11-Sifa Kumi Na Fadhila Zake: Maghfirah Na Ujira Adhimu Baada Ya Kuzichuma Sifa Kumi

 

Sifa Kumi Na Fadhila Zake

 

11-Maghfirah Na Ujira Adhimu Baada Ya Kuzichuma Sifa Kumi

 

 

 

Aayah kamili kuhusu sifa kumi ni: 

 

 

إِنَّ الْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمَاتِ وَالْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ وَالْقَانِتِينَ وَالْقَانِتَاتِ وَالصَّادِقِينَ وَالصَّادِقَاتِ وَالصَّابِرِينَ وَالصَّابِرَاتِ وَالْخَاشِعِينَ وَالْخَاشِعَاتِ وَالْمُتَصَدِّقِينَ وَالْمُتَصَدِّقَاتِ وَالصَّائِمِينَ وَالصَّائِمَاتِ وَالْحَافِظِينَ فُرُوجَهُمْ وَالْحَافِظَاتِ وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾

Hakika Waislamu wanaume na wanawake, na Waumini wanaume na wanawake, na watiifu wanaume na wanawake, na wasemao kweli wanaume na wanawake, na wanaosubiri wanaume na wanawake, na wanyenyekevu wanaume na wanawake, na watoao swadaqah wanaume na wanawake, na wafungao Swawm wanaume na wanawake, wanaojihifadhi tupu zao wanaume na wanawake, na wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume na wanawake; Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu.  [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Baada ya kutajwa sifa kumi katika Aayah tukufu, na pindi zikitekelezwa, Allaah ('Azza wa Jalla) Ameahidi kuwaghufuria madhambi waja Wake na kuwalipa ujira mkubwa, mtukufu. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا ﴿٣٥﴾

Allaah Amewaandalia maghfirah na ujira adhimu. [Al-Ahzaab: 35]

 

 

Vile vile Anasema katika Aayah nyingine:

 

 

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ ۙ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿٩﴾

Allaah Amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema; watapata maghfirah na ujira adhimu. [Al-Maaidah: 9]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni mwingi wa kughufuria madhambi ya waja Wake, kama ilivyothibiti katika Qur-aan:

 

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ ﴿٨٢﴾

Na hakika Mimi bila shaka ni Mwingi mno wa kughufuria kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akaendelea kuongoka.  [Twaaha: 82]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ

Naye Ndiye Ambaye Anapokea tawbah kutoka kwa waja Wake, na Anasamehe maovu [Ash-Shuwraa: 25]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١١٠﴾

Na atakayetenda ovu au akajidhulumu nafsi yake; kisha akamwomba Allaah maghfirah; atamkuta Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [An-Nisaa: 110]

 

 

Na Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى يَا ابْنَ آدَمَ،  إِنَّكَ مَا دَعَوْتَنِي وَرَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ عَلَى مَا كَانَ فِيكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنَانَ السَّمَاءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الْأَرْضِ خَطَايَا ثُمَّ لَقِيتَنِي لَا تُشْرِكُ بِي شَيْئًا لَأَتَيْتُكَ بِقُرَابِهَا مَغْفِرَةً))  أخرجه الترمذي وحسنه الألباني في الصحيحة  

Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah  Tabaaraka wa Ta’aalaa  Amesema: Ee bin-Aadam! Hakika ukiniomba na ukanitaraji (kwa malipo) Nitakughufuria yale yote uliyonayo na wala Sijali, Ee bin-Aadam! Lau zingefikia dhambi zako ukubwa wa mbingu, kisha ukaniomba maghfirah, Ningekughufuria bila ya kujali (kiasi cha madhambi uliyoyafanya). Ee bin-Aadam! Hakika ungenijia na madhambi yakaribiayo ukubwa wa ardhi, kisha ukakutana nami na hali hukunishirikisha chochote, basi Nami Nitakujia na maghfirah yanayolinga nayo.” [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan]

 

Vile vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameahidi kutuingiza katika Jannah  kwa Rahmah Yake pindi tukiifanyia kazi kwa kutenda mema.  Basi ni kujitahidi kuchuma sifa kama hizo kumi ambazo zinahitaji azimio dhubuti, jitihada na subira, na matarajio. Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ﴿٥٨﴾

Na wale walioamini na wakatenda mema, bila shaka Tutawawekea makazi ya ghorofa katika Jannah, yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje ujira wa watendao.

 

 

الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٥٩﴾

Ambao walisubiri na kwa Rabb wao wanatawakali. [Al-‘Ankabuwt: 58-59]

 

Neema za huko Peponi zimetajwa katika Aayah nyingi za Qur-aan na katika Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), miongoni mwazo ni:  

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي ظِلَالٍ وَعُيُونٍ﴿٤١﴾

Hakika wenye taqwa wamo katika vivuli na chemchemu.

 

 

وَفَوَاكِهَ مِمَّا يَشْتَهُونَ﴿٤٢﴾

Na matunda katika yale wanayoyatamani.

