Kupanga Uzazi Na Si Kuzuia Uzazi

SWALI:

 

Assalam Allaykum Warhamatullah wabarakatuH ,

swali langu ni hivi je mwanamke wa kiisalm anaruhusiwa kutumia njia za uzazi wa mpango za kisasa yaani kama contraceptives pills, loop, sindano n.k na hasa pale ambapo njia ya kalenda inashindikana kwa mwanamke huyo kutokuwa na mzunguko uliokuwa stable. Ninasubiri majibu - wenu katika imanii

 

 


 

JIBU: 

 

AlhamduliLLaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Asli ni kuwa Muislamu lazima aitakidi kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  ndiye Mwenye kuruzuku, kumruzuku yeye na walio katika dhimma yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Aayah zifuatazo:

 

 وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ إِلاَّ عَلَى اللّهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِين

 

Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Allaah. Naye Anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha. [Huwd 11: 6]

 

وَلاَ تَقْتُلُواْ أَوْلادَكُمْ خَشْيَةَ إِمْلاقٍ نَّحْنُ نَرْزُقُهُمْ وَإِيَّاكُم إنَّ قَتْلَهُمْ كَانَ خِطْءًا كَبِيرًا

 

Wala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi Tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa. [Al-Israa 17: 31]

 

 وَلاَ تَقْتُلُواْ أَوْلاَدَكُم مِّنْ إمْلاَقٍ نَّحْنُ نَرْزُقُكُمْ وَإِيَّاهُمْ  

 

Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao.  [Al-An’aam 6: 151]    

 

Inaruhusiswa kuzuia pindi kutakuweko sababu zinazokubalika katika shari’ah mfano:

 

  1. Afya ya mama:  kuwa mama haruhusiwi kitabibu kushika mimba kwa  sababu ana ugonjwa kwa mfano wa moyo, hawezi kuzaa ila kwa njia ya kutolewa mtoto kwa juu (caesarian) n.k.
  2. Afya ya mtoto: kukosa kunyonyeshwa kwa mtoto kwa sababu ya kuzaa watoto bila ya kuwa na nafasi ya kutosha baina ya mimba mbili, yaani  kabla ya mtoto wa kwanza kunyonya kwa muda wa miaka miwili, mama akapata mimba nyengine.  

 

Njia za kupanga Kizazi

 

Kuna njia mbili za kupanga kizazi:

 

1-    Kukata uzazi kabisa (Permanently) –

a)    Kwa mwanamume: Vasectomy

b)    Kwa mwanamke: Tubal ligation

 

Nji hizi haziruhusiwi  kabisa ila ikiwa hakuna njia nyengine ila hiyo.

 

2-    Kupanga kwa kutumia mbinu tofauti

 

a)    Kutumia madawa (Chemical): kwa mfano madawa ya kupanga uzazi; kama tembe (pills), shindano (injections).

b)    Kutumia vifaa (Mechanical): Kwa mfano mipira (condoms), koili (coil)

c)    Kutumia mbinu za kimwili (Physical): Kumwaga manii nje “Azl”, mpangilio wa tarkimu ya kalenda (Standard Days Method)

 

Hizi zinaruhusiwa ikiwa kuna sababu za kishari’ah tulizozitaja hapo awali. Na mwenye kujua mbinu bora zaidi kwako ni wewe mwenyewe kwa ushauri wa daktari mutakhasis (aliyebobea na stadi) muaminifu.

 

Tanbihi: Tusichukuwe uamuzi mikononi mwetu kwa kutumia njia ambazo zipo juu bila ya ushauri wa daktari kwani njia ya madawa ina madhara makubwa mwilini. Daktari ndio anaweza kuukuambia madawa ambayo yatakuwa na madhara madogo zaidi kwako na kila ukijiepusha ila kwa dharura ni bora zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share