002-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Allaah Hupokea Tawbah Za Waja Usiku Na Mchana

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Alhidaaya.com 

 

Hadiyth Ya 2

Allaah Hupokea Tawbah Za Waja Usiku Na Mchana

 

 

عَنْ أَبِي مُوسَى عَبْدِ الله بنِ قَبَسٍ الأَشْعَرِيِّ  (رضي الله عنه) عن النَّبيّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قال: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا)) رواه مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsaa ‘Abdillaah bin Qays Al-Ash‘ariyy (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Anakunjua Mkono Wake usiku ili Apokee tawbah ya mkoseaji mchana. Na Anakunjua Mkono Wake mchana ili Apokee tawbah ya mkoseaji usiku mpaka jua lichomoze Magharibi [mahali linapokuchwa])) [Muslim]

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

1. Umuhimu wa mja kukimbilia kutubu anapofanya maasi mchana au usiku. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ وَجَنَّةٍ عَرْضُهَا السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ أُعِدَّتْ لِلْمُتَّقِينَ

Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Rabb wenu na Jannah upana wake ni wa mbingu na ardhi imeandaliwa kwa wenye taqwa. [Aal-‘Imraan 3: 133]

 

Na pia rejea: At-Tahriym (66: 8), An-Nuwr (24: 31).

 

 

2. Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja Wake kuwapa muda wa kutubia maasi, lau sivyo Angeliwaadhibu na kuwaangamiza hapo hapo wanapotenda maasi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۖ فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِعِبَادِهِ بَصِيرًا ﴿٤٥﴾

Na lau Allaah Angeliwaadhibu watu kwa sababu ya waliyoyachuma, Asingeliacha juu ya ardhi kiumbe chochote kitembeacho, lakini Anawaakhirisha mpaka muda maalumu uliokadiriwa; utakapofika muda wao, basi hakika Allaah daima ni Mwenye kuona waja Wake. [Faatwir (35: 45)]

 

Rejeja pia:  An-Nahl (16: 61).

 

 

3. Rahma ya Allaah kwa waja Wake kutokutofautisha wakati wa tawbah japokuwa maasi mengine yanazidi mengineyo.

 

 

4. Tawbah inaendelea kupokelewa hadi milango ifungwe: Hadiyth: 

 

وعن أبي عبد الرحمن عبد الله بنِ عمَرَ بنِ الخطابِ رضيَ اللهُ عنهما عن النَّبي صلى الله عليه وسلم، قَالَ: ((إِنَّ الله عز وجل يَقْبَلُ تَوبَةَ العَبْدِ مَا لَمْ يُغَرْغِرْ)). رواه الترمذي، وَقالَ: ((حديث حسن)) 

Abuu ‘Abdir-Rahmaan, ‘Abdullaah bin ‘Umar bin Al-Khattwaab  (رضي الله عنهما)    amehadithia kwamba:  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)    amesema:  “Hakika Allaah  ‘Azza wa Jallaa Huikubali tawbah ya mja madamu roho yake haijafika kooni.” [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth hii ni Hasan, Ibn Maajah, Ahmad, na imepewa daraja ya Swahiyh na Al-Albaaniy]

 

Na pia:

 

عن أبي هُريرةَ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ تَابَ قَبْلَ أنْ تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِها تَابَ اللهُ عَلَيهِ)). رواه مسلم

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kutubia kabla ya jua kuchomoza upande wa Magharibi, Allaah Atamkubalia tawbah yake.” [Muslim]

 

 

5. Hii inaonyesha mapenzi makubwa ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwapatia waja Wake fursa hii ya dhahabu ambayo haifai kupotezwa na waja wenyewe.

 

 

6. Hadiyth inatoa mafunzo kwa Muislamu kutokumhukumu mwenziwe kuwa hatoghufuriwa madhambi yake. Rejea Hadiyth namba (99).

 

 

7. Mja hata afanye madhambi makubwa vipi, asikate tamaa na Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى), kwani Yeye Hughufuria madhambi yote. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ﴿٥٣﴾

Sema: Enyi waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote; hakika Yeye Ndiye Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Az-Zumar 39: 53]

 

 

8. Fadhila tele za tawbah zimetajwa katika Qur-aan na Sunnah, miongoni mwazo ni.

 

Kauli za Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]

 

Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) aliamrishwa awaambie watu wake:

 

وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُمَتِّعْكُم مَّتَاعًا حَسَنًا إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى وَيُؤْتِ كُلَّ ذِي فَضْلٍ فَضْلَهُ ۖ وَإِن تَوَلَّوْا فَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ كَبِيرٍ﴿٣﴾

Na kwamba: “Mwombeni Rabb wenu maghfirah kisha tubuni Kwake, Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu uliokadiriwa; na Atampa kila mwenye fadhila, fadhila Zake. Na mkikengeuka, basi hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa.” [Huwd: 3]

 

Nabiy Nuwh  (عليه السلام) alipowalingania watu wake aliwaambia watubie kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na akawatajia fadhila tele:

 

فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾

Nikasema: “Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu; hakika Yeye ni Mwingi mno wa kughufuria.

 

يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾

“Atakutumieni mvua tele ya kuendelea.”

