10-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Wanaume Na Wanawake Wanaomdhukuru Mno Allaah

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

10- Wanaume Na Wanawake Wanaomdhukuru Mno Allaah

 

 

 

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, na wafungao Swawm wanaume na wanawake, wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu. [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi ni sifa ya mwisho kutajwa katika Aayah hiyo tukufu.  Na kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni ‘ibaada pekee ambayo haina mipaka ya kutekelezwa kwake kutokana na kauli ya Allaah ('Azza wa Jalla):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا ﴿٤١﴾

Enyi walioamini!  Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru. [Suratul-Ahzaab: 41]  

 

 

Na kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni ‘ibaadah nyepesi kabisa inayoweza kudumishwa:

 

4-Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni ‘ibaadah nyepesi inayowezwa kudumishwa:

 

عن عبد الله بن بسرٍ رضي الله عنهُ أن رجلاً قال : يا رسول الله إن شرائع الإسلام قد كثرت علي فأخبرني بشيءٍ أتشبث به. قال : (( لا يزال لسانك رطباً من ذكر الله)) ألترمذي إبن ماجه وصححه شيخ الألباني   

Imepokelewa kutoka kwa Abdullaah Bin Busr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu mmoja alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! ‘Ibaadah za Dini zimekuwa nyingi kwangu, basi nieleze kitu ambacho nitaweza kudumu nacho?” Akasema: ((Ulimi wako utaendelea kuwa rutuba (yaani sio ukavu) kwa kumdhukuru Allaah)) [At-Tirmidhiy na Ibn Maajah na imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutajia jinsi ya kufikia daraja la kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi katika Hadiyth zifuatazo:

 

قَالَ اِبْن أَبِي حَاتِم  عَنْ أَبِي سَعِيد الْخُدْرِيّ رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : إِنَّ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((إِذَا أَيْقَظَ الرَّجُل اِمْرَأَته مِنْ اللَّيْل فَصَلَّيَا رَكْعَتَيْنِ كَانَا تِلْكَ اللَّيْلَة مِنْ الذَّاكِرِينَ اللَّه كَثِيرًا وَالذَّاكِرَات))   أبو داود ،

Ibn Abiy Haatim amesesma kutoka kwa Abuu Sa'iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  (Mume akimuamsha mkewe usiku wakaswali Rakaa mbili watakuwa usiku huo ni miongoni mwa wale wanaume na wanawake wanaomdhukuru Allaah sana))   [Abuu Daawuwd]

 

Pia:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : كَانَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَسِير فِي طَرِيق مَكَّة فَأَتَى عَلَى جُمْدَان فَقَالَ ((هَذَا جُمْدَان سِيرُوا فَقَدْ سَبَقَ الْمُفَرِّدُونَ)) قَالُوا وَمَا الْمُفَرِّدُونَ ؟ قَالَ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((الذَّاكِرُونَ اللَّه كَثِيرًا وَالذَّاكِرَات)) ثُمَّ قَالَ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((اللَّهُمَّ اِغْفِرْ لِلْمُحَلِّقِينَ)) قَالُوا وَالْمُقَصِّرِينَ قَالَ ((اللَّهُمَّ اِغْفِرْ لِلْمُحَلِّقِينَ)) قَالُوا وَالْمُقَصِّرِينَ قَالَ ((وَالْمُقَصِّرِينَ)) إمام أحمد تفرد به من هذا الوجه، ورواه مسلم دون آخره

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba:  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akitembea katika njia ya Makkah na alipofika mlima wa Jumdaan akasema: ((Huu ni (mlima wa) Jumdaan, endeleeni kwani Mufarriduwn wametangulia mbele)). Wakasema: Ni nani Mufarraduun? Akasema: ((Wanaomdhukuru Allaah sana wanaume na wanawake)). Kisha akasema: ((Ee Allaah, Waghufurie walionyoa nywele zao)). Wakasema: "Na waliopunguza". Akasema: ((Ee Allah Waghufurie walionyoa nywele zao)). Wakasema: "Na waliopunguza". Akasema: ((Na waliopunguza)). [Imaam Ahmad kaipokea kwa masimulizi hayo, na Muslim bila ya maelezo ya mwisho]

 

 

Na pia kuomba du’aa:

 

 