 

 

كُلُوا وَاشْرَبُوا هَنِيئًا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٤٣﴾

(Wataambiwa): “Kuleni na kunyweni kwa furaha kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda.”

 

 

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ﴿٤٤﴾

Hakika hivyo ndivyo Tunavyowalipa wafanyao ihsani. [Al-Mursalaat: 41-44]

 

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 أُولَـٰئِكَ لَهُمْ رِزْقٌ مَّعْلُومٌ ﴿٤١﴾

Hao watapata riziki maalumu.

 

 

فَوَاكِهُ ۖ وَهُم مُّكْرَمُونَ ﴿٤٢﴾

Matunda; nao ni wenye kukirimiwa

 

 

فِي جَنَّاتِ النَّعِيمِ ﴿٤٣﴾

Katika Jannaat za neema.

 

 

عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ ﴿٤٤﴾

Juu ya makochi ya enzi wakikabiliana.

 

 

يُطَافُ عَلَيْهِم بِكَأْسٍ مِّن مَّعِينٍ ﴿٤٥﴾

Wanazungushiwa gilasi za mvinyo kutoka chemchemu.

 

 

بَيْضَاءَ لَذَّةٍ لِّلشَّارِبِينَ ﴿٤٦﴾

Nyeupe, ya ladha kwa wanywaji.

 

 

لَا فِيهَا غَوْلٌ وَلَا هُمْ عَنْهَا يُنزَفُونَ ﴿٤٧﴾

Hamna humo madhara yoyote na wala wao kwayo hawataleweshwa.

 

 

وَعِندَهُمْ قَاصِرَاتُ الطَّرْفِ عِينٌ ﴿٤٨﴾

Na watakuwa nao wanawake wenye staha wanaoinamisha macho, wenye macho mapana mazuri ya kuvutia. 

 

 

كَأَنَّهُنَّ بَيْضٌ مَّكْنُونٌ ﴿٤٩﴾

 (Wanyororo, watakasifu) kama kwamba mayai yaliyohifadhiwa. [Asw-Swaafaat: 41-49]

 

 

Hiyo ni ahadi ya Allaah ('Azza wa Jalla) ambayo hakika Yeye Haendi kinyume nayo kama Anavyosema:

 

 لَـٰكِنِ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ لَهُمْ غُرَفٌ مِّن فَوْقِهَا غُرَفٌ مَّبْنِيَّةٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَعْدَ اللَّـهِ ۖ لَا يُخْلِفُ اللَّـهُ الْمِيعَادَ﴿٢٠﴾

 Lakini wale waliomcha Rabb wao, watapata maghorofa yaliyojengwa juu yake maghorofa, yanapita chini yake mito.  Ni ahadi ya Allaah. Allaah Hakhalifu miadi. [Az-Zumar: 20]

 

 

Kisa Cha Swahaba 'Amru bin Al-Jamuw’ aliyetamani Jannah:

 

 

'Amru bin Al-Jamuw’ (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa kilema. Alikuwa na watoto wa kiume wanne ambao walikuwa wakihudhuria vita mbali mbali.

Ulipofika wakati wa vita vya Uhud, 'Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alitamani kupigana vita hivyo lakini watu walimzuia kwa vile ni kilema wakimwambia: "Wewe umeruhusiwa kutokupigana vita kutokana na hali yako, kwa hiyo huna haja ya kwenda vitani." Lakini yeye akawajibu: "Inasikitisha kuwa watoto wangu wapate Jannah nami nisiipate."

 

wake pia alitaka sana mumewe apate fadhila ya kufariki katika hali ya Shahidi,  hivyo akamshikilia aende hivyo hivyo japokuwa   ni kilema, akimwambia: "Sioni kama  udhuru huo wako utakuzuia kwenda kupigana vita, ila labda naona kama una khofu tu ya kwenda vitani!”

 

Aliposikia hivyo 'Amru (Radhwiya Allaahu 'anhu) alijitayarisha kwenda vitani akaelekea Qiblah na kuomba: "Ee Allah Usinirudishe kwa familia yangu tena!"

 

 

Imesemekana kwamba alikwenda vitani na alionekana akipigana na huku akisema kwa fakhari: "Naapa kwa Allaah, hakika mimi naitamani Jannah!”

Mtoto wake alikuwa akimfuatilia nyuma yake. Wakipigana hadi wote wakauliwa.

 

 

Mke wake aliposikia kuwa mumewe na mtoto wake wamefariki, alituma ngamia ili wachukuliwe miili yao. Imesemekana kwamba miili yao ilipopandishwa juu ya ngamia na kuondoka, ngamia huyo aligoma kusimama. Alipolazimisha kusimama aligoma kuelekea Madiynah bali alirudia kuelekea jabali la Uhud. Mkewe alipoulizwa kuhusu hilo, akasema kuwa 'Amru (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliomba du'aa kuwa asirudishwe kwao. Na ndio ikawa sababu ya kugoma ngamia kurudi Madiynah.

 

 

 

 

 

Share