090-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Adhabu Kwa Waongopao Ndoto, Kusikiliza Siri Za Watu, Wachoraji Picha Zenye Roho
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 90
Adhabu Kwa Waongopao Ndoto, Kusikiliza Siri Za Watu, Wachoraji Picha Zenye Roho
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((مَنْ تَحَلَّمَ بِحُلْمٍ لَمْ يَرَهُ كُلِّفَ أَنْ يَعْقِدَ بَيْنَ شَعِيرَتَيْنِ وَلَنْ يَفْعَلَ، وَمَنْ اسْتَمَعَ إِلَى حَدِيثِ قَوْمٍ وَهُمْ لَهُ كَارِهُونَ أَوْ يَفِرُّونَ مِنْهُ صُبَّ فِي أُذُنِهِ الأنُكُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، وَمَنْ صَوَّرَ صُورَةً عُذِّبَ وَكُلِّفَ أَنْ يَنْفُخَ فِيهَا وَلَيْسَ بِنَافِخٍ)) البخاري
Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Anayedai kuwa ameona ndoto ambayo hakuiona, atalazimishwa apige fundo kati ya punje mbili za shayiri, wala hatoweza kufanya hivyo. Na anayesikiliza mazungumzo ya watu na ilhali wenyewe wanachukia, au wanamkimbia [mazungumzo yao asiyasikie], atamiminiwa risasi iliyoyeyuka Siku ya Qiyaamah. Na anayechora picha [ya chenye roho], ataadhibiwa na atalazimishwa aivuvie [aitie] roho wala hatoweza kuivuvia)). [Al-Bukhaariy]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Tisho kali la mwenye kuongopea watu kuhusu ndoto, kwani hivyo ni kumzulia uongo Allaah (سبحانه وتعالى) na kuwazulia watu.
2. Adhabu kali kwa anayesikiliza siri za watu, nalo ni miongoni mwa madhambi makubwa.
3. Kusikiliza siri za watu ni miongoni mwa maradhi ya moyo, nayo yanakutokana na kuchunguza mambo ya watu yaliyokatazwa. Allaah (سبحانه وتعالى) Anakataza katika kauli Yake:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا
Enyi walioamini! Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. Na wala msifanyiane ujasusi. [Al-Hujuraat (49: 12)].
4. Kila kiungo cha mwana Aadam kinachotenda maovu, kitakuja kumchongea mtu Siku ya Qiyaamah, yakiwemo masikio kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ﴿٢٠﴾
Mpaka watakapoufikia yatashuhudia dhidi yao, masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.
وَقَالُوا لِجُلُودِهِمْ لِمَ شَهِدتُّمْ عَلَيْنَا ۖ قَالُوا أَنطَقَنَا اللَّـهُ الَّذِي أَنطَقَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُوَ خَلَقَكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ﴿٢١﴾
Na wataziambia ngozi zao: “Mbona mnashuhudia dhidi yetu?” Zitasema: “Ametutamkisha Allaah Ambaye Ametamkisha kila kitu, Naye Ndiye Aliyekuumbeni mara ya kwanza na Kwake mtarejeshwa.
وَمَا كُنتُمْ تَسْتَتِرُونَ أَن يَشْهَدَ عَلَيْكُمْ سَمْعُكُمْ وَلَا أَبْصَارُكُمْ وَلَا جُلُودُكُمْ وَلَـٰكِن ظَنَنتُمْ أَنَّ اللَّـهَ لَا يَعْلَمُ كَثِيرًا مِّمَّا تَعْمَلُونَ﴿٢٢﴾
“Na hamkuwa mkijisitiri hata yasishuhudie masikio yenu, na wala macho yenu, na wala ngozi zenu; lakini mlidhania kwamba Allaah Hajui mengi katika yale mnayoyatenda.
وَذَٰلِكُمْ ظَنُّكُمُ الَّذِي ظَنَنتُم بِرَبِّكُمْ أَرْدَاكُمْ فَأَصْبَحْتُم مِّنَ الْخَاسِرِينَ﴿٢٣﴾
“Na hivyo dhana yenu mliyokuwa mkimdhania Rabb wenu, imekuangamizeni, mmekuwa miongoni mwa waliokhasirika.” [Fusw-swilat (41: 20-23)].
