04-Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd: Tawhiyd Ni Ahadi Waliyofungamana Viumbe Wote Na Allaah Kabla Ya Kuzaliwa Kwao

 

 

Umuhimu Na Fadhila Za Tawhiyd

 

04-Tawhiyd Ni Ahadi Waliyofungamana Viumbe Wote Na Allaah Kabla Ya Kuzaliwa Kwao

 

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alikusanya roho za wana Aadam wote kabla ya kuumbwa kwao, zikafungamana ahadi Naye ya kukiri kwamba Yeye Ndiye Rabb wao na kwamba watampwekesha bila ya kumshirikisha na zikaahidi pia kumtii:

 

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ﴿١٧٢﴾

Na pindi Rabb wako Alipochukua katika wana wa Aadam kutoka migongoni mwao, kizazi chao, na Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, “Je, Mimi siye Rabb wenu?” Wakasema: “Ndio bila shaka, tumeshuhudia!” (Allaah Akawaambia): “Msije kusema Siku ya Qiyaamah: hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya.”

 

أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ ۖ

Au mkasema: “Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla, nasi tulikuwa kizazi baada yao. [Al-A’raaf: 172-173]

 

Roho hizo ni za wana Aadam wote tokea Nabiy Aadam (‘Alayhis-Salaam) mpaka siku ya Qiyamaah. Kwa maana: wana Aadam wote wanaozaliwa au watakaozaliwa leo au kesho au mwakani na kuendelea mpaka Siku ya Qiyaamah, roho zao zimeshaumbwa. Dalili ni Hadiyth ifuatayo ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) kuhusu roho kupulizwa tumboni mwa mama anaposhika mimba inayofikia muda wa miezi minne (siku 120):    

 

عَنْ أَبِي عَبْدِ الرَّحْمَنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رضي الله عنه قَالَ: حَدَّثَنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم -وَهُوَ الصَّادِقُ الْمَصْدُوقُ: ((إِنَّ أَحَدَكُمْ يُجْمَعُ خَلْقُهُ فِي بَطْنِ أُمِّهِ أَرْبَعِينَ يَوْمًا نُطْفَةً، ثُمَّ يَكُونُ عَلَقَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يَكُونُ مُضْغَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يُرْسَلُ إلَيْهِ الْمَلَكُ فَيَنْفُخُ فِيهِ الرُّوحَ، وَيُؤْمَرُ بِأَرْبَعِ كَلِمَاتٍ: بِكَتْبِ رِزْقِهِ، وَأَجَلِهِ، وَعَمَلِهِ، وَشَقِيٍّ أَمْ سَعِيدٍ؛ فَوَاَللَّهِ الَّذِي لَا إلَهَ غَيْرُهُ إنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُهَا. وَإِنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَيَدْخُلُهَا)) رواه البخاري ومسلم

Kutoka kwa Abuu 'Abdir-Rahmaan 'Abdillaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: “Ametusimulia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake).  Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. Wa-Allaahi naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye ‘amali za watu wa Jannah hadi ikawa baina yake na Jannah ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya ‘amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya ‘amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya ‘amali ya watu wa Jannah akaingia Jannah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Share