110-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Anayejionyesha Kwa Watu (Riyaa) Allaah Atamfedhehesha Siku Ya Qiyaamah
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 110
Anayejionyesha Kwa Watu (Riyaa) Allaah Atamfedhehesha Siku Ya Qiyaamah
عَنْ جُنْدَبِ بْنِ عَبْدُ الله بْنِ سُفْيانَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ سَمَّعَ سَمَّعَ اللَّهُ بِهِ وَمَنْ رَاءَى رَاءَى اللَّهُ بِهِ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Jundab bin ‘Abdillaah bin Sufyaan (رضي الله عنه) amesema: “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
“Mwenye kuzungumza (au kusoma) ili watu wamsifu, Allaah Atamfedhehesha Siku ya Qiyaamah, na mwenye kuwafanyia watu riyaa (kwa amali njema ili aonekane ni mtukufu), Allaah Atazidhihirisha siri zake (Siku ya Qiyaamah).” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Al-Bukhaariy na Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Riyaa ni shirki ya kujificha.
2. Tahadharisho la riyaa na kujitukuza kwa jambo Alilolikataza Allaah (سبحانه وتعالى) [An-Najm: 32].
3. Makatazo ya kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika ‘amali. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
فَوَيْلٌ لِّلْمُصَلِّينَ ﴿٤﴾
Basi Ole kwa wanaoswali ...
الَّذِينَ هُمْ عَن صَلَاتِهِمْ سَاهُونَ ﴿٥﴾
Ambao wanapuuza Swalaah zao.
الَّذِينَ هُمْ يُرَاءُونَ ﴿٦﴾
Ambao wanajionyesha (riyaa). [Al-Maa’uwn: 4-6]
Reja pia: Al-Kahf (18: 110), Al-Baqarah (2: 264), An-Nisaa (4: 38, 142).
4. Riyaa inabatilisha ‘amali za Muislamu, huenda mtu akafanya juhudi na kupoteza muda, zikawa hazina thamani. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾
Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan 25: 23)]
Rejea pia Al-Kahf (18: 103-104).
5. ‘Amali za kwanza kuhukumiwa Siku ya Qiyaamah ni zile ambazo zitamdhihirisha mtu ikhlaasw yake.
Hadiyth: “Watu watatu watakuwa wa mwanzo kuhukumiwa Siku ya Qiyaamah; Aliyekufa shahidi, aliyejifunza elimu na Qur-aan akaifunza, aliyetoa mali yake. Wote wataingizwa motoni kwa kuwa wametenda kwa ajili ya kuonyesha watu.” [Muslim, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy]
6. Hapana budi kuwa na ikhlaasw katika kila ‘amali anayoitenda Muislamu kwa ajili ya kuzitafuta radhi za Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee.
7. Muhimu kusoma Du’aa ya Sunnah ili kujikinga na riyaa:
اللّهُـمَّ إِنّـي أَعـوذُبِكَ أَنْ أُشْـرِكَ بِكَ وَأَنا أَعْـلَمْ، وَأَسْتَـغْفِرُكَ لِما لا أَعْـلَم
Allaahumma inniy a’uwdhu Bika an ushrika Bika waanaa a’-alamu wa astaghfiruka limaa laa a’-lam
Ee Allaah hakika mimi Najikinga Kwako kutokana na kukushirikisha hali ya kuwa najua na ninakuomba maghfira na nisiyoyajua
Ni Hadiyth ya Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (رضي الله عنه), Kauli ya Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم)
خَطَبَنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ذَاتَ يَوْمٍ فَقَالَ: ((أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا هَذَا الشِّرْكَ فَإِنَّهُ أَخْفَى مِنْ دَبِيبِ النَّمْلِ)) فَقَالَ لَهُ مَنْ شَاءَ اللَّهُ أَنْ يَقُولَ: "وَكَيْفَ نَتَّقِيهِ وَهُوَ أَخْفَى مِنْ دَبِيبِ النَّمْلِ يَا رَسُولَ اللَّهِ؟" قَالَ: قُولُوا: ((اللَّهُمَّ إِنَّا نَعُوذُ بِكَ مِنْ أَنْ نُشْرِكَ بِكَ شَيْئًا نَعْلَمُهُ وَنَسْتَغْفِرُكَ لِمَا لَا نَعْلَمُ))
“Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) alituhutubia akasema: ((Enyi watu! Iogopeni shirki hii kwani imefichika zaidi kuliko kutambaa kwa sisimizi)) Akasema mmoja wa aliyejaaliwa na Allaah aseme: “Je vipi tujiokoe nayo na hali imefichika zaidi kuliko kutambaa kwa sisimizi ee Rasuli wa Allaah?”. Akasema: ((Semeni: Ee Allaah! Hakika sisi tunajikinga Kwako kutokana na kukushirikisha hali ya kuwa tunajua na tuinakuomba maghfira kwa tusiyoyajua)) - Ahmad (4/403), na wengineo na angalia: Swahiyh Al-Jaami’ (3/233) [3731] na Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb ya Al-Albaaniy (رحمه الله) (1/122) [36].
8. Muumin anayejitahidi kufanya ‘amali kwa ikhlaasw asimwache shaytwaan kumtia wasiwasi kuwa anafanya kwa riyaa akaogopa kutenda mema yake.
Hadiyth: Abuu Dharr (رضي الله عنه) alimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): ‘‘Ee Rasuli wa Allaah! Je, unaonaje kama mtu anafanya matendo mazuri, kisha watu wakamsifia kwa matendo yake? Akajibu: ((Hiyo ni sehemu ya baraka na radhi kwa Muumin [zitakazohifadhiwa kwake siku ya Qiyaamah])). [Muslim]