Zingatio: Pepo Si Ya Mweupe Wala Mweusi

 

Zingatio: Jannah Si Ya Mweupe Wala Mweusi

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Kwa hakika hakuna linalotuweka duniani isipokuwa ni kumuabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa mintarafu ya kuzipata rehma zake Muumba, miongoni mwa hizo rehma ni kuingizwa Jannah. Na waliotangulia wamenena: ‘Kila mlango una ufunguo wake’, na ufunguo wa Jannah ni uchaji Allaah.

 

Hapana shaka yoyote jamii zilizo nyingi zimepitia katika zama za ukabila na ubaguzi wa rangi. Wapo hapo enzi za Kijahilia wakiongozwa na Abu Jahal waliokuwa wakiwabagua sana watu mfano wa kina Bilaal (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Kosa ambalo kwa Muumba si kosa, lilikuwa ni kwao kina Bilaal kuwa na ngozi nyeusi.

 

Na kwa hakika hata Mayahudi wanaijua vyema dhambi ya ubaguzi, walitendewa makubwa na Hitler mwanzoni mwa karne ya 20. Waliuliwa, walinyanyaswa na walinyimwa haki nyingi; sababu kuu ni wao kuwa ni Mayahudi. Hata hivyo, Mayahudi nao wameshavuka mipaka ya Hitler, na wanawaua ndugu zetu Palestina bila ya sababu wala ustaarabu.

 

Tunapoikanyaga ardhi ya Marekani, basi nayo imejaa damu za ubaguzi na mvundo wa harufu ya unyanyasaji dhidi ya watu weusi, uliofanyika dhahir shahiri zaidi mnamo karne ya 19 na 20.

 

Mifano ni mingi mno, lakini yatosha kwa hapa kupiga mbizi katika ubaguzi huo juu. Sasa tukija lengo ya mifano hii, ni kuonesha dhahir namna mwanaadamu alivyokuwa mchoyo, mwenye husda katika rizki alizojaaliwa kuzipata. Akitaraji kuwa ni zake na kufaidika nazo peke yake, hutoa kila sababu ya kumdidimiza asiye kuwa na asili yake, kwa lengo tu la yeye kupata kikubwa. Kwake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) halipo hivyo, wala haitatokea kwa Rabb Aliye Muadilifu kuliko wote, kuwa ni mwenye kumnyima mweusi kuingia Jannah kutokana na rangi yake.

 

Kutokana na Sunnah, hususan ndani ya khutba ya kuaga ya Rasuli wa Allaah, tunaona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

“Watu wote wanatokana na Aadam na Hawaa, Mwarabu hana ubora juu ya asiye kuwa Mwarabu wala asiye kuwa Mwarabu hana ubora juu ya Mwarabu, pia mweupe hana ubora juu ya mweusi wala mweusi hana ubora juu ya mweupe – isipokuwa kwa Mchaji Allaah na mwenye matendo mazuri.”

 

Halikadhalika, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amekwishatueleza katika Hadiythul-Qudsiy kwamba, Jannah ni kwa wachaji Allaah, wenye kusubiri, wanaume kwa wanawake:

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) ambaye amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amesema: ((Nimewatayarishia waja Wangu wema kile ambacho jicho lolote halijapata kuona na sikio lolote halijapata kusikia na wala haijapata kupita katika moyo wa binaadamu)) Akasema Abu Hurayrah: Kwa hivyo, soma ukitaka:

 

فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ ﴿١٧﴾

Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. [As-Sajdah:17]. [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]

 

Hivyo, waache waseme na kubaguana hata katika vitabu vyao vya sheria na vyenginevyo, lakini Jannah itabakia kuwa ni ya Waislamu walio wachaji Allaah wote, weupe kwa weusi, wanaume kwa wanawake. Basi ni wapi kwengine kupatikane uadilifu kama si mbele ya Muumba wa Mbingu na Ardhi?

Share