Kuswali Nyuma Ya Imaam Anayevuta Sigara Inajuzu?
SWALI:
Assalaam Allaykum
Nashukuru kwa kunielewesha namna ya kuuliza swali namuomba M/Mungu awabariki kwa kazi mnayofanya
Swali:-
Je katika swala inaswihi kumfuta imaam anayevuta sigara?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kuvuta sigara ni kitendo kiovu na ni haraam kutokana na Shari'ah kwani kinakwenda kinyume na fitrah (maumbile ya asili) na pia kinaleta madhara kwa siha ya mtu anayevuta na vile vile siha ya wanaokuwa karibu naye.
Ikiwa katika mji yuko Imaam mwingine ambaye hana vitendo vibaya kama hicho cha kuvuta sigara, basi ni bora aswalishe yeye. Na kama hakuna mwingine isipokuwa yeye, basi Waislamu wanatakiwa waswali nyuma yake, kwa sababu kuswali Jamaa ni wajib na fadhila zake ni kubwa kuliko kuswali pekee japokuwa Imaam ni mtu muovu. Hii ni rai ya maulamaa wengi wao; wakiwa Ahmad bin Hanbal, Ash-Shaafi'iy. Imaam Ahmad pamoja na ma-Imaam wengine wa Sunnah wameona kwamba asiyeswali Swalah ya Ijumaa nyuma ya Imaam muovu ni mzushi.
Na rai sahihi ni kuwa aswali na Imaam muovu na hana haja kukidhi Swalah hizo.
Vile vile Imaam Al-Bukhaariy amesimulia
وترجم الإمام البخاري في صحيحه : باب إمامة المفتون والمبتدع ، ثم روى فيه ( 695 ) عَنْ عُبَيْدِ اللَّهِ بْنِ عَدِيِّ بْنِ خِيَارٍ أَنَّهُ دَخَلَ عَلَى عُثْمَانَ بْنِ عَفَّانَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ وَهُوَ مَحْصُورٌ فَقَالَ : إِنَّكَ إِمَامُ عَامَّةٍ [ أي : أنت إمام الناس ] ، وَنَزَلَ بِكَ مَا نَرَى ، وَيُصَلِّي لَنَا إِمَامُ فِتْنَةٍ وَنَتَحَرَّجُ ؟! يعني: نخشى من الحرج ، وهو الإثم ، في الصلاة معه فَقَالَ : الصَّلاةُ أَحْسَنُ مَا يَعْمَلُ النَّاسُ ، فَإِذَا أَحْسَنَ النَّاسُ فَأَحْسِنْ مَعَهُمْ ، وَإِذَا أَسَاءُوا فَاجْتَنِبْ إِسَاءَتَهُمْ
Katika mlango wa 'Baab Imaamat Al-Maftuun wa-Al-Mubtadi' (Mlango wa watu waovu na wazushi kuimamisha Swalah) kwenye Swahiyh ya Al-Bukhaariy, anasimulia kutoka 'UbayduLlah bin 'Adiyy ibn Khiyaar kwamba alikwenda kwa 'Uthmaan bin 'Affaan رضي الله عنه na kumwambia: "Wewe ni Imaam mkuu wa watu na umeona yanayotusibu, na sasa Imaam mwenye fitan anatuswalisha na sisi tunakhofu kufanya dhambi". Akasema "Swalah ni kitendo bora kabisa watu wakitimize. Watu wakifanya mema nanyi fanyeni mema nao, lakini wakifanya maovu basi jiepusheni na maovu
Kwa hiyo haikupasi kuacha kuswali Jama'ah japokuwa Imaam ni muovu. Lakini ukipata Imaam aliye bora kuliko yeye basi ni bora uswali naye.
Vile vile ujaribu kutafuta watu wampe nasiha huyo Imaam mwenye kuvuta sigara na kumfahamisha hukumu yake katika Shari'ah na vile vile akumbushwe madhara yake na umuhimu wa yeye kuacha sigara kutokana na cheo chake alichojaaliwa kuwa awe ni mfano bora kwa Waislamu wengine.
Na Allaah Anajua zaidi