134-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Makatazo Ya Kujishabihisha Na Makafiri
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 134
Makatazo Ya Kujishabihisha Na Makafiri
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) أنَّ رَسُول اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قال: ((إنَّ اليَهُودَ وَالنَّصَارى لاَ يَصْبغُونَ، فَخَالِفُوهُمْ)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hakika Mayahudi na Manaswara hawapaki rangi, wakhalifuni)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Maana yake: Ni kupaka rangi mvi za ndevu na mvi za nywele kichwani kwa rangi manjano au nyekundu. Ama kupaka rangi nyeusi, imekatazwa kama ilivyothibiti dalili yake katika Hadiyth iliyopokelewa na Muslim
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Pendekezo la kupaka rangi ili kuficha mvi kwa rangi ya manjano au nyekundu. Kutumia hinna ni bora zaidi, kwani ni Sunnah ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم). Juu ya hivyo, ni mada asili na kawaida na haileti madhara.
2. Makatazo ya kupaka rangi nyeusi ni kwa wanaume na wanawake, kwani hiyo inakuwa ni ghushi.
3. Kujiepusha kujifananisha na makafiri katika matendo yao kama mavazi yao, na kujipamba kwao.
Rejea Hadiyth namba (113), (115), (116).
4. Makatazo ya kujifananisha na makafiri katika kila jambo, na hivyo pia ni kutokufuata mila zao ambazo zimekuwa ni kigezo kwa Waislamu wengi wasiojua uovu wake au ambao bado hawataki kuacha maovu hayo. Mfano kusherehekea au kukubali mialiko ya sikukuu zao kama Krismasi, Mwaka mpya wa Kikristo na wa Hijri (wa Kiislamu), Pasaka, kusherehekea Siku ya Wajinga (April Fool), Siku ya mama (Mother’s day), Siku ya wapendanao (Valentine), Siku ya kuzaliwa (Birthday), n.k.
5. Kujifananisha na makafiri katika sherehe zao ni miongoni mwa madhambi makubwa, kwani humo wanamshirikisha Allaah (سبحانه وتعالى). Na Allaah (سبحانه وتعالى) Ameonya kufuata au kutaka mila yaani Dini zao. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَن تَرْضَىٰ عَنكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَىٰ حَتَّىٰ تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ ۗ
Na hawatoridhika nawe Mayahudi wala Manaswara mpaka ufuate mila zao. [Al-Baqarah (2: 120)]
Na pia rejea: Aal-'Imraan (3: 85).
6. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) pia ameonya kuwafuata na kujifananisha na makafiri. Hadiyth: ((Kuweni kinyume na Washirikina, punguzeni masharubu na fugeni ndevu)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Pia amesema (صلى الله عليه وآله وسلم) ((Mtafuata nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia)) Wakasema (Maswahaba): Ee Rasuli wa Allaah! Je, unamaanisha Mayahudi na Manaswara? Akasema: ((Hivyo nani basi mwengine?)). [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na pia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Anayejishabihisha na watu, basi naye ni miongoni mwao)). [Ahmad na Abu Daawuwd]
7. Shakhsiya ya Muislamu ni makhsusi katika kufuata maamrisho ya Dini yake, mavazi yake, adabu zake, kuandamana kwake na marafiki, na anapaswa kufuata Sunnah za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) wala haipasi kuwafuata wasio Waumini katika ada na mila zao.