24-Swabrun Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat -Tamaadhwur Bint As-Sulaymiyyah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)
24 - Subira Za Swahaabiyaat -
Tamaadhwur Bint As-Sulaymiyyah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)
Jina lake hasa ni Tamaadhwur bint 'Amr bin Ash-Shariyd bin Rabaah As-Sulaymiyyah. Alijulikana kwa jina la Al-Khansaa na vile vile Umm Ash-Shuhadaa (mama wa mashahidi) kutokana na watoto wake waliofariki katika jihaad ya kupigana vita. Pia alijulikana kuwa ni mwanamke mwenye haiba nzuri iliyojaa fadhila, tabia njema, ushujaa na subira kubwa.
Kabla ya kuingia katika Uislam, alikuwa akitunga mashairi ya beti mbili tatu hadi walipofariki kaka zake Mu'aawiyah na Swakhar bin 'Amr, alifikwa na huzuni kubwa sana hata akawatungia mashairi. Yakawa mashuhuri mno, hata yakazidi kumpatia umaarufu. Na imesemekana kwamba hakuweko mwanamke aliyekuwa hodari wa mashairi kama yeye.
Baada ya vifo vya kaka zake, alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na watu wake wa Banu Sulaym akasilimu. Ilipofika wakati wa vita vya Qaadisiyyah alidhihirisha subira yake kubwa alipokwenda vitani pamoja na watoto wake wanne wa kiume na akawausia kwa kuwaambia maneno haya mazito:
"Enyi watoto wangu, naapa kwa Yule Ambaye laa ilaaha illa Huwa (hakuna muabudiwa wa haki ila Yeye), nyinyi ni watoto wa baba mmoja, sikumkhini baba yenu, mmesilimu kwa kutii, mmehama kwa khiari yenu…" Akaendelea kuwanasihi hadi akasema "Mtakapoamka kesho In Shaa Allaah kwa salama, nendeni vitani kupigana na adui zenu, kwani mnajua Aliyowaandalia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ya thawabu nyingi kwa kupigana na makafiri. Tambueni kuwa nyumba ya milele (Jannah) ni bora kuliko nyumba ya kutoweka (Dunia), Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اصْبِرُوا وَصَابِرُوا وَرَابِطُوا وَاتَّقُوا اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٢٠٠﴾
Enyi walioamini! Subirini na zidini kuvuta subira na bakieni imara na mcheni Allaah ili mpate kufaulu. [Aal-‘Imraan: 200]
Wakaenda vitani na alipopata habari ya vifo vyao wote alisema: "AlhamduliLLaah kwa Yule Aliyenipa heshima ya kuuliwa kwao na namuomba Allaah kwa rahma Zake, Aniunganishe nao."
Al-Khansaa (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akaendelea kubakia katika subira na kuthibitisha iymaan yake hadi alipoaga dunia wakati wa ukhalifa wa 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu).
Al-Khansaa (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ametuonyesha mfano bora kabisa wa Swabrun Jamiyl kwa kuridhika na majaaliwa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na inapasa mzazi anayefiwa na mwanawe afuate nyayo zake.