عَنْ مُعَاذِ بْنِ جَبَلٍ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم أَخَذَ بِيَدِهِ وَقَالَ: ((يَا مُعَاذُ وَاللَّهِ إِنِّي لأُحِبُّكَ وَاللَّهِ إِنِّي لأُحِبُّكَ))‏.‏ فَقَالَ: ((أُوصِيكَ يَا مُعَاذُ لاَ تَدَعَنَّ فِي دُبُرِ كُلِّ صَلاَةٍ تَقُولُ: اللَّهُمَّ أَعِنِّي عَلَى ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ))‏ ‏.‏ وَأَوْصَى بِذَلِكَ مُعَاذٌ الصُّنَابِحِيَّ وَأَوْصَى بِهِ الصُّنَابِحِيُّ أَبَا عَبْدِ الرَّحْمَنِ ‏.‏

 

Imepokelewa kutoka kwa Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alimshika mkono wake akasema: ((Ee Mu’aadh!  Wa-Allaahi mimi nakupenda! Wa-Allaahi mimi nakupenda!)) Akasema: ((Nakuusia ee Mu’aadh usiache kusema katika kila baada ya Swalaah:

اللّهُـمَّ أَعِـنِّي عَلـى ذِكْـرِكَ وَشُكْـرِك وَحُسْـنِ عِبـادَتِـك

Allaahumma A’inniy ’alaa dhikrika washukrika wahusni ’Ibaadatika

 

Ee Allaah nisaidie juu Kukudhukuru, na kukushukuru na kukuabudu kwa uzuri utakikanao  

 

[Hadiyth ya Mu’aadh bin Jabal (رضي الله عنه) - Abu Daawuwd (2/86), An-Nasaaiy (3/53) na ameisahihisha Al-Albaaniy (رحمه الله) katika Swahiyh Abi Daawuwd (1/284)].

 

 

Fadhila za kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni nyingi mno, baadhi yake ni zifuatazo:

 

 

1-Ukimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Naye Atakukumbuka kama Anavyosema:

 

فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلَا تَكْفُرُونِ﴿١٥٢﴾

Basi nidhukuruni na Mimi Nitakukumbukeni; na nishukuruni wala msinikufuru. [Al-Baqarah: 152]

 

 

 

2-Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni ‘ibaadah bora kabisa yenye daraja ya juu:

 

 

 عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((ألاَ أُنَبِّئُكُمْ بِخَيْرِ أَعْمَالِكُمْ، وَأَزْكَاهَا عِنْدَ مَلِيكِكُمْ، وَأَرْفَعِهَا فِي دَرَجَاتِكُمْ، وَخَيْرٌ لَكُمْ مِنْ إِنْفَاقِ الذَّهَبِ وَالفِضَّةِ، وَخَيْرٌ لَكُمْ مِنْ أَنْ تَلْقَوْا عَدُوَّكُمْ فَتَضْرِبُوا أَعْنَاقَهُمْ وَيَضْرِبُوا أَعْنَاقَكُمْ؟)) قَالُوا : بَلَى: قَالَ: ((ذِكْرُ اللَّهِ تَعَالَى)) رواه الترمذي. قَال الحاكم أبو عبد الله: إسناده صحيح

Imepokelewa kutoka kwa Abu Ad-Dardaa(رضي الله عنه)   ambaye amesema: “Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hivi niwaambieni khabari ya matendo yenu bora zaidi, na ambayo ni masafi mno mbele ya Rabb wenu, na ambayo ni ya juu mno katika daraja zenu, na ambayo ni bora kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha, na ambayo ni bora kuliko kukutana na adui zenu mkawapiga shingo zao, nao wakakupigeni shingo zenu?))  Wakasema [Maswahaba]: Ndio. Akasema ((Ni kumdhukuru Allaah Ta’aalaa)). [At-Tirmidhiy na amesema Abu ‘Abdillaah: Isnaad yake ni Swahiyh]

 

 

3-Kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni kuwa karibu Naye:

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((يَقُولُ اللَّهُ تَعَالَى: أَنَا عِنْدَ ظَنِّ عَبْدِي بِي وَأَنَا مَعَهُ إِذَا ذَكَرَنِي، فَإِنْ ذَكَرَنِي فِي نَفْسِهِ ذَكَرْتُهُ فِي نَفْسِي، وَإِنْ ذَكَرَنِي فِي مَلَإٍ ذَكَرْتُهُ فِي مَلَإٍ خَيْرٍ مِنْهُمْ، وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ بِشِبْرٍ تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا،  وَإِنْ تَقَرَّبَ إِلَيَّ ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ بَاعًا، وَإِنْ أَتَانِي يَمْشِي أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً)) متفق عليه

 Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) ambaye amesema: Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)  alisema: ((Allaah Ta’aalaa Anasema: Mimi ni vile mja Wangu anavyonidhania. Niko pamoja naye anaponitaja. Anaponitaja katika nafsi yake, Ninamtaja katika nafsi Yangu, anaponitaja katika hadhara, Ninamtaja katika hadhara bora zaidi. Na anaponikaribia shibiri Ninamkaribia dhiraa, anaponikaribia dhiraa, Ninamkaribia pima, anaponijia kwa mwendo [wa kawaida] Ninamwendea mbio)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Madhara ya kutokumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 

1-Kukaa katika kikao bila ya kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni kujichumia dhambi.

 

 

قال صلى الله عليه وسلم: ((مَا جَلَسَ قَوْمٌ مَجْلِسًا لَمْ يَذْكُرُوا اللَّهَ فِيهِ وَلَمْ يُصَلُّوا عَلَى نَبِيِّهِمْ إِلَّا كَانَ عَلَيْهِمْ تِرَةً فَإِنْ شَاءَ عَذَّبَهُمْ وَإِنْ شَاءَ غَفَرَ لَهُمْ))  

Na amesema (صلى الله عليه وسلم): ((Hapana watu wowote wale, wanaokaa kikao kisha wasimdhukuru Allaah humo, wala wasimswalie Nabiy wao ila watakuwa wana dhambi. Akipenda Atawaadhibu na Akipenda Atawaghufuria))  [Hadiyth ya Abuu Hurayrah(رضي الله عنه)   - At-Tirmidhiy [3380] na taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/140)] 

 

Na pia: 

 

وقال صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ قَعَدَ مَقْعَدًا لَمْ يَذْكُرِ اللَّهَ فِيهِ، كَانَتْ عَلَيْهِ مِنَ اللَّهِ تِرَةٌ, وَمَنِ اضْطَجَعَ مَضْجَعًا لَمْ يَذْكُرِ اللَّهَ فِيهِ ، كَانَتْ عَلَيْهِ مِنَ اللَّهِ تِرَةٌ))

Na amesema (صلى الله عليه وسلم): ((Anayekaa kikao chochote kile asimdhukuru Allaah katika kikao hicho basi ana dhambi kutoka kwa Allaah, na anayelala sehemu yeyote ile kisha asimdhukuru Allaah wakati wakuinuka sehemu hiyo basi ana dhambi kwa Allaah)) [Hadiyth ya Abu Hurayrah(رضي الله عنه)   - Abu Daawuwd (4/264) [4856] na wengineo na taz. Swahiyh Al-Jaami’ (5/342) [6477].

 

 

 

2-Kukaa katika kikao bila ya kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni kama mzoga wa punda na kuwa na majuto.

 

 

وقال صلى الله عليه وسلم: ((مَا مِنْ قَوْمٍ يَقُومُونَ مِنْ مَجْلِسٍ لَا يَذْكُرُونَ اللَّهَ فِيهِ إِلَّا قَامُوا عَنْ مِثْلِ جِيفَةِ حِمَارٍ وَكَانَ لَهُمْ حَسْرَةً))

Na amesema (صلى الله عليه وسلم): ((Hapana watu wowote wale wanaosimama katika kikao walichokaa, kisha wasimdhukuru  Allaah ila watakuwa wanasimama kama mzoga wa punda, na watakuja juta [kwa kutokumdhukuru Allaah])) [Hadiyth ya Abu Hurayrah(رضي الله عنه)   - Abu Daawuwd (4/264) [4855], Ahmad (2/389) na taz Swahiyh Al-Jaami’ (5/176) [5750].

 

 

 

3-Asiyemdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) ni kama mtu aliyekufa.

