137-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Viumbe Waovu Kabisa Wajengao Misikiti Katika Makaburi Ya Waja Wema Wakachora Picha Zao
Lu-ulu-un-Manthuwrun
(Mkusanyiko Wa Hadiyth Mbali Mbali Na Mafunzo Yake)
Hadiyth Ya 137
Viumbe Waovu Kabisa Wajengao Misikiti Katika
Makaburi Ya Waja Wema Wakachora Picha Zao
عَنْ عَائِشَةَ (رضي الله عنها) قَالَتْ: لَمَّا اشتَكَى النَبي صلى الله عليه وسلم ذَكَرَ بعْضُ نِسَائِهِ كَنِيسَة رَأتْهَا بأرض الحَبَشةِ يُقَالُ لَهَا "مَارِيَةُ" وَكَانَتْ أُمُّ سَلَمَةَ وَأمُّ حَبيبَةَ أتتا أرْضَ الحَبَشَةَ، فَذَكَرَتَا من حُسْنِهَا وَتَصَاوير فِيهَا، فَرَفَعَ رَأسَهُ صلى الله عليه وسلم وَقالَ: ((أولئِكَ إِذَا مَاتَ فِيهِم الرَّجُلُ الصالح بَنَوْا عَلَى قَبْرِهِ مَسْجِداً ثُمَّ صَورُوا فِيهِ تِلْكَ الصُّورَ، أولئِكَ شِرَارُ الْخَلْقِ عِنْدَ الله)) متفق عليه
Imepokelewa kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) amesema: “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alipougua, mmoja katika wakeze alitaja kanisa aliloliona katika nchi ya Uhabashi liitwalo ‘Maariyah’. Ummu Salamah na Ummu Habiybah walikuwa wamewahi kwenda nchi ya Uhabashi. Wakataja uzuri wake na picha zilizokuwa humo. Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akakiinua kichwa chake akasema: ((Hao, anapokufa mwema miongoni mwao, hujenga Msikiti juu ya kaburi lake. Kisha wakazichora ndani yake picha hizo. Hao ni viumbe waovu mbele ya Allaah)). [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo Na Mwongozo:
1. Haramisho la kujenga Misikiti katika makaburi, kwani ni kushabihiana na makafiri na hivyo ni shirki kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) katika Hadiyth: Imepokelewa kutoka kwa Jundub bin ‘Abdillaah (رضي الله عنه) amesema: “Nilimsikia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم ) kabla hajaondoka duniani kwa siku tano akisema: ((Fahamuni! Hakika waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Manabii wao ni Misikiti. Fahamuni! Msiyafanye makaburi ni Misikiti, hakika mimi nawakataza jambo hilo)). [Muslim]
2. Kutembelea makaburi ya waja wema kwa kutufu kaburini mwake au kuligusa na kujipangusa, na kuwaomba ni bid’ah (uzushi) na miongoni mwa shirki kubwa, kwani ni kuitakidi kuwa waja wema hao wana uwezo wa kuwanufaisha na kuwadhuru na hali hakuna awezaye hayo isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى). Anasema (سبحانه وتعالى):
يَدْعُو مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَضُرُّهُ وَمَا لَا يَنفَعُهُ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الضَّلَالُ الْبَعِيدُ ﴿١٢﴾
Humwomba badala ya Allaah ambavyo visivyomdhuru na wala visivyomnufaisha. Huo ndio upotofu wa mbali.
يَدْعُو لَمَن ضَرُّهُ أَقْرَبُ مِن نَّفْعِهِ ۚ لَبِئْسَ الْمَوْلَىٰ وَلَبِئْسَ الْعَشِيرُ ﴿١٣﴾
Humwomba yule ambaye dhara yake iko karibu kuliko manufaa yake. Bila shaka ni mlinzi muovu kabisa, na bila shaka ni rafiki muovu kabisa. [Al-Hajj (22: 12-13)]
Rejea pia: Al-A’raaf (7: 194, 197), Al-Israa (17: 56), Sabaa (34: 22), Yuwnus (10: 18, 106-107), Al-‘Ankabuwt (29: 17).
3. Kuwatukuza wafu katika makaburi yao na kuwafanyia ‘ibaadah ni katika ujahili unaofanana na washirikina wa Makkah waliokuwa wakitoa hoja zao kuwa hawakuwa wakiwaabudu bali ni kujikurubisha kwa Allaah: Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):
وَالَّذِينَ اتَّخَذُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ
Na wale waliojichukulia badala Yake walinzi (wakisema): “Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah tumkaribie. [Az-Zumar (39: 3)]
4. Swalaah mbele ya kaburi ni haraam, ikiwa ni katika Msikiti au mbali na Msikiti.
5. Wanaodai kuwa kaburi la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) liko katika Msikiti ni kutokufahamu hali halisi ilivyokuwa ya kwamba:
(i) inajulikana kuwa Msikiti wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ulijengwa kabla ya kufariki kwake, kwa hiyo haukujengwa katika kaburi lake.
(ii) Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuzikwa katika Msikiti wake, bali alizikiwa nyumbani kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) nyumba ambayo ilitengana na Msikiti. Ila kosa lilitokea wakati Msikiti ulipopanuliwa mwisho wa karne ya kwanza, ulipobomolewa na kujengwa upya na kupanuliwa ndipo vyumba vya wake zake Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) vilipoingia katika eneo la Msikiti na ndani ya moja ya vyumba ndipo lilipo kaburi la Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) na kwa sababu pia haifai kuvunjwa kaburi lake au kufukuliwa na kuhamishwa.
Rejea Hadiyth namba (83), (129).
6. Haramisho la kuchora picha za viumbe wenye roho.
Rejea Hadiyth namba (120).
7. Mwenye kutenda mambo hayo mawili; kujenga Misikiti kaburini na kuchora picha ni kiumbe mwovu kabisa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) kutokana na sababu zake zilizotajwa na kukatazwa.
8. Hima kubwa ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwafunza Waumini yasiyopasa kutendwa kama shirki ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) haisamehi ikiwa mtu hakurudi kutubia. Hakuweza kuvumilia kusikia maovu, na akatoa nasiha hapohapo juu ya kuwa alikuwa anaugua.
9. Nasiha hizo za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ni miongoni mwa nasiha za mwisho katika uhai wake.