036-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Hana Iymaan Na Hatoingia Jannah Mwenye Kumtendea Jirani Shar

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 36

 

Hana Iymaan Na Hatoingia Jannah Mwenye Kumtendea Jirani Shari

 

Alhidaaya.com

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((وَاللَّهِ لاَ يُؤْمِنُ، وَاللَّهِ لاَ يُؤْمِنُ،  وَاللَّهِ لاَ يُؤْمِنُ!))  قِيلَ: مَنْ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟  قَالَ: الَّذِي لاَ يَأْمَنُ جَارُهُ بَوَائقَهُ)) متفق عليه

 وَفِي رِوَايَة: ((لاَ يَدْخُلُ الْجَنَّةَ مَنْ لاَ يَأْمَنُ جَارُهُ بَوَائِقَهُ)) مسلم

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Wa-Allaahi hakuamini (hana Iymaan). Wa-Allaahi hakuamini, Wa-Allaahi hakuamini!)) Akaulizwa: Nani ee Rasuli wa Allaah?  Akasema: ((Ambaye jirani yake hasalimiki na shari zake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Na katika riwaayah nyengine: ((Hatoingia Jannah ambaye jirani yake hasalimiki na shari zake)) [Muslim]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Uislamu unasisitiza kumtendea wema jirani. Umuhimu wake hadi kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ameapa kwa Allaah! Na katika Hadiyth nyengine:

 

عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَا زَالَ جِبْرِيلُ يُوصِينِي بِالْجَارِ حَتَّى ظَنَنْتُ أَنَّهُ سَيُوَرِّثُهُ)). متفق عليه

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رضي الله عنهما) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Jibriyl hakuacha kuniusia jirani mpaka nikadhani kuwa atamrithisha [mali yangu])). [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

2. Mojawapo ya uthibitisho wa Iymaan ya Muumin ni kutomuudhi jirani.

 

 

3.Kumfanyia wema jirani ni sababu mojawapo ya kuingia Jannah, na kinyume chake ni kuingia motoni.

 

4. Muislamu anatakiwa ajiepushe na sifa mbaya ya kuudhi mtu na awe mwenye tabia njema na mwenye kulinda haki za watu.

 

 

5. Jirani ni aliye ubavuni, mtaani au hata aliye mbali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

 وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا ۖ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا وَبِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَالْجَارِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَالْجَارِ الْجُنُبِ وَالصَّاحِبِ بِالْجَنبِ وَابْنِ السَّبِيلِ وَمَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ مَن كَانَ مُخْتَالًا فَخُورًا ﴿٣٦﴾

Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni ihsaan wazazi wawili na jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini na jirani mwenye ujamaa na jirani asiye na ujamaa na rafiki wa karibu, na msafiri aliyeishiwa masurufu, na wale iliyowamiliki mikonoyenu ya kulia. Hakika Allaah Hapendi mwenye majivuno mwenye kujifakharisha.  [An-Nisaa (4: 36)]

 

 

6. Uislamu haukubagua kufanya wema hata kwa jirani asiye Muislamu anapaswa kutendewa wema.

Rejea: Al-Mumtahinah (60: 8-9).

 

 

7. Kumfanyia wema jirani na kutomuudhi ni katika uthibitisho wa Iymaan. Na Hadiyth: ((Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho, basi asimuudhi jirani yake)) [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd na at-Tirmidhiy]

 

 

Na pia Hadiyth: ((Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho, amfanyie wema jirani yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share