 

وقال صلى الله عليه وسلم: ((مَثَـــلُ الـــذي يَـــذكُرُ ربَّـــهُ وَالـــذي لا يـــذكُرُهُ، مَثَـــل الحـــيِّ والمَيِّــتِ))

Na amesema (صلى الله عليه وسلم): ((Mfano wa anayemdhukuru  Mola wake na asiyemdhukuru ni mfano wa aliye hai na maiti)) [Hadiyth ya Abu Muwsaa Al-Ash’ariyy(رضي الله عنه)   -Al-Bukhaariy  pamoja Al-Fat-h (11/208) au namba [6407] 

 

 

 

Swahaba ‘Abdullaah Ibn ‘Amru Ibn Al-‘Aasw - Swahaba aliyekuwa akimdhukuru sana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

Ni Swahaba ambaye aliingia katika Uislamu kabla ya baba yake tokea siku aliyochukua kiapo cha utiifu.   Alikuwa mwenye moyo uliojaa nuru ya twaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

   

Alitumia wakati wote katika kusoma na kuifahamu Qur-aan ili utakapofika wakati wa kumalizika wahyi wote awe ameshaihifadhi yote. Na hakuisoma tu kwa ajili ya uwezo wa kuihifadhi, bali aliisoma na kufuata amri zake kama Maswahaba wengineo.

 

‘Abdullah ibn ‘Amru ibn Al-‘Aasw alikuwa mwenye taqwa ya hali ya juu na mtekelezaji ‘ibaadah kwa wingi.

 

Katika vita dhidi ya maadui wa Kiislamu alionekana katika mstari wa mbele kabisa akitamani kufariki kama shahidi. Na alikuwa akionekana daima Msikitini, na alikuwa mwenye kupenda kufunga swawm na kuswali Swalaah za usiku. Ulimi wake ulikuwa ni wa kila mara kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla). Alikuwa akikhitimisha Qur-aan kila siku moja.

 

Hali yake hii ilimfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amnasihi apunguze ‘ibaadah ili aweze kutekeleza mengineyo yenye haki naye.   

 

Hadiyth yake mashuhuri imerekodiwa na Maimaam sita wa Hadiyth. 

 

 

  "كنت أصوم الدهر، وأقرأ القرآن كل ليلة، قالفإما ذكرت لرسـول الله  صلى الله عليه وسلم ، وإما أرسل لي، فأتيته، فقال: "ألم أُخبر أنك تصوم الدهر وتقرأ القرآن كل لـيـلـة ؟" فقلت: بلى يا نبي الله؛ ولم أرد إلا الخـيـر، قال: "فـإن بحـسـبك أن تصوم من كل شهر ثلاثة أيام... ، ثم قال: "واقرأ القرآن في كل شهر"، قال: قلت: يا نبي الله: إني أطيق أفضل من ذلك، قال: "فاقرأه في سـبـع، ولا تـزد عـلــى ذلك، فإن لزوجك عليك حقاً، ولزورك عليك حقاً، ولجسدك عليك حقاً، قال: فشددت؛ فشدد علي، قال: وقال لي النبيصلى الله عليه وسلم: "لعلك يطول بك العـمــر"، فصرتُ إلى الذي قال لي النبيصلى الله عليه وسلم ، فلما كبرت وددت أني قبلت رخصة النبي صلى الله عليه وسلم.

“Nilikuwa nikifunga mwaka mzima, na nikisoma Qur-aan kila usiku. Alipojulishwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaniita kwake nikaenda. Akasema: ((Nimesikia kwamba unafunga mwaka mzima na unasoma (unakhitimisha) Qur-aan kila usiku?)) Nikasema: Ndio ee Rasuli wa Allaah. Wala sitaki lolote ila kheri tu. Akasema: ((Inakutosheleza ukifunga katika kila mwezi siku tatu…)) Kisha akasema: ((Na usome Qur-aan (ukhitimishe) kila mwezi)). Akasema: Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah, mimi hakika naweza kufanya vizuri zaidi ya hivyo. Akasema: ((Basi soma katika siku saba na usizidishe juu ya hivyo, kwani mke wako ana haki na wewe, na wageni wako wana haki kwako, na mwili wako una haki kwako)). Akasema: Kila nikimkazania (nizidishe ‘ibaadah) alikuwa akinikazania (nipunguze). Akasema: Akaniambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Huenda umri ukawa mrefu kwako)) Nikaendeleza (‘ibaadah) kama alivyoniambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Nilipokuwa mkubwa kiumri nilipendelea kufuata rukhsa aliyonipa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Share