23-Swabrun-Jamiyl: Subira Za Swahaabiyaat - Faatwimah Bint Muhammad (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)
23 - Subira Za Swahaabiyaat - Faatwimah Bint Muhammad (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa)
Alikuwa ni kipenzi mno wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hadi kwamba alipokuwa anataka kusafiri huhakikisha kwamba Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ni wa mwisho kumuaga. Na anaporudi kutoka safarini huenda kwanza Msikitini kuswali rakaa mbili kisha huelekea nyumbani kwa Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kisha ndio huenda kwa wake zake (Radhwiya Allaahu ‘anhunna) Hata aliwahi kusema: ((Faatwimah ni sehemu inayotokana na mimi, atayemghadhibisha amenighadhibisha)).
Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alivumilia mno mitihani kadhaa kama mateso ya baba yake mpenzi na vifo katika familia yake. Mtihani mmojawapo mkubwa aliovumilia ni siku ile ‘Uqbah bin Abi Mu’iytw alipotupa taka juu ya kichwa cha baba yake aliyekuwa amesujudu mbele ya Al-Ka’bah. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliendelea kusujudu na hakuinua kichwa chake mpaka alipokuja Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kuondoa taka zile.
Mtihani mwengine ulikuwa katika siku za mwanzo za kulingania watu katika Uislamu, wakati Waislamu walipogomewa na makafiri Quraysh wa Makkah na kuzungukwa wakiwa katika bonde la Baniy Haashim muda wa miaka mitatu bila kupelekewa chakula. Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa akiwaona Waislamu wakiwa katika shida na njaa hata ikawabidi kula majani na ngozi. Wakati mwengine kilikuwa kikiwafikia chakula kwa njia ya kufichwa tena kwa siri. Hali hiyo iliathiri sana siha yake kwani alikuwa na umbo dhaifu tokea utotoni mwake. Lakini pia ilimuongezea iymaan, ushujaa pamoja na ukuaji wa akili na fikra.
Alifikwa na misiba mingi ukianza na kifo cha mama yake Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Kifo chake kilitokea katika mwaka uliojulikana ni ‘Aam Al-Huzn (mwaka wa huzuni) kwa kifo hicho cha mama yake. Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliweza kuyastahamilia yote hayo, akasubiri na kusimama imara pamoja na baba yake huku akimshughulikia na kumsaidia katika kuliziba pengo la mama yake Khadiyjah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na kwa ajili hiyo alikuwa akijulikana kwa 'mama wa baba yake.'
Misiba mingineyo ni kifo cha dada yake Ruqayyah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Kisha katika mwaka wa nane Hijriyyah alifariki dada yake Zaynab (Radhwiya Allaahu ‘anhaa). Na mwaka wa tisa alifariki dada yake mwengine, Ummu Kulthuwm (Radhwiya Allaahu ‘anhaa).
Mwisho kabisa ni msiba mkubwa zaidi wa kifo cha baba yake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alifariki siku ya Jumatatu mwezi wa Rabiy’ul Awwal mwaka wa kumi na moja Hijriy. Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alikuwa akimuona baba yake akihangaika alipokuwa akivuta pumzi zake za mwisho, akawa anamwambia: "Masikini baba yangu unataabika." Na baba yake akawa anamwambia: ((Baba yako hatopata tabu tena baada ya leo ee Faatwimah)). Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akawa analia kila anapomuona baba yake akihangaika huku akivuta pumzi zake za mwisho, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa kila anapopata fahamu akimwambia: ((Usilie ee binti yangu, bali nitakapokufa useme: “Innaa liLLaahi wa innaa Ilayhi raaji’uwn)). Ilipotoka roho yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaaga dunia, Faatwimah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alisema: “Ee baba yangu! Umemuitikia Rabb wako, ee baba yangu! Jannah ya Firdaws makazi yako.”
Alivumilia pia kuishi maisha ya shida pamoja na mumewe ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye alikuwa anapomaliza shughuli zake nje, hurudi nyumbani kumsaidia mkewe kazi za nyumba. Amesema ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu): “Nilipomuoa Faatwimah hatukuwa tukimiliki zaidi ya ngozi ya kondoo tuliyokuwa tukiitandika wakati wa usiku na kulala juu yake, na wakati wa mchana tulikuwa tukiikalia, na hatukuwa na mfanya kazi wa kutusaidia shughuli za nyumba, na (Faatwimah) alipoletwa nyumbani, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa mtungi wa maji na gilasi mbili pamoja na kitambaa na mito miwili iliyojazwa ndani yake majani ya mtende." Aliwahi kutaka msaada kwa baba yake ampatie mtumishi kumsadia kazi za nyumba lakini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa lililo bora zaidi nalo ni kumfunza badala yake aina ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Alimfunza kwamba pale anapokuwa anataka kulala amsabbih Allaah (Subhaana Allaah) mara thelathini na tatu, amhimidi (AlhamduliLLaah) mara thelathini na tatu, na amtukuze (Allaahu Akbar) mara thelathini na nne. Faatwihmah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipokea nasaha hiyo akapata usahali katika kazi zake za nyumba pamoja na baraka nyinginezo katika maisha yao. Na hiyo ni fadhila kuu mojawapo kwake kwamba anachuma thawabu za Waumini wanaoitumia aina hiyo ya tasbiyh mpaka siku ya Qiyaamah.