Zingatio: Mwaka Mpya: Nyinyi Mna dini Yenu Nasi Tuna Diyn Yetu

 

Zingatio: Mwaka Mpya: Nyinyi Mna dini Yenu Nasi Tuna Diyn Yetu

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Si Qur-aan, Sunnah, Swahaba, Mataabi’iyn, Mataabi’ Tabi’iyn, na Salafus-Swaalih kwa ujumla wala ’Ulaamaa wa Kiislamu waliohalalisha kujumuika na makafiri kwenye sherehe zao za Kikafiri.

 

Miongoni mwa sherehe ambazo zinafurahikiwa mno na Waislamu ni Mwaka Mpya wa Kikiristo ingawa haimo sikukuu hiyo katika orodha ya sherehe za Kiislamu. Masuala mengi yanabaki kichwani bila ya majibu: “Ni kwa sababu gani haswa Muislamu ashiriki sherehe hizo? Kwani Mola Mtukufu Hakuwatunukia Waislamu siku zao za kusherehekea? Je, Mtume hakujua kwamba kitakuja kizazi ambacho hakitatofautisha Uislamu na Ukafiri?”

 

Kutokana na ujinga wetu Waislamu ndio maana tunarushiwa mabomu kwenye ardhi zetu, tunaendelea kutawaliwa, kuteswa, kunyanyaswa na mengineyo. Hao wanaotutesa ndio tunaoshirikiana nao kwenye tafrija zao za uzushi. Yote haya yanatokana na Waislamu kuacha kutambuwa kwamba Uislamu wao ni kamili, hautaki viraka wala kuongezewa matambara. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]

 

Pia Qur-aan imeshakata kauli kwamba makafiri wana dini yao na sisi tuna Uislamu wetu. Yashangaza kuwaona Waislamu wakiwa hawaelewi ama wanajitia upofu wa mafundisho haya:

 

قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ ﴿١﴾لَا أَعْبُدُ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٢﴾وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٣﴾وَلَا أَنَا عَابِدٌ مَّا عَبَدتُّمْ ﴿٤﴾وَلَا أَنتُمْ عَابِدُونَ مَا أَعْبُدُ ﴿٥﴾لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾

Sema: Enyi makafiri! Siabudu yale mnayoyaabudu. Na wala nyinyi si wenye kuabudu Yule Ninayemwabudu. Na wala mimi si mwenye kuabudu yale mnayoabudu.  Na wala nyinyi si wenye kuabudu Yule Ninayemwabudu. Nyinyi mna dini yenu; nami nina Dini yangu. [Al-Kaafiruwn: 1-6]

 

Kwa kuongezea, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametubainishia kwamba zama zetu zitakuwa zinachanganya mambo tukashindwa kuchambua baina ya haqq na baatwil. Hizi ndio zama za kukamata vyema Sunnah iliyoachwa na Nabiy pamoja na kuachana na mambo yote yenye mashaka matupu:

 

"Mtafuata Sunnah (nyendo) za watu waliokuwa kabla yenu, kiganja kwa kiganja, mkono kwa mkono, hata wakiingia kwenye shimo la kenge mtawafuata".  Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah, 'Je, Unamaanisha Mayahudi na Manaswara?' Akasema: "Kwani nani zaidi ya wao?".

 

Kwa upande wa Swahaba, tunamkuta jemadari Sayyidna ‘Umar bin Al-Khattwaab akitwambia:

 

"Jiepusheni na maadui wa Allaah katika sherehe zao."

 

Ni vyema pia kunukuu maneno ya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah:

 

"Sisi Waislamu tusifanye jambo lolote lilokuwa si la kawaida katika siku hizi. Iwe kama siku yoyote nyingine katika maisha yetu bila ya kuwa imekhusishwa na lolote kama mfano wao watu wa Vitabu walivyokuwa hawasherehekei wala kuzifanya siku zetu za 'Iyd kuwa ni khaswa (maalum) kwao." 

 

Ya Allaah tunakuomba  kutokana na Nuru ya Wajihi wako, ambayo inaangazia mbingu na inaondoa kiza na kutawala  mambo yote ya dunia na akhera ili hasira Yako isitufikie au ghadhabu Yako isituangukie; utuongoze katika njia iliyonyooka na utusamehe madhambi yetu. Kwa hakika tunakiri kwamba hakuna mamlaka wala nguvu na uwezo ila Wako peke Yako.

 

Wa Allaahu A'alam

 

Share