya Allaah imshukiye yule atakayesema kitu kingine chochote kinyume na hili.” [Uk. 203]
10 - Imaam 'Uthmaan bin Sa’iyd ad-Daarimiy (Rahimahu-Allaah) kasema:
“Waislamu wamekubaliana kwamba Allaah Yupo juu ya kiti Chake cha enzi na juu ya mbingu Zake.” [Uk. 213]
Faida: Baadhi ya Dalili katika Qur-aan Na Sunnah:
الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾
Ar-Rahmaan; Yuko juu (Istawaa) ya ‘Arsh. [Twaahaa: 5]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ﴿٤﴾
Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa) ya ‘Arsh. [As-Sajdah: 4]
Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ رَبَّكُمُ اللَّـهُ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ﴿٥٤﴾
{Hakika Rabb wenu ni Allaah Ambaye Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa) ya ‘Arsh }. [Al-A’raaf: 54]
Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
تَعْرُجُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ إِلَيْهِ فِي يَوْمٍ كَانَ مِقْدَارُهُ خَمْسِينَ أَلْفَ سَنَةٍ ﴿٤﴾
{Malaika na Ar-Ruwh (roho za viumbe au Jibriyl) wanapanda Kwake katika siku kadiri yake ni miaka khamsini elfu}. [Al-Ma’aarij: 4].
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾
Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?
أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ﴿١٧﴾
Au mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokutumieni tufani ya mawe basi mtajua vipi maonyo Yangu. [Al-Mulk: 16-17]
Hata Fir-‘awn alikiri kuwa Allaah Yuko juu:
وَقَالَ فِرْعَوْنُ يَا هَامَانُ ابْنِ لِي صَرْحًا لَّعَلِّي أَبْلُغُ الْأَسْبَابَ ﴿٣٦﴾ أَسْبَابَ السَّمَاوَاتِ فَأَطَّلِعَ إِلَىٰ إِلَـٰهِ مُوسَىٰ وَإِنِّي لَأَظُنُّهُ كَاذِبًا ﴿٣٧﴾
{Na Fir’awn akasema: “Ee Haamaan nijengee mnara ili nifikie njia. “Njia za mbinguni ili nimchungulie Ilaah wa Muwsaa, kwani hakika mimi namdhania ni muongo}. [Ghaafir: 36-37]
Katika Sunnah:
عن أبي هريرة رضي الله عنه: تُعرَضُ الأعمالُ يومَ الاثنينِ والخميسِ فأحبُّ أن يُعرَضَ عملي وأنا صائمٌ
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Amali zinapandishwa siku ya Jumatatu na Alkhamiys, basi napenda kwamba zipandishwe 'amali zangu nikiwa mimi nina Swawm.” [Swahiyh At-Tirmidhiy 747, Swahiyh At-Targhiyb 1041]
Na pia,
Kufaridhishwa Swalaah tano mbingu ya saba [Al-Bukhaariy na wengineo]
Na pia,
Abdullaah bin ‘Amr amesimulia kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Kuwa na huruma kwa waliopo ardhini, ili Yule aliyepo juu ya mbingu apate kuwa na Rahmah kwako”. [Imaam Al-Bukhaariy, Imaam Muslim na wengineo]
Na pia,
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na pia,
Abu Bakr Asw-Swiddiyq amesema: “Yule aliyekuwa akimuabudu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), (na atambue kwamba) Muhammad amekufa, na yule anayemuabudu Allaah, (na atambue kwamba) Allaah Yuko juu ya mbingu Milele Anaishi, wala hafi.” [Imaam Al-Bukhaariy na wengineo]