Kufuata Swalah Ya Jamaa Bila Ya Kumuona Imaam

 

SWALI:

Inafaa kufuata jamaa nikiwa peke angu chumbani wakati ukumbini wanaume wanasali jamaa nami nasikia takbir zote?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Inajuzu kwa maamuma kumfuata Imaam na kati yao kuna kizuizi (mfano ukuta) ikiwa maamuma hao wanafahamu anayotenda Imaam katika Swalah kwa ima kumuona au kusikia. Lakini haifai mtu kuswali kwa kufuata Swalah ya radio au televisheni.

Amesema Al-Bukhariy, kuwa al-Hasan amesema: “Hakuna tatizo kwa mtu kuswali na baina yake yeye na Imam kuna mto”. Na amesema Abu Mjliz: “Unaweza kumfuata Imam hata ikiwa baina yenu kuna njia au ukuta ikiwa atasikia takbiratul Ihram”.

Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   aliswali katika chumba chake na Maswahaba رضي الله عنهم  wakawa wanamfuata nyuma yake. kwa hivyo Swalah ambayo mtu ataswali katika chumba chake na akawa anawaona walio ukumbini au kuisikia sauti ya Imaam hivyo kuwezesha yeye kumfuata bila ya matatizo itakuwa sawa. Lakini ni lazima ifahamike kuwa chumba hicho ni lazima kiwe nyuma ya maamuma wengine wanaoswali au ubavuni mwa ukumbi huo.

 Wa Allaahu A'alam

 

Share