27-Swabrun Jamiyl: Subira Za Maimaam - Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah)
27 - Subira Za Maimaam - Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah)
Subira ya Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) ilikuwa zaidi katika kukanusha kwake kuwa Qur-aan imeumbwa.
Imepokewa kuwa Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alimuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenye ndoto akimwambia: “Ee Ahmad! Kwa hakika utatahiniwa hivyo subiri Allaah Atanyanyua elimu yako mpaka Siku ya Qiyaamah.”
Mtihani ulianza baada ya Maamuwn kushika madaraka ya ukhalifa. Maamuwn alielemea katika rai ya Mu’tazilah na akiwakurubisha katika utawala wake.
Mwalimu wa Maamuwn alikuwa ni Abu al-Hudhayl al-‘Allaaf na Qaadhi alikuwa ni Ahmad bin Abi Daawuwd ambao walikuwa viongozi wa Mu’tazilah.
Maamuwn alifuata msimamo wa kuwa Qur-aan imeumbwa lakini alijizuia kuwalazimisha watu na Wanachuoni kukamatana na itikadi hiyo potofu kwa kuchelea fitnah. Hata hivyo alishauriwa na Qaadhi wake, Ibn Abi Daawuwd na baraza lake la watu na hata kukinaishwa.
Maamuwn akamwandikia gavana wake wa Iraaq, Is-haaq bin Ibraahiym na kumuamuru awakusanye wale wote waliokuwa chini yake miongoni mwa ma-Qaadhi na Wanachuoni na awalazimishe kuwa Qur-aan imeumbwa na atakayekataa afungwe, azuiwe au auliwe.
Fitnah hii ikapamba moto huko Iraq. Watu wengi wakafungwa, kuadhibiwa na kuuwawa kwa tendo hilo la Khalifa Maamuwn. Na kuwakaribisha marafiki waovu kiasi cha kumfanya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah kusema; “Sidhani kama Allaah Atamwacha Maamuwn kwa mtihani aliowaingizia Waislam.”
Mtihani wa fitnah hiyo ukawa mkubwa kabisa, Wanachuoni wane walibaki katika msimamo nao ni; Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) na Muhammad bin Nuwh na wengine wawili ambao nao mwishoni walishindwa kuendelea na msimamo wao na kusema kama walivyosema watu.
Maamuwn aliamrisha akamatwe Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) na Muhammad bin Nuwh na wapelekwe katika hali ya kufungwa juu ya ngamia mmoja.
Muhammad bin Nuwh alifariki njiani kabla ya kufika Twarsuws kwa Maamuwn. Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alibakia peke yake. Mjumbe kutoka kwa Maamuwn alimjia na kumwambia: “Khalifa amekutayarishia upanga ambao hajawahi kumuulia mtu yeyote!”
Imaam Ahmad akasema: “Namuomba Allaah Anitosheleze na msaada Wake.” Akamuomba Allaahs akiwa njiani asiuone uso wa Maamuwn na asimkutanishe naye.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipokea du’aa ile na muda si mrefu ikamfikia habari kuwa Maamuwn kafariki kabla ya Imaam Ahmad kukutana naye. Baada ya habari hiyo Imaam Ahmad alirejeshwa jela kwa mara nyingine.
Baada ya hapo ukhalifa ulishikwa na al-Mu’taswim, ambae aliusiwa kumkurubisha Ibn Abi Daawuwd katika majlis yake na kuendelea kushikamana na itikadi ya Uumbwaji wa Qur-aan. Hiyo ndio iliyokuwa itikadi ya watu baada ya hapo, wakati huo Imaam Ahmad akiwa jela.
Imaam Ahmad alikuwa jela na al-Mu’taswim alimtoa jela na kumleta katika majlis pamoja na kumuwekea kikao pamoja na Ibn Abi Daawuwd na Wanachuoni (waovu) kuhusu mjadala wa uumbwaji wa Qur-aan, na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akiwapa dalili zenye kutosheleza kutoka katika Qur-aan yenyewe na Sunnah, na mara kwa mara akiwaambia: “Nipeni dalili kutoka kitabu cha Allaah na Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Siku hiyo majlis ilipita bila muwafaka wowote ule.
