125-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Miongoni Mwa Madhambi Makubwa Ni Kumshirikisha Allaah, Kuwaasi Wazazi, Kuua Mtu, Kuapa Uongo
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 125
Miongoni Mwa Madhambi Makubwa Ni Kumshirikisha Allaah,
Kuwaasi Wazazi, Kuua Mtu, Kuapa Uongo
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو بْن الْعاص (رضي الله عنهما) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ َقَالَ: ((الْكَبَائِرُ الإِشْرَاكُ بِاللَّهِ، وَعُقُوقُ الْوَالِدَيْنِ، وَقَتْلُ النَّفْسِ، وَالْيَمِينُ الْغَمُوسُ)) البخاري وفي رواية لَهُ: أنَّ أَعْرَابِياً جَاءَ إِلَى النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: يَا رَسُولَ اللَّه، مَا الْكَبَائِر؟ ُ قَالَ: ((الإشْرَاكُ بِاللَّهِ)) قَالَ: ثُمَّ مَاذَا؟ قَالَ: ((الْيَمِينُ الْغَمُوسُ)) قُلْتُ: وَمَا الْيَمِينُ الْغَمُوسُ؟ قَالَ: ((الَّذِي يَقْتَطِعُ مَالَ امْرِئٍ مُسْلِمٍ!)) يَعْنِ: بِيَمِينٍ هُوَ فِيهَا كَاذِب
Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amri bin Al-‘Aasw (رضي الله عنهما) amesema kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Madhambi makubwa ni kumshirikisha Allaah, kuwaasi wazazi wawili, kuua nafsi na yamini [kiapo] ya uongo)). [Al-Bukhaariy] Na katika riwaayah nyingine: “Alikuja Mbedui mmoja kwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah? Ni yepi madhambi makubwa? Akasema: ((Kumshirikisha Allaah)) Akasema: Kisha yepi? Akasema: ((Yamini ya uongo)). Nikauliza: Ni ipi yamini ya uongo? Akasema: ((Ni ambayo mtu hujichukulia mali ya Muislamu!)) yaani akaapa kwa uongo. [Al-Bukhaariy]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Uharamisho wa kuapa uongo na zaidi inapokuwa ni kwa ajili ya kula mali za watu bila haki na kwa ubatilifu, ikiwa ni kwa ribaa au kwa dhulma ya aina yoyote. Allaah (سبحانه وتعالى) Anatahadharisha:
وَلَا تَأْكُلُوا أَمْوَالَكُم بَيْنَكُم بِالْبَاطِلِ وَتُدْلُوا بِهَا إِلَى الْحُكَّامِ لِتَأْكُلُوا فَرِيقًا مِّنْ أَمْوَالِ النَّاسِ بِالْإِثْمِ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١٨٨﴾
Na wala msiliane mali zenu kwa ubatilifu na mkazipeleka (rushwa) kwa mahakimu ili mle sehemu katika mali ya watu kwa dhambi na hali mnajua. [Al-Baqarah (2: 188)]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):
وَأَخْذِهِمُ الرِّبَا وَقَدْ نُهُوا عَنْهُ وَأَكْلِهِمْ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ ۚ وَأَعْتَدْنَا لِلْكَافِرِينَ مِنْهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٦١﴾
Na kuchukua kwao ribaa na hali walikatazwa kuichukua; na kula kwao mali za watu kwa ubatilifu. Na Tumeandalia kwa makafiri miongoni mwao adhabu iumizayo. [An-Nisaa (4: 161).
Rejea pia An-Nisaa (4: 29).
2. Kiapo cha uongo ni miongoni mwa madhambi makubwa yanayostahiki adhabu kali kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى).
3. Kiapo cha uongo kimesawazishwa kuwa sawa na kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى) na kuua mtu, na kuasi wazazi, kwani yote ni dhulma zinazohusiana na haki za watu.
Rejea Hadiyth namba (19).
4. Aina ya viapo ni vitatu;
(i) Al-Yamiyn Al-Ghamuws (Kiapo cha uongo):
Ni kula kiapo huku anakusudia kuongopa, kama vile kusema: “Wa-Allaahi nimenunua kitu kadhaa kwa shilingi laki moja”, naye hakukinunua hivyo. Hukmu yake: Atimize kafara kama ilivyotajwa katika Al-Maaidah (5: 89). Lakini kafara pekee katika kiapo hiki haitotosha, bali pamoja na kafara, mhusika anatakiwa alete tawbah na kuomba maghfirah (msamaha), kwani kosa hili ni kubwa sana, na hasa ikiwa yamini hiyo itamfikisha kwenye kumega haki ya mtu mwengine kwa njia isiyo ya halaal. Hii ndio kauli ya jamhuri (Wanachuoni wengi).
(ii) Al-Yamiyn Al-Laghw (Kiapo cha upuuzi):
Ni kile kipitayo ulimini mwa Muislamu bila kuikusudia, kama yule ambaye katika mazungumzo yake hujitokeza kwa wingi mno wa neno: “Wa-Allaahi hapana”. Hukmu yake ni: ((Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi)) kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Al-Maaidah (5: 89).
(iii) Al-Yamiyn Al-Mun’aqidah (Kiapo cha kufungika):
Ni kukusudia jambo la baadaye. Kama vile Muislamu kusema: “Wa-Allaahi nitalifanya jambo kadhaa” Au “Wa-Allaahi sitolifanya…” kisha akafanya kinyume chake. Hukmu yake: ((….lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti)) kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى) katika Al-Maaidah (5: 89).
