26-Swabrun Jamiyl: Subira Za Taabi'iyn - Sa'iyd Bin Jubayr (Rahimahu Allaah)
25 - Subira Za Taabi'iyn - Sa'iyd Bin Jubayr (Rahimahu Allaah)
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alijitolea maisha yake kwa ajili ya Uislam, na hakumuogopa yeyote ila Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alizaliwa katika mji wa Kuwfaa. Watu wengi walifaidika na elimu yake iliyojaa faida. Alikuwa akiwafundisha watu kuhusiana na Dini na dunia yao.
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alikuwa ni Imaam mkubwa katika maimaam wa Fiqh katika zama za dola ya Umawiyyah kiasi cha kupata ushuhuda wa elimu aliyokuwa nayo kwa ‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwa uhodari wake wa Fiqh na elimu mbalimbali.
Ilikuwa kawaida ya watu wa Makkah wanaokwenda kutembelea wakiwaambia watu wa Kuwfaa: “Si mnae Ibn Ummi Ad-Dahmau.” [wakimkusudia Sa’iyd bin Jubayr.
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alikuwa ni mtu mwenye umbuji na fasaha, msema kweli, na moyo uliohifadhi, haogopi watawala dhalimu, hanyamazii haki, kwani mwenye kunyamazia haki ni shaytwaan kiziwi.
Hajjaaj bin Yuwsuf alimkamata baada ya kumtengenezea tuhuma ya uongo na aliazimia kummaliza. Hata hivyo Hajjaaj hakuweza kufunga mdomo wa Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) katika kuzungumza ukweli kwa kumtisha.
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alikuwa Muumin mwenye iymaan ya ukweli akifahamu kuwa mauti, uhai na riziki viko katika Mikono ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na hakuna mwengine mwenye uwezo wa hivyo.
Hajjaaj alibadilisha mbinu na akatumia njia ya kumweka mbali na haki Sa’iyd bin Jubayr kwa kumshawishi Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) kwa mali na maslahi ya kidunia kwa kumpa mali nyingi, hata hivyo Imaam huyu badala ya kuchukua mali ile alimpa Hajjaaj darsa ambalo hakuweza kulisahau.
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alimwambia Hajjaaj: “Ee Hajjaaj! Ikiwa umekusanya mali hii ili ikukinge na fazaa ya Siku ya Qiyaamah, basi ni vizuri, hata hivyo ukae ukifahamu kuwa fazaa moja ya Siku ya Qiyaamah humhizi kila mwenye kunyonyesha kwa kila anachonyonyesha!”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) alimfahamisha Hajjaaj kuwa mali ni katika njia kubwa ya kutengeneza amali za watu na mambo ya Aakhirah ya mtu, ikiwa mwenye mali hiyo amezikusanya kwa njia ya halali ili imwepushe na fazaa za Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾
“Siku hayatofaa mali wa watoto.
إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾
“Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa: 88-89]
Kwa mara nyingine jitihada za Hajjaaj kumshawishi Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) zilishindwa kwani hakuwa ni katika wenye kuabudu dunia na hakuwa katika wale wanaouza Dini yao kwa ajili ya dunia yao. Hajjaaj aliendelea kumtisha Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) kuwa atamkamata na kummaliza na mazungumzo yafuatayo yakawa baina yao:
Hajjaaj: “Ole wako ee Sa’iyd!”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah): “Ole ni kwa wale waliotoka Jannah na kuingizwa motoni.”
Hajjaaj: “Unapendelea nikuue namna gani?”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah): “Chagua mwenyewe ee Hajjaaj! Wa-Allaahi huwezi kuniua namna yeyote ile ila kifo kitakuangamiza katika Aakhirah!”
Hajjaaj: “Je, unapenda nikusamehe?”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah): “Ikiwa ni msamaha basi ni kutoka kwa Allaah, na wewe huna msamaha wala udhuru.”
Hajjaaj: “Nendeni mkamuue!”
Walipoondoka kwenda kumuua, mwanae Sa’iyd bin Jubayr alilia alipomuona katika hali hiyo, akamwangalia kisha akamwambia: “Nini kinachokuliza? Unalia nini wakati baba yako umri wake ni miaka hamsini na saba!” (kwa maneno hayo) rafiki yake nae akalia.
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akamwambia: “Kinakuliza nini?”
Yule mtu: “Kilichokusibu.”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah): “Usilie, katika elimu ya Allaah mambo yalikuwa yawe hivi, kisha akasoma:
مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ﴿٢٢﴾
Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umo katika Kitabu kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. [Al-Hadiyd: 22]
Kisha Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akacheka na watu wake wakashangazwa na wakamwambia Hajjaaj naye akaamrisha arejeshwe.
Hajjaaj akamuliza: “Nini kikuchekeshacho?”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akajibu; “Nashangazwa na jeuri yako kwa Allaah na huruma Yake kwako.”
Hajjaaj akasema: “Muuweni!”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akasoma:
إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾
“Hakika mimi nimeelekeza uso wangu kwa Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi nimeelemea haki, nami si katika washirikina.” [Al-An’aam: 79]
Hajjaaj: “Mwelekezeni pasipo Qiblah!”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akasoma:
وَلِلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿١١٥﴾
Na Mashariki na Magharibi ni ya Allaah; basi popote mnapogeuka kuna Wajihi wa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote [Al-Baqarah: 115]
Hajjaaj: “Mpigeni na mlazeni uso chini.”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akasoma:
مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾
Kutokana nayo (ardhi) Tumekuumbeni, na humo Tutakurudisheni, na kutoka humo Tutakutoeni mara nyingine. [Twaahaa: 55]
Hajjaaj: “Mchinjeni!”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah): “Ama mini nashuhudia kuwa laa ilaaha illa Allaah (hapana muabudiwa wa haki ila Allaah) Asiye na mshirika, na Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni mja Wake na Rasuli Wake. Ichukue roho yangu ee Hajjaaj, utanikuta nayo Siku ya Qiyaamah.”
Kisha Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) akamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) akisema: “Ee Rabbi, Usimsalitishe mtu mwengine ili amuue baada yangu.”
Sa’iyd bin Jubayr (Rahimahu Allaah) Alikufa mwaka 95H. Wamekhitalifiana wanahistoria umri wake wa kufariki; wako wanaosema alifariki akiwa na umri wa miaka 49 na wengine wamesema alikufa akiwa na umri wa miaka 57. Alifariki hali ulimi wake ukimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).