031-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Du’aa Ya Malaika Kila Siku Kwa Mtoaji Sadaka Na Mzuiaji

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 31

 

Du’aa Ya Malaika Kila Siku Kwa Mtoaji Sadaka Na Mzuiaji

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه)  أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَا مِنْ يَوْمٍ يُصْبِحُ الْعِبَادُ فِيهِ إلاَّ مَلَكَانِ يَنْزِلاَنِ فَيَقُولُ أَحَدُهُمَا: اللَّهُمَّ أَعْطِ مُنْفِقًا خَلَفًا. وَيَقُولُ الأَخَرُ: اللَّهُمَّ أَعْطِ مُمْسِكًا تَلَفًا)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Kila siku inayowapambaukia watu kuna Malaika wawili wanateremka, mmoja wao akiomba: Ee Allaah! Mwenye kutoa [sadaka] mlipe zaidi. Na mwengine huomba: Ee Allaah! Mwenye kuzuia mpe hasara)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Inapendekezeka kutoa sadaka kila siku ili kupata du’aa ya Malaika na kukhofu kuombewa hasara. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ ﴿٥﴾

Basi yule anayetoa (mali) na akamcha Allaah.

 

وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ ﴿٦﴾

Na akasadikisha Al-Husnaa.

 

فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ ﴿٧﴾

“Basi Tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi”

 

وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ ﴿٨﴾

Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza.  

 

وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ ﴿٩﴾

Na akakadhibisha Al-Husnaa.

 

فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ ﴿١٠﴾

Na Tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.

 

وَمَا يُغْنِي عَنْهُ مَالُهُ إِذَا تَرَدَّىٰ ﴿١١﴾

Na itamsaidia nini mali yake atakapoporomoka kuangamia (motoni).  [Al-Layl (92: 5-11)]

 

 

 

2. Allaah (سبحانه وتعالى) Ametoa ahadi kumwongezea mwenye kutoa mali yake. Rejea: Al-Baqarah (2: 245, 261), Al-Hadiyd (57: 11), Sabaa (34: 39).

 

 

3. Inafaa kumuombea mtoaji sadaka, Allaah (سبحانه وتعالى) Amlipe zaidi kwa alichotoa, na du’aa kwa bakhili anayezuia kutoa katika Njia ya Allaah  (سبحانه وتعالى) hasara panapohitajika.

 

 

4. Sadaka ni katika ‘amali bora kabisa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى), kwani Ameitaja sana katika Qur-aan na hata kwamba Ameitanguliza kabla ya nafsi katika Aayah za Jihaad.

 

Rejea: An-Nisaa (4: 95), At-Tawbah (9: 20, 41, 81), Al-Hujuraat (49: 15), As-Swaff (61: 11).

 

 

5. Fadhila tele za kutoka sadaka katika Qur-aan na Sunnah. Rejea Hadiyth namba (32), (62).

Share