040-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Sifa Nne Za Kuchagua Mke Mali, Nasaba, Uzuri Na Dini
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 40
Sifa Nne Za Kuchagua Mke Mali, Nasaba, Uzuri Na Dini
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((تُنْكَحُ الْمَرْأَةُ لأَرْبَعٍ: لِمَالِهَا وَلِحَسَبِهَا وَجَمَالِهَا وَلِدِينِهَا. فَاظْفَرْ بِذَاتِ الدِّينِ تَرِبَتْ يَدَاكَ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mwanamke huolewa kwa sababu nne; Kwa mali yake, nasaba yake [ukoo], uzuri wake na Dini yake. Tafuta mwenye Dini ubakie salama)). [Al-Bukhaariy na Muslim] (yaani usiharibikiwe katika maisha yako).
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Uislamu umetoa mwongozo katika kila jambo hata katika kutafuta mke mwema.
2. Kupata mke mwenye Dini ni sababu ya mume kupata utulivu katika maisha ya ndoa, kwani mke mwenye Dini atafuata shariy’ah za Dini yake na atajitahadharisha kutokutoka nje ya mipaka. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ
Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. [An-Nisaa (4: 34)]
3. Sifa njema nyenginezo za mke mwema mwenye Dini zimetajwa na Allaah (سبحانه وتعالى) katika kauli Yake:
عَسَىٰ رَبُّهُ إِن طَلَّقَكُنَّ أَن يُبْدِلَهُ أَزْوَاجًا خَيْرًا مِّنكُنَّ مُسْلِمَاتٍ مُّؤْمِنَاتٍ قَانِتَاتٍ تَائِبَاتٍ عَابِدَاتٍ سَائِحَاتٍ ثَيِّبَاتٍ وَأَبْكَارًا﴿٥﴾
Akikutalikini, asaa Rabb Wake Akambadilishia wake bora kuliko nyinyi; Waislamu, Waumini, watiifu na wanyenyekevu, wanaotubia, wenye kufanya ‘ibaadah, wanaofunga Swiyaam au wanaohajiri kwa ajili ya Allaah, wajane, na walio bikra. [At-Tahriym: 5]
4. Mke mwenye Dini ni mwenye kumnufaisha mumewe katika kushirikiana kwa kila upande wa maisha yao, ikiwa ni wakati wa furaha na shida, malezi ya watoto, kuhifadhi mali yake, siri yake, nayo ni furaha kamili kwa familia yote.
Hadiyth: ((Je, siwaambii hazina bora aliyonayo mwanamme? Ni mke mwema [mchaji Allaah]; ambapo anapomuangalia, anamfurahisha, na anapomuambia chochote, anamtii na anapokuwa hayupo nyumbani, anatizama [mke] maslahi ya mumewe)). [Abu Daawuwd]
6. Mke mwenye Dini ni sababu mojawapo ya kuidumisha ndoa.
7. Mke mwenye Dini bila shaka atakuwa ni mwenye taqwa na ni sababu mojawapo ya kupata mafanikio ya duniani na Aakhirah.
8. Katika uchaguzi wa mume au mke, Dini inatakiwa ipatiwe kipaumbele.