100-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayedhihirisha Furaha Kwa Msiba Wa Mwenziwe Huenda Akaonjeshwa Yeye Msiba
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 100
Anayedhihirisha Furaha Kwa Msiba Wa Mwenziwe Huenda Akaonjeshwa Yeye Msiba
عَنْ وَاثِلَةَ بْنِ الأسْقَعِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لاَ تُظْهِرْ الشَّمَاتَةَ لإَخِيكَ فَيَرْحَمَهُ اللَّهُ وَيَبْتَلِيكَ)) رواه الترمذي وَقَالَ هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ
Imepokelewa kutoka kwa Waathilah bin Al-Asqa’i (رضي الله عنه) amesema: “Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Usidhihirishe furaha kwa msiba alioupata nduguyo, Asije Allaah Akamrehemu na Akakuonjesha wewe)). [At-Tirmidhiy na amesema Hadiyth Hasan]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Makatazo ya kufurahia msiba wa mwenzio, kwani Waislamu wote ni ndugu na inawapasa kuoneana huruma na kupendeleana kheri.
Rejea Al-Hujuraat (49: 10), Al-Fat-h (48: 29).
2. Muislamu aumie anapoumia nduguye na afurahi anapofurahi nduguye.
Rejea Hadiyth namba (20), (21).
Pia Hadiyth:
عن النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَثَلُ الْمُؤْمِنِينَ فِي تَوَادِّهِمْ وَتَرَاحُمِهِمْ وَتَعَاطُفِهِمْ مَثَلُ الْجَسَدِ؛ إِذَا اشْتَكَى مِنْهُ عُضْوٌ تَدَاعَى لَهُ سَائِرُ الْجَسَدِ بِالسَّهَرِ وَالْحُمَّى))
Kutoka kwa Nu’maan bin Bashiyr kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mfano wa Waumini katika kupendana na kurehemeana kwao na kuhurumiana kwao ni sawa na mwili mmoja, kikishtakia kiungo kimoja, basi mwili mzima utakosa usingizi na kushikwa na homa)). [Al-Bukhaariy]
3. Hali ya furaha na misiba, shida na faraja, umaskini na utajiri n.k. huzunguka baina ya watu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِن يَمْسَسْكُمْ قَرْحٌ فَقَدْ مَسَّ الْقَوْمَ قَرْحٌ مِّثْلُهُ ۚ وَتِلْكَ الْأَيَّامُ نُدَاوِلُهَا بَيْنَ النَّاسِ
Inapokuguseni majeraha basi yamekwisha wagusa watu majeraha kama hayo. Na hizo ni siku Tunazizungusha zamu (za mabadiliko ya hali) baina ya watu [Aal-‘Imraan: 140]
4. Tahadharisho katika Hadiyth hiyo kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) kumjaalia anayefurahia msiba wa mwenziwe umfikie naye apate kuonja dhiki yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تَهِنُوا فِي ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ ۖ إِن تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ ۖ وَتَرْجُونَ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا يَرْجُونَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٠٤﴾
Wala msilegee kuwaandama watu (maadui). Mkiwa mnaumia basi nao pia wanaumia kama mnavyoumia. Na mnataraji kutoka kwa Allaah wasiyoyataraji wao. Na Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [An-Nisaa (4: 104)]