Anataka Kumpa Mtoto Wake Jina La Mkristo Kwa Madai Alikuwa Mtu Mwema

 

SWALI:

 

Asalaam aleikum,Alhamdullilah tunamshukuru allah kwa kutujalia website ya alhidaaya kwani inayuelimisha jinsi ya kumja mungu wetu.Mimi nimependa sana jina la Seth alikuwa baba mkwe wangu na alikuwa mkarimu sana na mwenye huruma na mpole mpenda watu lakini ni mkristo mama mkwe wangu ambaye alikuwa muislam alizaa na huyo baba (mwenyezi Mungu awasamehe kwa huruma zake).Natamani Allah akinijalia mtoto wa kiume nimuite SETH je inafaa? nimejaribu kuangalia maana yake nikaona si mbaya ila naomba fatwaa zaidi.

  


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kutokana na Swali lako, haipasi kabisa kumpa mtoto wa Kiislamu jina la Dini nyinginezo hata kama jina hilo litaonekana zuri kwa mtazamo wake, vilevile haifai kumpa jina la asiyekuwa Muislamu kwa madai mtu huyo alikuwa mwema! Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza sana sisi kuwaiga makafiri katika mambo yao na kakemea sana suala la kujifananisha nao.

Na Muislamu mwenye iymaan ya Dini yake anatakiwa awe na fakhari na Dini yake na si kuacha mafunzo ya Dini yake na kutafuta ya kikafiri. Na tambua kwamba haimaanishi kuwa unapompa mtu jina la mtu mwema kwamba naye atakuwa mwema, si lazima, isipokuwa sisi Waislamu tunataraji hivyo kwa kuwapa watoto majina ya Maswahaba na waja wema waliotangulia na huku tukijitahidi waige mienendo yao. Kadhaalika, mtoto anapokuwa na jina lake jema, kimantiki linamsukuma ajinasibishe na kujifananisha na jina lake jema ambalo linawakilisha sifa au kiumbe aliyekuwa mwema katika Dini hii. Ndio kukawa na umuhimu mkubwa sana wa kuwapa watoto majina mazuri ya watu wema katika Dini.

 

Uislamu umetupa mwongozo mzuri kabisa wa kuwapa majina watoto wetu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Jiiteni majina ya Mitume. Na majina yapendezayo zaidi kwa Allaah ni ‘Abdullaah na ‘Abdur-Rahmaan” [Abu Daawuwd na an-Nasaa’iy].

Majina ya Mitume wengi imetajwa katika Qur-aan. Hutoweza kukosa humo kupata jina litakalokupendezea. Vile vile unaweza kuwapa majina ya Maswahaba, au majina ya Maimaam wa Kiislamu, na majina ya Waja Wema waliotangulia. Na Kwa hiyo kuna chaguo kubwa na pana ya majina ya Kiislamu. Sasa iweje basi Muislamu ayaache au akose kupata jina zuri katika Dini yake na aelekee kutafuta majina ya wasio Waislamu?

 

Kadhaalika, tunawanasihi sana Waislamu kutojichanganya na wasio Waislamu na kujenga mahusiano na urafiki nao, au hata kuwafanya ni wapenzi na wasiri wao. Allaah Amelikemea sana hili kwenye Aayah kadhaa, na Mtume Wake vilevile amelikataza na ametaka sisi Waislamu tusuhubiane na Waumini na tuchague marafiki wazuri hata katika Waislamu wenzetu. Tusifanye urafiki na ukaribu na makafiri na vilevile hata katika Waislamu tuchague marafiki wema na wale wenye kufuata Dini na wenye maadili mema. Matatizo mengi na mambo mfano wa swali kama hili, huchangiwa na kujichanganya na makafiri na hata kuvutika na mambo yao.

 

Kwa manufaa zaidi tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo:

 

Kumpa Mtoto Jina Lisilokuwa La Kiislamu Inafaa?

 

Fiqh Ya Kuwaita Majina Watoto

 

Majina Ya Watoto Na Maana Yake

 

Kumwita Mtoto Jina La Maulaana

 

Hukmu Ya Kuwapa Watoto Majina Ya Allaah Au 'Abdur-Rasuul, 'Abdul-Husayn

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share