043-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Wanaopendana Kwa Ajili Ya Allaah Watakuwa Chini Ya Kivuli Chake
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 43
Wanaopendana Kwa Ajili Ya Allaah Watakuwa Chini Ya Kivuli Chake
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِنَّ اللَّهَ يَقُولُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ: أَيْنَ الْمُتَحَابُّونَ بِجَلاَلِي الْيَوْمَ أُظِلُّهُمْ فِي ظِلِّي يَوْمَ لاَ ظِلَّ إِلاَّ ظِلِّي)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Allaah Atasema Siku ya Qiyaamah: Wako wapi wanaopendana kwa Utukufu Wangu? Leo Nitawaweka kivulini katika kivuli Changu, Siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli Changu)). [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Bishara kwa Waumini wanaopendana kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwamba watapata fadhila ya kuwekwa kivulini Siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli cha Allaah (سبحانه وتعالى).
2. Fadhila ya kujumuishwa pamoja katika Ardhw Al-Mahshar (ardhi ya mkusanyiko) Siku ya Qiyaamah, kabla ya kuingia Jannah.
3. Kupenda kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) ni jambo dogo mno kulingana na thawabu na fadhila zake.
4. Hadiyth hii ni tashjiy’ (himizo) kwa Waumini wanaopendana kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) wazidi kutenda mema, waambatane katika kuamrishana mema na kukatazana maovu, na kufanyiana kila aina ya wema. Na fadhila yao ni Rahma ya Allaah (سبحانه وتعالى) juu yao ya kivuli hicho, pamoja na mazuri waliyoandaliwa huko Jannah. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ ۗ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾
Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao, wanaamrisha mema na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote. [At-Tawbah (9: 71)]
Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa ya Maswahaba wao kwa wao na kwa kipenzi chao Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kama Anavyosema Allaah. [Rejea Al-Fat-h (48: 29)].
5. Kuna haja kubwa ya kupendana kwa ajili ya Allaah (سبحانه وتعالى) ili kupata kivuli Chake, kwani jua Siku hiyo litakuwa kali mno si kama jua la duniani, bali litakuwa karibu mno na utosi wa watu.
[Hadiyth:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمْ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لا ظِلَّ إِلا ظِلُّهُ: الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَشَابٌّ نَشَأ فِي عِبَادَةِ رَبِّهِ، وَرَجُلٌ قَلْبُهُ مُعَلَّقٌ فِي الْمَسَاجِدِ، وَرَجُلَانِ تَحَابَّا فِي اللَّهِ اجْتَمَعَا عَلَيْهِ وَتَفَرَّقَا عَلَيْهِ، وَرَجُلٌ طَلَبَتْهُ امْرَأَةٌ ذَاتُ مَنْصِبٍ وَجَمَالٍ فَقَالَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ، وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لا تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ، وَرَجُلٌ ذَكَرَ اللَّهَ خَالِيًا فَفَاضَتْ عَيْنَاهُ)) متفق عليه
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: (i) Imaam (kiongozi) muadilifu. (ii) Kijana ambaye amekulia katika ibaada ya Rabb wake. (iii) Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti (iv) Watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake. (v) Mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: Mimi namkhofu Allaah! (vi) Mtu aliyetoa swadaqa yake akaificha hadi kwamba mkono wake wa kushoto usijue nini ulichotoa mkono wake wa kulia. (vii) Mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]