073-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kutaja Jina Mlangoni Unapoulizwa “Nani Wewe”

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 73

Kutaja Jina Mlangoni Unapoulizwa “Nani Wewe”

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 عن جَابِرَ (رضي الله عنه) قَال: أَتَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  فَدَقَقْتُ الْبَابَ فَقَالَ:  ((مَنْ ذَا؟)) فَقُلْتُ: أَنَا. فَقَالَ: ((أَنَا أَنَا؟)) كَأَنَّهُ كَرِهَهَا. - متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه) ambaye amesema: “Nilimwendea Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم) nikagonga mlango akauliza: ((Nani huyu?)) Nikajibu: “Mimi”. Akasema: ((Mimi, mimi!?)) kama kwamba alikuwa amechukia.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

 

1. Kubisha hodi mlangoni ni miongoni mwa Akhlaaq (tabia) njema na ni amri kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾

Enyi walioamini! Msiingie nyumba zisizokuwa nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salamu wenyewe. Hivyo ni bora kwenu ili mpate mkakumbuka. [An-Nuwr (24: 27)]

 

Rejea pia An-Nuwr (24: 59)]

 

 

2. Kubisha hodi ni mara tatu, na ikiwa mtu hakujibiwa, basi anapaswa asiingie bali arudi na kwenda zake kwani hivyo ndio heshima na itaepusha kufichuka siri za nyumba, na utakaso zaidi kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ ۖ وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا ۖ هُوَ أَزْكَىٰ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٢٨﴾

Na msipokuta humo yeyote; basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: “Rejeeni!” Basi rejeeni. Huo ni utakaso zaidi kwenu. Na Allaah Mjuzi wa myatendayo. [An-Nuwr (24: 28)]

 

 

3. Ni Sunnah mtu kujitambulisha jina au umaarufu wake anapoulizwa jina lake baada ya kugonga mlango.

 

 

4. Inachukiza kujibu ‘mimi’ au vyovyote vinginevyo bila ya kutaja jina linalokutambulisha.

 

 

5. Kujitambulisha jina inatakiwa pia katika hali nyinginezo kama mtu anapokutana katika kiza cha njiani n.k akaulizwa jina lake.

 

 

6. Mafunzo haya ni sawa na mafunzo katika Hadiyth ya Israa Wal Mi’raaj pindi Jibriyl (عليه السلام) alipotaka idhini ya kuingia katika kila mbingu, alipoulizwa: “Nani?” Akajibu: “Jibriyl.” Akaulizwa: “Nani yuko na wewe?”  Akajibu: “Muhammad.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

7. Mafunzo pia kutoka kwa Maswahaba Abu Dharr na Ummu Haaniy (رضي الله عنهما) katika hali mbalimbali, walipomsalimia Nabiy (صلى الله عليه  وآله وسلم ) akawauliza: ((Nani?)) wakajibu kwa majina yao. [Kila mmoja ametajwa katika Hadiyth ya pekee].

 

 

 

 

 

Share