048-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Haki Ya Allaah Ni Kumwabudu Bila Kumshirikisha Na Kitu
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 48
Haki Ya Allaah Ni Kumwabudu Bila Kumshirikisha Na Kitu
عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ (رضي الله عنه) قَالَ كُنْتُ رِدْفَ النَّبِيّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى حِمَارٍ فَقَالَ: ((يَا مُعَاذُ، تَدْرِي مَا حَقُّ اللَّهِ عَلَى عِبَادِهِ، وَمَا حَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اللَّهِ؟)) قُلْتُ: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ قَالَ: ((فَإِنَّ حَقَّ اللَّهِ عَلَى الْعِبَادِ أَنْ يَعْبُدُوهُ ولاَ يُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا، وَحَقُّ الْعِبَادِ عَلَى اللَّهِ أَنْ لاَ يُعَذِّبَ مَنْ لاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا)) قَقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، أَفلاَ أُبَشِّرُ النَّاسَ؟ قَالَ: ((لاَ تُبَشِّرْهُمْ فَيَتَّكِلُوا)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) amesema: Nilikuwa nyuma ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) nimepanda punda, akasema: ((Ee Mu’aadh! Unajua nini haki ya Allaah juu wa waja Wake na haki ya waja juu ya Allaah?)) Nikajibu: Allaah na Rasuli Wake wanajua zaidi: Akasema:((Haki ya Allaah kwa waja Wake ni kwamba wamwabudu na wasimshirikishe na chochote. Na haki ya waja kwa Allaah ni kwamba Hatomwadhibu yeyote ambaye hamshirikishi na kitu)). Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Nibashirie watu? Akasema: ((Usiwabashirie wasije kuitegemea)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Rahma za Allaah (سبحانه وتعالى) kwa waja kuwaghufuria na kutowaadhibu wanaporudi kutubu Kwake.
2. Haki ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kila mja ni kwamba wasimshirikishe na kitu chochote katika ‘Ibaadah zao. Allaah (سبحانه وتعالى) Amemuamrisha Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) aseme:
قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾
Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Hakika mimi ni mtu kama nyinyi, nafunuliwa Wahy kwamba: Hakika Mwabudiwa wa haki wenu ni Ilaah Mmoja Pekee. Hivyo anayetaraji kukutana na Rabb wake, basi na atende ‘amali njema na wala asishirikishe yeyote katika ‘ibaadah za Rabb wake” [Al-Kahf (18: 110)]
Rejea pia: [An-Nisaa (4: 36), Al-An’aam (6: 151)].
3. Shirki ni miongoni mwa Al-Kabaair (Madhambi makubwa) kwa dalili kadhaa miongoni mwazo ni Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):
(ألاَ أُنبِّئكم بأكبرِ الكبائر؟ الإشراك بالله)) متفق عليه.
((Je, hivi nikujulisheni madhambi makubwa kabisa? Ni kumshirikisha Allaah)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
عَنْ أبي أيوب الأنصاري رضي الله عنه انَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَنْ جَاءَ يَعْبُدُ اللَّهَ وَلاَ يُشْرِكُ بِهِ شَيْئًا وَيُقِيمُ الصَّلاَةَ وَيُؤْتِي الزَّكَاةَ وَيَجْتَنِبُ الْكَبَائِرَ كَانَ لَهُ الْجَنَّةُ)). فَسَأَلُوهُ عَنِ الْكَبَائِرِ فَقَالَ: ((الإِشْرَاكُ بِاللَّهِ وَقَتْلُ النَّفْسِ الْمُسْلِمَةِ وَالْفِرَارُ يَوْمَ الزَّحْفِ)).
Imepokelekewa kutoka kwa Abu Ayyuwb Al-Answaariyy (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Atakayekuja akiwa anamwambudu Allaah wala hamshirikishi na chochote, na anasimamisha Swalaah, na anatoa Zakaah, na anajiepusha na Al-Kabaair (madhambi makubwa) atapata Al-Jannah)) Wakamuuliza kuhusu Al-Kabaair akasema: ((Kumshirkisha Allaah na kumuua Muislamu, na kukimbia (vita) siku ya mapambano (vita).)) [An-Nasaaiy (4009) na ameisahihisha Al-Albaaniy]
[Rejea pia Hadiyth Namba 108] kuhusu madhambi makubwa yanayoangamiza.
4. Allaah (سبحانه وتعالى) Hamghufurii mja anayemshirikisha, lakini Anaghufuria madhambi mengineyo. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾
Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu. [An-Nisaa (4: 48)]
Rejea pia: [An-Nisaa (4: 116)]
5. Kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) kunamharamisha mtu na Jannah na makazi yake ni motoni. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ
Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. [Al-Maaidah (5: 72)].
6. Inafaa kubashiria habari njema ikiwa itasababisha mtu kutenda mema na kumweka mtu katika hali bora zaidi ya iymaan yake na taqwa.
7. Hikma ya njia aliyopendelea sana Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwafunza Maswahaba kwa kuwauliza maswali.
8. Dhihirisho la unyenyekevu wa Maswahaba ulikuwa kwamba hawajibu lolote wasilolijua ili kujionyesha uhodari wao wa kufahamu jambo, bali walimwachia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ajibu mwenyewe yale wasiyokuwa na ujuzi nayo. Hili ni funzo kwa mwanafunzi katika adabu za kutafuta elimu, na anapaswa mwanafunzi kuwa na unyenyekevu wa aina huu.
8. Matahadharisho mengi na makemeo na adhabu kali za kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) zimetajawa katika Qur-aan na Sunnah lakini watu wengi bado wanamshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى)!