Kupangusa Uso Baada Ya Kusoma Du’aa Inafaa?
Kupangusa Uso Baada Ya Kusoma Du’aa Inafaa?
SWALI:
Assalam aleikum
ningependa munifahamishe kuhusu mtu kufuta uso wake akimaliza dua wakati anaposema Amin, je kuna hadith yoyote ama kithibitisho kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) alikuwa akifanya hivyo? Jaza yenu iko kwa Allaah subhanahuu wa Ta'aalaa kwa kazi munayo fanya, Shukran
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kupangusa uso baada ya kuomba du’aa si kitendo cha Sunnah, na Hadiyth nyingi zilizopokelewa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aailihi wa sallam) alipokuwa akiomba du’aa zake hakuwa akipangusa uso wake baada ya du’aa. Na hata katika Khutbah ya Ijumaa au Swalaah ya Istisqaa haikuthibiti kwamba alipangusa mikono yake usoni. Hadiyth moja au mbili zilizosimuliwa kuhusu kitendo hiki zimechambuliwa kuwa ni Hadiyth dhaifu, na 'ulaamaa wamekubaliana kwamba kitendo hiki hakipo katika Shari’ah.
Na hata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akimaliza Swalaah zake na kutoa salaam, hakuwa kamwe akipangusa uso wake kama ilivyo ada ya Waislamu wengi hivi leo wanavyofanya na hawajui kwanini wanafanya hivyo na hata ukimuuliza mtu anashindwa kukupa jibu, na wengine wanajibu kuwa wamejikuta wakikuwa na kuona ikifanywa hivyo na wao wanafanya. Muislamu anapaswa kufanya matendo yake yote ya ‘Ibaadah kwa dalili na si kwa kubahatisha au kuiga bila dalili.
Na Allaah Anajua zaidi