Mjadala ule uliendelea kwa muda wa siku tatu, Imaam Ahmad akithibiti pale pale penye haki bila kutetereka na kila akiulizwa: “Unasema nini kuhusu Qur-aan?” Hujibu: “Ni maneno ya Allaah yasiyoumbwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ﴿٦﴾
Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah (Qur-aan), [At-Tawbah: 6]
Na pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
الرَّحْمَـٰنُ ﴿١﴾
Ar-Rahmaan.
عَلَّمَ الْقُرْآنَ ﴿٢﴾
Amefundisha Qur-aan. [Ar-Rahmaan: 1-2]
Na wala Hakusema ‘Khalaqal Qur-aan (Ameumba Qur-aan)’, na pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
يس ﴿١﴾
Yaa Siyn.
وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
Naapa kwa Qur-aan yenye hikmah. [Yaasiyn: 1-2]
Hakusema “Wal-Qur-aanil Makhluwq”. (Na Qur-aan iliyoumbwa)
Baada ya hapo al-Mu’taswim akakusanya Fuqahaa na ma-Qaadhi wote katika nchi wajadiliane na Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) kwa muda wa siku tatu naye mwenyewe akiwepo.
Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alijadiliana nao na kurudisha tuhuma zao dhidi ya Qur-aan kwa hoja thabiti zenye kukata na baada ya hapo al-Mu’taswim akasema: “Ahmad ametushinda!”
Wale washawishi na viongozi waovu wakakoleza fitnah ile kwa kumdhihaki Khalifa al-Mu’taswim nao kwa kusema: “Ahmad amewashinda Makhalifa wawili!” Maneno yale yakamkera sana al-Mu’taswim na akashikwa na hasira.
Na kwa kulinda hadhi yake akamtishia Imaam Ahmad kumuua. Naye Imaam Ahmad akajibu: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Si halali damu ya Muislamu aliyeshuhudia Laa ilaaha illa-Allaah, nami ni Rasuli wa Allaah, ila kwa mambo matatu…)). Sasa kwa nini damu yangu iwe ni halaal nami sijaleta katika hayo? Ee Amiyrul Muuminiyn, kumbuka kisimamo chako kwa Allaah ni kama kisimamo changu sasa hivi kwako.”
Baada ya maneno hayo al-Mu’taswim akanyamaza na kulainika. Ibn Abi Daawuwd akaingiza maneno yake na kusema: “Ukimuacha utakuwa umeacha madhehebu ya Maamuwn, au itaendela kusemwa kuwa amewashinda makhalifa wawili.” Hapo tena akaja juu al-Mu’taswim na akaamrisha kurejeshwa jela Imaam Ahmad kwa mara nyingine tena.
Siku zikapita na ilipofika Ramadhwaan wakamtoa Imaam Ahmad jela na wakaanza kumpiga hali yakuwa yupo katika Swawm. Al-Mu’taswim akawaleta wapiga mijeledi na kumpiga na kila mwenye kumpiga Imaam Ahmad mijeledi miwili hurudi nyuma na kwenda mbele mtu mwingine mpya wa kumpiga mijeledi. Na al-Mu’taswim akiwashadidisha kuendelea kupiga huku akisema kwa nguvu: “Allaah Aikate mikono yenu!” Kisha wakamtoa nguo zake na kubakisha kikoi chake tu na kuendelea kumpiga hadi akazimia. Alipozindukana, wakamchukua na kumpeleka nyumbani kwake akiwa hawezi kutembea kwa yaliyomkuta. Jeraha zake zilipopona akaenda Msikitini akitoa darasa zake na kufundisha Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na baada ya muda fitnah ile ikakoma.
