104-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Kunong’ona Mbele Ya Wengineo Husababisha Maudhi Na Dhana Mbaya
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 104
Kunong’ona Mbele Ya Wengineo Husababisha Maudhi Na Dhana Mbaya
عَنْ ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) أنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَال: ((إِذَا كُنْتُمْ ثلاَثَةً فلاَ يَتَنَاجَى اثْنَانِ دُونَ الآخَرِ حَتَّى تَخْتَلِطُوا بِالنَّاسِ مِنْ أَجْلِ أَنْ يُحْزِنَهُ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Mas’uwd (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Mnapokuwa watatu, basi wawili wasinong’onezane bila kumshirikisha mwengine hadi wajiunge watu wengine [kumtoa katika upweke yule aliyeachwa katika mazungumzo] na watu, kwa sababu kufanya hivyo kutamhuzunisha [yule wa tatu])). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Makatazo ya kunong’onezana wawili anapokuweko mtu wa tatu ili asiudhike na kuhisi vibaya.
2. Kunong’onezana mbele ya wengineo huenda kukasababisha kutia shaka au dhana mbaya kwa ambaye hakushirikishwa katika mnong’ono.
3. Makatazo ya kunong’onezana pasi na kuwashirikisha wengineo hata ikiwa ni zaidi ya idadi iliyotajwa na hata kwa jambo la kheri haipasi. Na kwa jambo la shari Amekataza Allaah (سبحانه وتعالى).
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا تَنَاجَيْتُمْ فَلَا تَتَنَاجَوْا بِالْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَمَعْصِيَتِ الرَّسُولِ وَتَنَاجَوْا بِالْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ الَّذِي إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴿٩﴾
Enyi walioamini! Mnaponong’onezana, basi msinong’onezane kuhusu dhambi na uadui na kumuasi Rasuli, bali nong’onezaneni kuhusu wema na taqwa; na mcheni Allaah Ambaye Kwake Pekee mtakusanywa.
إِنَّمَا النَّجْوَىٰ مِنَ الشَّيْطَانِ لِيَحْزُنَ الَّذِينَ آمَنُوا وَلَيْسَ بِضَارِّهِمْ شَيْئًا إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۚ وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ﴿١٠﴾
Hakika mnong’ono unatokana na shaytwaan ili awahuzunishe wale walioamini, na wala hawezi kuwadhuru chochote isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Na kwa Allaah watawakali Waumini. [Al-Mujaadalah: 9-10]
Rejea pia: Al-Maaidah (5: 2)
4. Uislamu unapendelea amani baina ya ndugu na kufunza adabu njema na njia za kuepusha kila aina ya maudhi au maovu ya nafsi.
5. Kutokunong’onezana ni katika adabu za kikao baina ya Waislamu.
6. Athari ya hivyo ni mbaya, kwani dhana hiyo mbaya inaweza kuzaa uadui na chuki.