087-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kusengenya Ni Kumtaja Mtu Kwa Asilolipenda Na Kuzua Ni Kutaja Jambo Asilokuwa Nalo
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 87
Kusengenya Ni Kumtaja Mtu Kwa Asilolipenda
Na Kuzua Ni Kutaja Jambo Asilokuwa Nalo
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْغِيبَةُ؟)) قَالُوا: اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: ((ذِكْرُكَ أَخَاكَ بِمَا يَكْرَهُ)) قِيلَ: أَفَرَأَيْتَ إِنْ كَانَ فِي أَخِي مَا أَقُولُ؟ قَالَ: ((إنْ كَانَ فِيهِ مَا تَقُولُ فَقَدْ اغْتَبْتَهُ وَإِنْ لَمْ يَكُنْ فِيهِ فَقَدْ بَهَتَّهُ)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliuliza: ((Je mnajua maana ya Ghiybah [Kusengenya]?)) Wakasema: Allaah na Rasuli Wake wanajua. Akasema: ((Ni kumtaja ndugu yako kwa jambo analolichukia)). Akaulizwa: Hebu nieleze, iwapo ndugu yangu anayo yale niyasemayo? Akasema: ((Ikiwa analo hilo usemalo basi umeshamsengenya, na ikiwa hana hilo usemalo basi umeshamzushia uongo)). [Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Onyo la kutumia ulimi kwa maovu kama kupeana majina mabaya, kutukanana na ghiybah, Allaah (سبحانه وتعالى) Anaonya haya katika kauli Zake:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِّن قَوْمٍ عَسَىٰ أَن يَكُونُوا خَيْرًا مِّنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِّن نِّسَاءٍ عَسَىٰ أَن يَكُنَّ خَيْرًا مِّنْهُنَّ ۖ وَلَا تَلْمِزُوا أَنفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ ۖ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ﴿١١﴾
Enyi walioamini! Wanaume wasiwafanyie dhihaka na kudharau wanaume wengineo asaa wakawa bora kuliko wao, wala wanawake kwa wanawake wengineo, asaa wakawa bora kuliko wao. Na wala msifedheheshane kwa kutukanana na wala msiitane majina (mabaya) ya utani. Ubaya ulioje kuita jina la ufasiki baada ya iymaan. Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ﴿١٢﴾
Enyi walioamini! Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msifanyiane ujasusi, na wala wasisengenyane baadhi yenu wengineo. Je, anapenda mmoja wenu kwamba ale nyama ya nduguye aliyekufa? Basi mmelichukia hilo! Na mcheni Allaah! Hakika Allaah ni Mwingi wa kupokea tawbah, Mwenye kurehemu. [Al-Hujuraat: 11-12]
Na adhabu zake kali zimetajawa katika Qur-aan na Sunnah. Rejea Al-Humazah (104: 1) Pia rejea Al-Israa (17: 36), An-Nuwr (24: 11-21).
Na rejea pia Hadiyth namba (86), (88), (93), (126).
2. Tofauti ya ghiybah na buhtaan ni kwamba ghiybah ni kumsengenya mtu kwa sifa aliyonayo. Ama buhtaan ni kumsingizia sifa ya uongo. Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى) katika kisa cha ifk alichozuliwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa jambo ambalo hakulifanya:
وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾
Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! (Utakasifu ni Wako) huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!” [An-Nuwr: 16]
Na hivyo ni kuwaudhi Waumini jambo ambalo Allaah (سبحانه وتعالى) Amelikemea kama Anavyosema:
وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ بِغَيْرِ مَا اكْتَسَبُوا فَقَدِ احْتَمَلُوا بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ﴿٥٨﴾
Na wale wanaowaudhi Waumini wa kiume na Waumini wa kike bila ya kuwa wamechuma kosa, basi kwa yakini wamejibebea usingiziaji mkuu wa dhulma na dhambi bayana. [Al-Ahzaab (33: 58)]
2. Kudhihirisha daraja ya maovu ya ulimi, ghiybah na kuzulia, kukashifu n.k.
Rejea kisa cha Ifk katika Al-Bukhaariy na Aayah zake katika Suwrah An-Nuwr (24: 11-20).
3. Kuwazulia Waumini maovu ni miongoni mwa madhambi saba makubwa yanayomuangamiza mtu yaliyotajwa katika Hadiyth namba (108).
Na adhabu yake pia ni kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾
Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui. [An-Nuwr 24: 19)]
4. Ghiybah, buhtaan, kukashifu, kufanya istihzai, kejeli, ni aina ya maradhi ya moyo muovu, nayo ni maradhi makuu katika jamii. Muumin wa kweli hujiweka mbali nayo ili afike Siku ya Qiyaamah akiwa na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa: 88-89].
5. Ghiybah na buhtaan inakula ‘amali njema za mtu Siku ya Qiyaamah, kwani inahusiana na haki za bin Aadam ambazo hazisameheki ila mwenyewe asamehe. Dalili ni Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ؟)) قَالُوا: الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لاَ دِرْهَمَ لَهُ وَلاَ مَتَاعَ . فَقَالَ: ((إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلاَةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ)) مسلم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Je, Mnamjua muflis?)) Wakasema [watu]: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu [pesa] wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”. Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swiyaam, na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao [aliowadhulumu] atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni))]. [Muslim]
Rejea pia Hadiyth namba (19).
Na Hadiyth ifuatayo:
عبد الله بن عمرو أنهم ذكروا عند رسول الله صلى الله عليه وسلم رجلاً فقالوا: لا يأكل حتى يُطعم، ولا يَرحل حتى يُرحل، فقال النبي صلى الله عليه وسلم: ((اغتبتموه)) فقالوا: يا رسول الله: إنما حدثنا بما فيه قال: ((حسبك إذا ذكرت أخاك بما فيه)) المحدث: الألباني - المصدر : السلسلة الصحيحة
Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru (رضي الله عنه) kwamba walimtaja mtu mmoja mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakasema: "Hali hadi alishwe, wala haendi hadi apelekwe." Akasema Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ((Mmemsengenya)). Wakasema: "Ee Rasuli wa Allaah wa Allaah, tumehadithia ya kweli aliyonayo." Akasema: ((Inakutosheleza kumsema ndugu yako kwa aliyonayo)) [Al-Albaaniy katika Silsilatus-Swahiyhah]
6. Uislamu unafunza usalama kati ya jamii na kusisitiza kuheshimiana.
Rejea Hadiyth namba (22), (23), (94), (126).
7. Hikma ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwafunza Maswahaba kwa kuwauliza jambo kwa swali, ambayo inamfanya mtu aelewe haraka jambo. Hii ni mojawapo ya njia nzuri sana ya ufundishaji ambayo inatumiwa leo na waalimu.