Na Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَقْفُ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ ۚ إِنَّ السَّمْعَ وَالْبَصَرَ وَالْفُؤَادَ كُلُّ أُولَـٰئِكَ كَانَ عَنْهُ مَسْئُولًا ﴿٣٦﴾
Na wala usifuatilie ambayo usiyokuwa nayo ujuzi. Hakika masikio na macho na moyo; vyote hivyo vitakuwa vya kuulizwa (Siku ya Qiyaamah). [Al-Israa (17: 36)]
5. Tisho kali kwa mwenye kuchora picha yenye roho, kwani wanamwiga Muumba kuhusu Uwezo Wake ambao hakuna Awezaye kuumba chochote isipokuwa Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) na kwamba ni watu watakaopata adhabu kali kabisa.
Hadiyth kadhaa zimetahadharisha adhabu zake, miongoni mwazo ni:
عَنْ عَائِشَةَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم) قَال: ((أَشَدُّ النَّاسِ عَذَابًا يَوْمَ القِيَامَةِ الَّذِينَ يُضَاهِئُونَ بِخَلْقِ اللَّهِ))
Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللهُ عَنْهَا) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watakaokuwa na adhabu kali Siku ya Qiyaamah ni wanaomuiga Allaah katika uumbaji Wake)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na pia:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ (رضي الله عنهما) : سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((كُلُّ مُصَوِّرٍ فِي النَّارِ يُجْعَلُ لَهُ بِكُلِّ صُورَةٍ صَوَّرَهَا نَفْسٌ يُعَذَّبُ بِهَا فِي جَهَنَّمَ))
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما): Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Kila mchoraji picha atakuwa motoni. Kila picha aliyoichora, itatiwa roho nayo itamuadhibu katika Jahannam)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Na pia:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((قَالَ اللهُ تَعَالَى: وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنْ ذَهَبَ يَخْلُقُ كَخَلْقِي؛ فَلْيَخْلُقُوا ذَرَّةً، أَوْ لِيَخْلُقُوا حَبَّةً، أَوْ لِيَخْلُقُوا شَعِيْرَةً )) أَخْرَجَاهُ
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Allaah Aliyetukuka Amesema: Nani dhalimu zaidi kuliko anayejaribu kuumba kama kuumba Kwangu? Basi na waumbe chembe moja au waumbe punje ya nafaka, au waumbe chembe ya shayiri)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
6. Kila ‘amali ovu au nzuri ina malipo yake tofauti.
7. Mifano ya Allaah (سبحانه وتعالى) kuhusu kutisha jambo lisilowezekana kutendwa au kutendeka kama kupiga fundo kati ya punje mbili za shayiri, na Allaah (سبحانه وتعالى) Anatoa mifano kama hiyo katika kauli Zake:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ ۚ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ ۖ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ۚ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ ﴿٧٣﴾
Enyi watu! Imepigwa mfano basi isikilizeni kwa makini! Hakika wale mnaowaomba badala ya Allaah hawawezi kuumba nzi japo wakijumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu chochote kile hawawezi kukiambua tena. Amedhoofika mwenye kutaka matilabu na mwenye kutakiwa. [Al-Hajj (22: 73)].
Na pia mfano wa ambaye anamkanusha Allaah (سبحانه وتعالى) na Aayat Zake:
إِنَّ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَاسْتَكْبَرُوا عَنْهَا لَا تُفَتَّحُ لَهُمْ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَلَا يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ حَتَّىٰ يَلِجَ الْجَمَلُ فِي سَمِّ الْخِيَاطِ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُجْرِمِينَ ﴿٤٠﴾
Hakika wale waliokadhibisha Aayaat Zetu na wakazifanyia kiburi, hawatofunguliwa milango ya mbingu na wala hawatoingia Jannah mpaka ngamia aingie katika tundu ya sindano. Na hivyo ndivyo Tunavyowalipa wakhalifu. [Al-A’raaf (7: 40)].