008-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kukimbilia Kutoa Swadaqah Kabla Ya Mauti

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

Hadiyth Ya 8  

Kukimbilia Kutoa Swadaqah  Kabla Ya Mauti

www.alhidaaya.com

 

 

عن أبي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  قَالَ: جَاءَ رَجُلٌ إِلَى النَّبِيِّ (صلى الله عليه و آله وسلم) فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّهِ, أَيُّ الصَّدَقَةِ أَعْظَمُ أَجْرًا؟ قَالَ: ((أَنْ تَصَدَّقَ وَأَنْتَ صَحِيحٌ شَحِيحٌ تَخْشَى الْفَقْرَ وَتَأْمُلُ الْغِنَى وَلاَ تُمْهِلُ حَتَّى إِذَا بَلَغَتْ الْحُلْقُومَ قُلْتَ لِفُلاَنٍ كَذَا وَلِفلاَنٍ كَذَا وَقَدْ كَانَ لِفُلاَنٍ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  amesema: “Mtu mmoja alikuja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Ni swadaqah ipi yenye ujira mkubwa zaidi?  Akasema: ((Ni utoe swadaqah nawe umzima, unataka mali bado, unakhofia ufukara na unatarajia utajiri. Wala usichelewe mpaka roho ikafika kwenye koo, ukaanza kusema: fulani ana haki kadhaa na fulani ana haki kadhaa na fulani alikuwa ana haki kadhaa)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

1. Swadaqah ya aliye mzima ni bora kuliko ya mgonjwa kwa sababu aghlabu bin Aadam anakuwa mchoyo na bakhili anapokuwa katika afya kamili. Hivyo, atakapotoa wakati yu mzima itakuwa ni swadaqah ya niyyah safi na mapenzi ya kutoa kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

 

2. Kukimbilia kutenda mema wakati una umri na siha kabla ya kufikwa na mtihani wa magonjwa na ufukara. Rejea: Al-Baqarah (2: 148).

 

Na amrisho la kutoa swadaqah kabla ya kufika siku ambayo halitomfaa mtu lolote. Rejea: Al-Baqarah (2: 254).

 

 

3. Kukimbilia kutoa swadaqah kabla ya kufikwa na mauti kama Anavyoonya Allaah (سبحانه وتعالى).

 

وَأَنفِقُوا مِن مَّا رَزَقْنَاكُم مِّن قَبْلِ أَن يَأْتِيَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوْلَا أَخَّرْتَنِي إِلَىٰ أَجَلٍ قَرِيبٍ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ الصَّالِحِينَ﴿١٠﴾

Na toeni katika yale Tuliyokuruzukuni kabla hayajamfikia mmoja wenu mauti akasema: “Rabb wangu! Lau Ungeliniakhirisha mpaka muda wa karibu hivi, basi ningetoa swadaqah na ningelikuwa miongoni mwa Swalihina.”

 

وَلَن يُؤَخِّرَ اللَّـهُ نَفْسًا إِذَا جَاءَ أَجَلُهَا ۚ وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ﴿١١﴾

Lakini Allaah Haiakhirishi kamwe nafsi yeyote inapokuja ajali yake na Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [ Al-Munaafiquwn (63: 10-11).]

 

 

4. Mali ya kudumu khasa ni ile anayoitoa Muislamu kabla ya kufariki kwake, ama baada ya hapo ni mali ya warithi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ ۖ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ ۗ  

Mlivyo navyo nyinyi vinatoweka, na vilioko kwa Allaah ni vya kubakia. [An-Nahl (16: 96)]

 

 

Pia rejea Hadiyth namba (54), (62), (71), (77).  

 

Pia Hadiyth imepokelewa kutoka kwa Mutwarrif: ((Bin Aadam husema: Mali yangu, mali yangu!  Ee bin Aadam! Je, una mali yoyote isipokuwa uliyoimaliza, uliyoitumia, uliyoivaa kisha ikachafuka, au [bora mali] uliyoitolea swadaqah ikatangulizwa?)) [Muslim]

 

 

5. Kukumbuka mauti na kuyakhofia kila mara khasa unapotaka kufanya jambo jema au kutenda ovu.

 

 

6. Kutoa wakati unaaga dunia hakuruhusiwi ki-shariy’ah, na chochote utakachotoa wakati huo kuwapatia ahli yako na jamaa, hakitahesabiwa, kwani Allaah (سبحانه وتعالى) tayari Ashampatia kila mmoja haki yake kutoka kwa aliyefariki.

 

 

7. Inafaa mja atumie vyema neema ya afya, uzima na mali, kwani hivi ni vitu ambavyo havidumu. Na ikiwa hatoweza kuvitumia kwa maslahi yake na kujikurubisha kwa Allaah (سبحانه وتعالى), basi atakuwa amekhasirika. Rejea Hadiyth namba (9).

 

Share