Kumuoa Binti Bila Ra Radhi Za Baba Yake
SWALI:
MUNGU AKUZIDISHIENI JUHUDI NA ILMU NA AKULIPENI UJIRA MZURI KATIKA AWALIPAO WAJA WAKE WEMA KWA NJIA HII INOTUPATIA FAIDA KWA NJIA YA KIRAHISI..WASSALA LLAHU ALLA SAYYIDI NA MUHAMMAD WAAALA ALIHI WAASHABIHI WASSALAM...
MIMI NI MWANAMME
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.
Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn
Katika mas-ala haya ya ndoa tumezungumzia mara nyingi yale masharti ambayo yanafaa kutekelezwa ili ndoa iswihi. Miongoni mwayo ni:
1- Idhini ya baba mzazi au walii wa msichana.
2- Kupatikane mashahidi wawili waadilifu.
3- Kukubali kwa bwana na bibi harusi kwa ndoa hiyo bila kulazimishwa.
Moja tu kati masharti haya ikikosekana basi ndoa yenyewe haiswihi kabisa. Na katika swali la muulizaji ni kuwa hakujapatikana idhini ya walii (baba) wa huyo msichana, hivyo ndoa haitaswihi.
Nasaha yetu ya kwanza ni kuwa kwa vile baba amekataa kutoa ruhusa kwa yale aliyoyasikia kukuhusu katika maasiya uliyokuwa ukiyafanya, inatakiwa utume watu wazee waende wakamueleweshe huyo baba kuwa mambo yamebadilika na siyo kama yalivyokuwa. Hata huyo binti yake ambaye atakuwa anamjua baba vilivyo anatakiwa amueleze mama yake na pia baba yake kuhusu ukweli wa mambo. Ikiwa hata baada ya kuelezwa baba bado amedinda na hataki hiyo harusi kufanyika, munaweza kuchukua hatua ya pili.
Hatua hii ni wewe kwenda kwa Qadhi ikiwa katika mji unaoushi yupo mmoja au kwa Shaykh ambaye anafanya pia kazi ya kuozesha na ameboea kwa kiasi fulani kuhusu mas-ala ya Dini. Huyu Qadhi au Shaykh atamuita huyo baba amsikilize kuhusu sababu zake za kukataa kutoa idhini. Ikiwa sababu zake zinakubalika kisheria basi ndoa haitaweza kufanyika lakini ikiwa hana sababu za msingi za kukataa basi Qadhi atakuwa ndiye walii wa msichana naye atakuozesha na ndoa hiyo itakuwa ni halali.
Lakini kwa uzoefu tulionao kuhusu mas-ala haya ni kuwa jaribu kuchukua hatua ya kwanza mpaka ifanikiwe kwa idhini ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwani hatua ya pili inakuja na matatizo ya msichana kukatwa kabisa na wazazi wake na hivyo hata wajukuu wenu kutopata kuwajua babu na bibi zao kwa upande wa mama.
Tunakuombea kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akunyoshee mambo yako na ikiwa huyo msichana ana kheri nawe afanye moyo wa baba ulainike na akubali. Lakini ikiwa hana kheri nawe basi Akupatie badala njema kwa msichana mwengine mwenye Dini, Imani na maadili mema, Aamiyn.
Na Allah Anajua zaidi