5. Haya ni tahadhari kwetu tusiingie katika madhambi hayo makubwa ambayo yanaangamiza kama yalivyotajwa hapa shirki, kuwaasi wazazi, kuua pasi na haki na pia yamini ya uongo.
6. Haramisho la kumshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى). Rejea Hadiyth namba (48), (108), (119).
7. Haramisho la kuwaasi wazazi. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾
Na Rabb wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima.
وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾
Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: “Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni.” [Al-Israa (17: 23-24)]
Na baadhi ya Hadiyth za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu kuwaasi wazazi:
عَنْ أَنَس وَغَيْره أَنَّ النَّبِيّ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ لَمَّا صَعِدَ الْمِنْبَر ثُمَّ قَالَ (( آمِينَ آمِينَ آمِينَ)) " قِيلَ يَا رَسُول اللَّه عَلَامَ مَا أَمَّنْت ؟ قَالَ (( أَتَانِي جِبْرِيل فَقَالَ يَا مُحَمَّد رَغِمَ أَنْف رَجُل ذُكِرْت عِنْده فَلَمْ يُصَلِّ عَلَيْك قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل دَخَلَ عَلَيْهِ شَهْر رَمَضَان ثُمَّ خَرَجَ فَلَمْ يُغْفَر لَهُ قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِينَ ثُمَّ قَالَ رَغِمَ أَنْف رَجُل أَدْرَكَ وَالِدَيْهِ أَوْ أَحَدهمَا فَلَمْ يُدْخِلَاهُ الْجَنَّة قُلْ آمِينَ فَقُلْت آمِين)) صحيح الترمذي و قال الشيخ الأباني حسن صحيح
Imepokelewa kutoka kwa Anas na wengineo kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipopanda juu ya minbar aliitikia ((Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn)). Alipoulizwa kwa nini ameitikia hivyo akasema: ((Amenijia Jibriyl akasema: “Ee Muhammad, ole wake yule ambaye unapotajwa hakuswalii, hivyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye umeingia mwezi wa Ramadhwaan kisha akatoka bila ya kughufuriwa, kwa hiyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn. Kisha akasema: “Ole wake yule ambaye amewakuta wazazi wake au mmoja wa wazazi wake lakini wasimuingize Jannah. Hivyo sema Aamiyn”. Nikasema Aamiyn)) [Swahiyh At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa Hadiyth hiyo ina daraja ya Hasan Swahiyh]
Kuwatii wazazi na kutokuwaasi ni katika haki zao kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) katika Hadiyth:
Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Mtoto hawezi kumlipa babake (kwa yale aliyomfanyia) isipokuwa anapomkuta kuwa ni mtumwa, akamnunua kisha kumwacha huru.” [Muslim, Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy].
Rejea Hadiyth namba (34),
8. Haramisho la kuua mtu bila ya haki. Allaah (سبحانه وتعالى) Ametaja katika Aayah kadhaa zikiwemo:
وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ أَن يَقْتُلَ مُؤْمِنًا إِلَّا خَطَأً ۚ وَمَن قَتَلَ مُؤْمِنًا خَطَأً فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ وَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰ أَهْلِهِ إِلَّا أَن يَصَّدَّقُوا ۚ فَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ عَدُوٍّ لَّكُمْ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ وَإِن كَانَ مِن قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ فَدِيَةٌ مُّسَلَّمَةٌ إِلَىٰ أَهْلِهِ وَتَحْرِيرُ رَقَبَةٍ مُّؤْمِنَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ شَهْرَيْنِ مُتَتَابِعَيْنِ تَوْبَةً مِّنَ اللَّـهِ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿٩٢﴾
Na haiwi kwa Muumin amuue Muumin ila kwa kukosea tu. Na atakayemuua Muumin kwa kukosea basi aachilie huru mtumwa Muumin na atoe diya kwa kuifikisha kwa ahli zake, isipokuwa watolee wenyewe swadaqah. Na ikiwa ni miongoni mwa watu wa maadui zenu naye ni Muumin, basi (aliyeua) aachilie huru mtumwa Muumin. Na ikiwa ni miongoni mwa watu ambao kuna mkataba baina yenu na baina yao; basi wapewe diya kuifikisha kwa ahli wake na aachiliwe huru mtumwa Muumin. Asiyepata, afunge Swiyaam miezi miwili mfululizo; kuwa ni tawbah kwa Allaah. Na Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.
وَمَن يَقْتُلْ مُؤْمِنًا مُّتَعَمِّدًا فَجَزَاؤُهُ جَهَنَّمُ خَالِدًا فِيهَا وَغَضِبَ اللَّـهُ عَلَيْهِ وَلَعَنَهُ وَأَعَدَّ لَهُ عَذَابًا عَظِيمًا ﴿٩٣﴾
Na atakayemuua Muumini kwa kusudi, basi jazaa yake ni Jahannam, ni mwenye kudumu humo na Allaah Atamghadhibikia na Atamlaani na Atamuandalia adhabu kuu. [An-Nisaa (4: 92-93)]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾
Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu. [Al-Furqaan (25: 68)]
Rejea pia Hadiyth namba (108), (132).