Zingatio: Usimuombe Muhammad, Bali Muombe Allaah
Zingatio: Usimuombe Muhammad, Bali Muombe Allaah
Naaswir Haamid
Waislamu sote tunakiri na kutamka kwa ndimi zetu kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Nabiy wa mwisho, naye ni mbora wa viumbe, mwenye tabia bora za kupigiwa mfano na sisi tunawajibika kuzifanyia kazi.
Hata hivyo, juu ya hikmah zake, cheo na daraja alichonacho, hatustahiki hata kidogo kumuomba Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika lolote tunalohitajia kuliomba. Wala hatuwajibiki kuamini kwamba du’aa isiyopita transit kwake, haikubaliwi. Hilo sio sahihi katu, kwani Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa malaaikah wala jamii isiyokuwa yetu sisi. Ni mwenzetu, mwenye maumbile sawa na sisi, kilichobadilika kutoka kwake ni kupokea wahyi tu.
Rabb wetu, Anasema kwamba tumuombe Yeye, kwani Ndiye Anayezisikia du’aa zetu na malalamiko yetu:
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾
Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]
Pia Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ
Na Rabb wenu Amesema: Niombeni, Nitakuitikieni. [Ghaafir: 60]
Kwa upande wake, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba tusimtukuze kama walivyomtukuza Manaswara kwa Nabiy ‘Iysaa hadi kumpa daraja na cheo sawa cha Rabb:
"Msinitukuze (kwa kunipandisha cheo kama cha Allaah) kama walivyomtukuza Manaswara ‘Iysaa mwana wa Maryam, hakika mimi ni mja, kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake." [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Wala hawa Manasara hawakuishia hapo, nao pia wakajitukuza na kujipachika vyeo vya Unabii na Utume, na kujidai kuweza kuombwa na wanaadamu wenzao pamoja na kusamehe madhambi. Hayo kwetu yatabakia ni uzushi mkubwa na ni shirki iliyo wazi.
Kwa hapa, tunaomba tuzingatie kwamba du’aa yoyote inatakiwa kuelekezwa moja kwa moja, kiroho na kimatamshi kwake Muumba wala sio kwa Nabiy. Tunaona ndani ya jamii zetu za Kiswahili, mtu anapojitoka, anapotokewa na tatizo la ghafla au mfano wa hayo; basi kauli ya mwanzo linalomjia mdomoni ni la kishirikina: Nabiy! na mfano wa hayo.
Ee ndugu yangu Muislamu, umesahau ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti. Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivi sasa ni maiti, asiyeweza hata kusikia maombi yetu, seuze kuweza kutuombea kwa Rabb. Sasa iweje leo neno lako la mwanzo unapotokezewa na shida liwe Nabiy!?
Na wengine wapo waliochupa mipaka, wakawapatia vyeo wanaowaita masharifu, mashekhe, mamufti, maqadhi, mawalii na kadhalika, wakawatumia kuzipitisha du’aa zao kwao. Ni ushirikina na uzushi ulioje. Utakuta kwenye du’aa zao wakisema: Kwa kuhudhuria Muhammad, mawlaana, sharaful-anbiyaa, wa shuyukhina, al-faatihah! Ujahili ulioje huu, Rabb wetu yupo karibu kuliko mapigo ya mioyo yetu, ya nini kupata taabu kuzipitisha du’aa kupitia kwa viumbe vinavyotegemea rahmah zake?
Tunamalizia kwa kuzinasihi nyoyo zetu na za Waislamu wote, kuachana na aina hii ya shirki, kwani tutakuwa tunamuomba kiumbe badala ya kumuomba Muumba.