005-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kuvunjia Kiapo Kitendo Kiovu Kwa Kilicho Chema
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 5
Kuvunjia Kiapo Kitendo Kiovu Kwa Kilicho Chema
عَنْ أبي طريفٍ عَدِيَّ بْنَ حَاتِمٍ الطَّائي (رضي الله عنه) قال: سَمِعْتُ رسول اللَّهِ (صلى الله عليه و آله وسلم) يَقُولُ: ((مَنْ حَلَفَ عَلَى يَمِينٍ ثُمَّ رَأَى أَتْقَى لِلَّهِ مِنْهَا فَلْيَأْتِ التَّقْوَى)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Twariyf ‘Adiyy bin Haatim (رضي الله عنه) amesema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Atakayeapa yamini [kufanya jambo] kisha akaona linalomridhisha zaidi Allaah kuliko aliloliapia, basi amche Allaah kwa kufanya linalomridhisha Allaah)). [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Aayah na Hadiyth nyingi zimesisitiza kuwajibika kuwa na taqwa na faida zake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَقُولُوا قَوْلًا سَدِيدًا ﴿٧٠﴾
Enyi walioamini! Mcheni Allaah na semeni kauli nyofu ya haki.
يُصْلِحْ لَكُمْ أَعْمَالَكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
Atakutengenezeeni ‘amali zenu, na Atakughufurieni madhambi yenu; na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu. [Al-Ahzaab (33: 70-71)]
Rejea pia: At-Tawbah (9: 119), Al-Maidah 95: 35).
2. Mwenye kuazimia kufanya maasi asiyatende japokuwa ameyaapia kutenda.
3. Kuruhusika kuvunja kiapo na kafara zake kama ilivyotajwa katika kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٨٩﴾
Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa. Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu. Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu. Hivyo ndivyo Allaah Anavokubainishieni Aayaat (na hukmu) Zake ili mpate kushukuru. [Al-Maaidah (5: 89)]
Rejea pia Hadiyth namba (92), (102), (125).
4. Kujizua kuapa katika maasi kama kuapa katika kumvutia mteja biashara au katika kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى):
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اَللَّهِ (صَلَّى اَللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((الْحَلِفُ مَنْفَقَةٌ لِلسِّلْعَةِ مَمْحَقَةٌ لِلْكَسْبِ)) أَخْرَجَاهُ
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Kwa kuapa, [muuzaji] huenda akamshawishi mnunuaji kununua bidhaa, lakini kunafuta Baraka za Allaah)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
وَعَنْ سَلْمَانَ: أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ (صَلَّى اَللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((ثَلاثَةٌ لاَ يُكَلِّمُهُمْ اَللَّهُ وَلاَ يُزَكِّيهِمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ: أُشَيمِطٌ زَانٍ وَعَائِلٌ مُسْتَكْبِرٌ وَرَجُلٌ جَعَلَ اَللَّهَ بِضَاعَتَهُ لاَ يَشْتَرِي إِلاَّ بِيَمِينِهِ وَلاَ يَبِيعُ إِلاَّ بِيَمِينِه)) رَوَاهُ اَلطَّبَرَانِيُّ بِسَنَدٍ صَحِيحٍ
Na Imepokelewa kutoka kwa Salmaan kwamba: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watu watatu ambao Allaah Hatowasemesha, wala Hatowatakasa, na watapata adhabu kali: Mzinifu mzee, maskini anayetakabari, na mtu aliyejaaliwa na bidhaa, lakini hanunui ila kwa kuapa [wa-Allaahi] na hauzi ila kwa kuapa [wa-Allaahi)) [At-Twabaraaniy kwa isnaad Swahiyh]
Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mwenye kuapa akasema katika kiapo chake: Naapa kwa Laata na ‘Uzzaa (majina ya waabudiwa wa uongo) aseme: Laa ilaaha illa Allaah. Na atakayemwambia mwenzake: Njoo tuchezeshe kamari, basi atoe swadaqah.” [Al-Bukhaariy]
5. Umuhimu wa kupata radhi za Allaah (سبحانه وتعالى) kuliko jambo jengine lolote lile.