 

وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾

“Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito.” [Nuwh: 10-12]

 

 

Na Nabiy Huwd (عليه السلام) aliwaambia watu wake:

 

وَيَا قَوْمِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ وَلَا تَتَوَلَّوْامُجْرِمِينَ﴿٥٢﴾

“Na enyi kaumu yangu!  Mwombeni maghfirah Rabb wenu, kisha tubieni Kwake, Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua tele ya kumiminika na Atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu, na wala msikengeuke mkawa wahalifu.” [Huwd: 52]

 

وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُمَتِّعْكُم مَّتَاعًا حَسَنًا إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى وَيُؤْتِ كُلَّ ذِي فَضْلٍ فَضْلَهُ ۖ وَإِن تَوَلَّوْا فَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ كَبِيرٍ﴿٣﴾

Na kwamba: “Mwombeni Rabb wenu maghfirah kisha tubuni Kwake, Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu uliokadiriwa; na Atampa kila mwenye fadhila, fadhila Zake. Na mkikengeuka, basi hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa.” [Huwd: 3]

 

Na Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

 عن ابنِ عباسٍ رضي الله عنهما أنَّ رَسُولَ الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ: ((لَوْ أنَّ لابنِ آدَمَ وَادِيًا مِنْ ذَهَبٍ أحَبَّ أنْ يكُونَ لَهُ وَادِيانِ، وَلَنْ يَمْلأَ فَاهُ إلا التُّرَابُ، وَيَتْوبُ اللهُ عَلَى مَنْ تَابَ)). مُتَّفَقٌ عليه

'Abdullaah bin ‘Abbaas na Anas bin Maalik (رضي الله عنهما) wamehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Lau mwana Aadam angalikuwa na bonde la dhahabu, angalipendelea awe na mabonde mawili, wala hakuna kitakachoweza kumtosheleza mdomo wake isipokuwa ni mchanga. Na Allaah Humkubalia tawbah ya yule mwenye kutubia.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na pia:

 

عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((الَلَّهُ أَشَدُّ فَرَحًا بِتَوْبَةِ عَبْدِهِ حِينَ يَتُوبُ إِلَيْهِ مِنْ أَحَدِكُمْ كَانَ عَلَى رَاحِلَتِهِ بِأَرْضِ فَلاَةٍ فَانْفَلَتَتْ مِنْهُ وَعَلَيْهَا طَعَامُهُ وَشَرَابُهُ فَأَيِسَ مِنْهَا فَأَتَى شَجَرَةً فَاضْطَجَعَ فِي ظِلِّهَا قَدْ أَيِسَ مِنْ رَاحِلَتِهِ فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذَا هُوَ بِهَا قَائِمَةً عِنْدَهُ فَأَخَذَ بِخِطَامِهَا ثُمَّ قَالَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ: "اللَّهُمَّ أَنْتَ عَبْدِي وَأَنَا رَبُّكَ" ‏ أَخْطَأَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ)) مسلم

 

Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Allaah Hufurahikiwa mno na tawbah ya mja Wake wakati anapotubia Kwake kuliko furaha ya mmoja wenu aliyekuwa amempanda mnyama wake kwenye jangwa (la joto kali hakuna mtu), kisha mnyama huyo aliyebeba chakula chake na maji yake akampotea, na akakata tamaa kabisa ya kumpata tena. Akaenda kwenye mti, akalala chini ya kivuli chake huku akiwa amekata tamaa kabisa ya kumpata tena mnyama wake. Akiwa katika hali hiyo (ya kutojua nini la kufanya), mara anashtuka kumwona huyo amesimama mbele yake, akaikamata hatamu yake, na kwa ile furaha akasema:  "Ee Allaah, Wewe ni mja wangu na mimi ni Rabb wako.” Alikosea (kumshukuru Rabb wake) kwa wingi wa furaha aliyokuwa nayo.” [Muslim]

 

Na pia:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِيمَا يَحْكِي عَنْ رَبِّهِ عَزَّ وَجَلَّ قَالَ: ((أَذْنَبَ عَبْدٌ ذَنْبًا فَقَالَ: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي،  فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى:  أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ فَقَالَ:  أَيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي،  فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: عَبْدِي أَذْنَبَ ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ فَقَالَ: أَيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي،  فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ. اعْمَلْ مَا شِئْتَ فَقَدْ غَفَرْتُ لَكَ)) البخاري و مسلم

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kuhusu mambo aliyohadithia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  kutoka kwa Rabb Wake (‘Azza wa Jalla) kwamba ((Mja wa Allaah alifanya dhambi na akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. Kisha akarudi tena kufanya dhambi akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. Kisha akarudia tena dhambi na akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. (Allaah Akasema): Fanya utakavyo, kwani Nimekughufuria)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

9. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akitubia mara 70 au mara 100 kwa siku, hivyo basi sisi tunapaswa kutubia zaidi ya hivyo:

عن أبي هريرةَ رضي الله عنه قَالَ: سمعْتُ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((واللهِ إنِّي لأَسْتَغْفِرُ الله وأَتُوبُ إِلَيْه في اليَوْمِ أَكْثَرَ مِنْ سَبْعِينَ مَرَّةً)). رواه البخاري

Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)   akisema: “Wa-Allaahi mimi namuomba Allaah maghfirah na natubia Kwake zaidi ya mara sabini kwa siku.” [Al-Bukhaariy]

 

Na pia:

 

وعن الأَغَرِّ بنِ يسار المزنِيِّ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((يَا أَيُّهَا النَّاسُ، تُوبُوا إِلى اللهِ واسْتَغْفِرُوهُ، فإنِّي أتُوبُ في اليَومِ مائةَ مَرَّةٍ)). رواه مسلم.

Al-Agharri bin Yasaar Al-Muzaniyy (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)    amesema: “Enyi watu, tubieni kwa Allaah na mumuombe maghfirah. Hakika mimi natubia Kwake mara mia kwa siku.” [Muslim]

 

 

Share