108-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Madhambi Saba Yanayoangamiza

 

Lu-ulu-un-Manthuwrun

(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)

 

Hadiyth Ya 108

Madhambi Saba Yanayoangamiza

 

Alhidaaya.com

 

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه عن النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((اجْتَنِبُوا السَّبْعَ الْمُوبِقَاتِ)) قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا هُنَّ؟  قَالَ: ((الشِّرْكُ بِاللَّهِ وَالسِّحْرُ وَقَتْلُ النَّفْسِ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلاَّ بِالْحَقِّ وَأَكْلُ الرِّبَا وَأَكْلُ مَالِ الْيَتِيمِ وَالتَّوَلِّي يَوْمَ الزَّحْفِ وَقَذْفُ الْمُحْصَنَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ الْغَافلاَتِ)) متفق عليه

 

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه)  kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:((Jiepusheni na mambo saba yanayoangamiza!)) Wakauliza: Ni yepi hayo ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni kumshirikisha Allaah, sihri [uchawi], kuua nafsi Aliyoiharamisha Allaah isipokuwa kwa haki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kukimbia wakati wa kupambana na adui na kuwatuhumu uzinifu wanawake Waumini waliohifadhika walioghafilika)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

 

Mafunzo Na Mwongozo:

 

 

1. Imaam An-Nawawiy amesema: “Hadiyth hii ni dalili kwamba maasi na dhambi kubwa kabisa ni kumshirikisha Allaah.

 

 

2. Shirki ni dhambi isiyosamehewa ikiwa hatotubia mtu kabla ya kufariki kwake kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):

 إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ 

 Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae [An-Nisaa (4: 48, 116)]

 

 

3. Na anayemshirikisha Allaah hatoingia Peponi kama Anavyoonya Allaah (سبحانه وتعالى):

  إِنَّهُ مَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ حَرَّمَ اللَّـهُ عَلَيْهِ الْجَنَّةَ وَمَأْوَاهُ النَّارُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ﴿٧٢﴾

  Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni motoni. Na madhalimu hawatopata yeyote mwenye kunusuru. [Al-Maaidah (5: 72)]

 

Bali kutomshirikisha ni ufunguo wa Jannah kutokana na Hadiyth: ((Atakayefariki akiwa hakumshirikisha kitu Allaah Ta’aalaa, Ataingia Peponi)). [Muslim]

 

Rejea pia Hadiyth namba (11), (48), (95).

 

 

4. Kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) ni dhulma kubwa kabisa, kwani Yeye ni Muumba wa kila kitu.

 

Rejea:  Luqmaan (31: 13), Al-An’aam (6: 82).

 

 

5. Aayah na Hadiyth nyingi zimetaja ubaya wa kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى).

 

Rejea Hadiyth namba (119), (131), (136).

 

 

6. Haramisho la kuua mtu bila ya haki.

 

Rejea Al-An’aam (6: 151), An-Nisaa (4: 92-93), Al-Furqaan (25: 68), Al-Israa (17:33).

 

 

7. Haramisho la kula ribaa. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 الَّذِينَ يَأْكُلُونَ الرِّبَا لَا يَقُومُونَ إِلَّا كَمَا يَقُومُ الَّذِي يَتَخَبَّطُهُ الشَّيْطَانُ مِنَ الْمَسِّ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا إِنَّمَا الْبَيْعُ مِثْلُ الرِّبَا ۗ وَأَحَلَّ اللَّـهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا ۚ فَمَن جَاءَهُ مَوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّهِ فَانتَهَىٰ فَلَهُ مَا سَلَفَ وَأَمْرُهُ إِلَى اللَّـهِ ۖ وَمَنْ عَادَ فَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٧٥﴾

Wale wanaokula ribaa hawatosimama (Siku ya Qiyaamah) ila kama anavyosimama yule aliyezugwa na shaytwaan kwa kuguswa na kupatwa. Hivyo kwa sababu wao wamesema: “Hakika biashara ni kama ribaa.” Na Allaah Amehalalisha biashara na Ameharamisha ribaa. Basi atakayefikiwa na mawaidha kutoka kwa Rabb wake akakoma; basi ni yake yale yaliyopita, na hukumu yake iko kwa Allaah. Na atakayerudia basi hao ni watu wa motoni, wao humo ni wenye kudumu.

يَمْحَقُ اللَّـهُ الرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ كَفَّارٍ أَثِيمٍ ﴿٢٧٦﴾

Allaah Huifuta baraka (mali ya) ribaa na Huzibariki swadaqah. Na Allaah Hapendi kila kafiri apapiae madhambi. [Al-Baqarah: (275-276)]

 

 Na Aayah zinaendelea hadi namba (279).

 

Rejea pia: Aal-‘Imraan (3: 130) na Hadiyth nyingi zimeharamisha ribaa.

 

Rejea pia Hadiyth namba (109).

   

 

 

8. Haramisho ya kula mali ya yatima. Rejea: Al-An’aam (6: 152), Al-Israa (17: 34), An-Nisaa (4: 2)]. Na pia Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

  إِنَّ الَّذِينَ يَأْكُلُونَ أَمْوَالَ الْيَتَامَىٰ ظُلْمًا إِنَّمَا يَأْكُلُونَ فِي بُطُونِهِمْ نَارًا ۖ وَسَيَصْلَوْنَ سَعِيرًا ﴿١٠﴾

Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma hapana shaka kwamba wanakula katika matumbo yao moto, na watauingia moto uliowashwa vikali mno.  [An-Nisaa (4: 10)]

 

 

9. Aayah nyingi na Hadiyth zimesisitiza kuhusu kuwatendea wema mayatima na fadhila za kulea.

 

Rejea: Al-Baqarah (2: 83,  177,  215, 220),  An-Nisaa (4: 6,  36), Al-Anfaal (8: 41), Al-Hashr (59: 7), Al-Fajr (89: 17), Adhw-Dhwuhaa (93: 9).

 

 

10. Haramisho la kukimbia vita. Rejea Al-Anfaal (8: 15-16).

 

 

11. Haramisho la kuwatuhumu wanawake wema na adhabu yake. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى): 

 إِنَّ الَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ الْغَافِلَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ لُعِنُوا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٢٣﴾

Hakika wale wanaowasingizia machafu wanawake watwaharifu, walioghafilika, Waumini; wamelaaniwa duniani na Aakhirah na watapata adhabu kuu.

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [An-Nuwr (24: 23-24)]

 

Rejea pia An-Nuwr (24: 4, 19)  

 

 

12.  Uislamu umemdhihirishia bin Aadam mambo ya kheri na maovu yatakayomuangamiza.

 

 

13. Mambo haya mpaka katika mambo yanayoangamiza ni kuwa yanavunja mahusiano baina ya mja na Muumba Wake na baina ya waja wao kwa wao.

 

 

14. Uislamu umekuja kujenga uhusiano mwema baina ya wana Aadam ili watu wakae kwa kuheshimiana baina yao. Mambo haya (yaliyotajwa) yanapofanyika, yanaharibu uhusiano mwema na kuvunja jamii.

 

 

 

Share