Baada ya muda al-Mu’taswim akafariki na baada ya hapo akatawala Khalifa al-Waathiq Billaah. Ibn Abi Daawuwd na kundi lake la Wanachuoni waovu wakawasiliana na al-Waathiq ili wamburuze katika fitnah, na kweli fitnah ikarudi kwa mara nyingine isipokuwa al-Waathiq hakushughulika na Imaam Ahmad. Baada ya muda si mrefu Imaam Ahmad akapotea katika ukhalifa wa al-Waathiq kwa muda wa miaka mitano. Mwishoni mwa maisha ya al-Waathiq, alirudi kwa Rabb wake na akaongozwa katika hidaaya. Akaikanusha kauli ya kuwa Qur-aan imeumbwa. Kisha haukupita muda akafariki.
Baada ya hapo wakatawala makhalifa wema nao ni Mutawakkil ambaye alitangaza Sunnah na akawaandikia Wanachuoni sehemu mbalimbali kuwa wawakataze watu kujiingiza katika fitnah ile. Kisha tena baada ya muda akatoa tangazo lingine muhimu kwa dola nzima kuachana na bid’ah ile ya itikadi potofu ya kuwa Qur-aan ni kiumbe (imeumbwa). Furaha ikatawala kila sehemu katika dola baada ya tangazo lile, na fitnah na mtihani ule ukaondoka na haki kushinda batili. Ikawa ni hadithi pindi Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alipokuwa akiulizwa wakati ule wa mtihani: “Ee Aba Abdillaah! Batili imeshinda haki.” Yeye alikuwa akijibu: “Wa-Allaahi batili haiwezi kushinda haki.”
Kwa hakika katika masomo muhimu ya mtihani huu, ni kule kuthibiti kwa Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) juu ya haki na kusubiri katika balaa lililomkumba. Kwa hakika Imaam Ahmad alishinda kwa iymaan na ushujaa aliokuwa nao na zikaanguka mbele yake serikali kubwa ulimwenguni katika wakati wake. Na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akatoka katika mtihani huu kama vile upanga unapotoka katika ala yake au kama mbalamwezi kwenye usiku wa kiza, na akaweza kuzuia tatizo kubwa ambalo lingeukumba Ummah wa Kiislamu. Na hivyo kubaki ‘Aqiydah ya Ahlu Sunnah Wal-Jamaa’ah ikiwa ni safi isiyochafuliwa na takataka za Muu’tazilah na upotofu wao na wale wote waliowafuata.
Siku zikapita na Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akafariki kama walivyofariki kabla yake Maamuwn, al-Muutaswim na al-Waathiq na wale majambazi waliojivika jina la uanachuoni nao wakafa mifano ya Ahmad bin Abi Daawuwd na wengineo.
Swali linalijitokeza hapa ni kuwa: Historia imetuhifadhia nini juu ya maisha ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) na maisha ya majambazi wale?’ Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) alikuwa ni Mwanachuoni katika Wanachuoni wakubwa wa Kiislamu, katika zama zake, baada ya kifo chake hadi wakati huu tuliokuwa nao.
Mwisho wake, jeneza lake lilikuwa ni dalili na alama za Uislamu na elimu yake, vitabu vyake vikabakia hadi kwenye zama zetu leo hii kama kwamba bado anaishi nasi. Kinyume chake historia imetunukulia mwisho mbaya wa wale walioshiriki katika fitnah ile, na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atawalipa hapa duniani kabla ya Aakhirah.
Ama Qaadhi wa Mu’tazilah Ahmad bin Abi Daawuwd ambaye akitoa fatwa ya ruhusa ya kupigwa kwa ‘Ulamaa na kuwekwa kwao jela na kuwaua, aliulizwa baada ya al-Waathiq kumuua Imaam Ahmad bin Naswri al-Khuza’iy akasema: “Allaah (Amenipiga) Ameniadhibu kwa kupooza!” Mtu huyu alipata shida na tatizo hilo la kupooza akawa kitandani mwake amepotelewa na fahamu kwa muda wa miaka minne kabla ya kufariki kwake.