081-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Adhabu Kali Kwa Anayeficha Elimu

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

 

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 81

 

Adhabu Kali Kwa Anayeficha Elimu

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ سُئِلَ عَنْ عِلْمٍ فَكَتَمَهُ أَلْجَمَهُ اللَّهُ بِلِجَامٍ مِنْ نَارٍ يَوْمَ الْقِيَامَةِ)) رواه أبو داوود و الترمذي وقال: حديث حسن

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Anayeulizwa jambo katika elimu na akaficha, atafungwa lijamu ya moto Siku ya Qiyaamah)). [Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Hatari ya kuficha elimu nayo inatokana na uchoyo wa elimu ambao watu wa kale walioneana wivu kwayo wakakhitilafiana. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 وَآتَيْنَاهُم بَيِّنَاتٍ مِّنَ الْأَمْرِ ۖ فَمَا اخْتَلَفُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۚ

 Na Tukawapa hoja bayana ya mambo (ya Dini). Basi hawakukhitilafiana isipokuwa baada ya kuwajia elimu kwa kufanyiana baghi na uhusuda baina yao [Al-Jaathiyah (45: 17)]

 

Reja pia: Al-Baqarah (2: 159), (174), Aal-‘Imraan (3: 19), Ash-Shuwraa (42: 14).

 

 

 

2. Kuficha elimu ni miongoni mwa dhambi kubwa kwa vile inastahiki adhabu kali kama ilivyotajwa katika Hadiyth na pia laana za Allaah (سبحانه وتعالى) kama Anavyosema (سبحانه وتعالى):

 

إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَـٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّـهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ ﴿١٥٩﴾

Hakika wale wanaoficha yale Tuliyoyateremsha katika hoja bayana na mwongozo baada ya kuwa Tumeyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao Anawalaani Allaah na wanalaaniwa na kila mwenye kulaani.

 

إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا وَأَصْلَحُوا وَبَيَّنُوا فَأُولَـٰئِكَ أَتُوبُ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنَا التَّوَّابُ الرَّحِيمُ ﴿١٦٠﴾ 

Isipokuwa wale waliotubu na wakatengenea na wakabainisha (haki); basi hao Napokea tawbah zao, Na Mimi ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Baqarah (2: 159-160)].

 

 

 

3. Sababu mojawapo ya kumuingiza mtu motoni ni kuficha elimu, hivyo ni wajibu kutahadhari na jambo hili.

 

 

 

4. Ujinga wa kutokuelewa fadhila za kutoa elimu badala ya kuificha, kwani ndio itakayomfaa mtu baada ya kufariki kwake.

Rejea Hadiyth namba (16), (77), (78),  (80).

 

 

5. Kuifunza elimu ni kama kuitolea swadaqah, hivyo Allaah (سبحانه وتعالى) Humzidishia mtu kila anachokitoa kwa ajili Yake. Kinyume chake ni kama kuzuia mali bila ya kuitoa katika Njia ya Allaah.  Hadiyth ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم):

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((مَثَلُ الَّذي يَتعَلَّمُ العِلْمَ ثُمَّ لا يُحَدِّثُ بهِ، كمَثَلِ الَّذي يَكْنِزُ الكَنزَ فلا يُنْفِقُ منهُ)) أخرجه الطبراني في: المعجم الأوسط (689) وصححه الألباني في السلسة الصحيحة (3479)

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mfano wa ambaye anajifunza elimu kisha asiihadithie ni kama mfano wa ambaye anaweka hazina wala asiitoe [fiy sabiliLLaah])) [Atw-Twabaraaniy fiy Mu’jim Al-Awsatw (689), na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3479)]

 

 

6. Ni jambo la kufahamika kuwa kila unapotoa kitu kama elimu vile ndivyo inavyozidi kuongezeka kama vile Swadaqah. Na hivi ndivo shukurani kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuwa ametoa mtu kile Alichomruzuku. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

 Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: “Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (neema Zangu); na mkikufuru, basi hakika adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym 14: 7)]

 

 

  

Share