10-Madhara Ya An-Namiymah (Kufitinisha): Maana, Hukumu Na Adhabu Zake
Madhara Ya Ghiybah (Kusengenya) Na An-Namiymah (Kufitinisha)
10- An-Namiymah: Maana, Hukumu Na Adhabu Zake
Maana ya An-Namiymah:
Ni kufitinisha, kwa maana kuchongeza kwa kuhamisha au kupeleka maneno baina ya watu ili kusababisha wachukiane.
Mfano kumwambia mwenzio: "Fulani kakusengenya wewe kadhaa na kadhaa." Au, "Fulani anakuchukia wala hakupendi."
Kufitinisha huku kunaweza kuwa ni kwa kutamka maneno, au kwa kuandika au hata kwa kuonyesha ishara. Inaweza kuwa ni kufitinisha kwa kumsingizia mtu au hata kama huyo mtu alisema kweli usemi huo haijuzi kufitinisha.
Mtu kama huyu mwenye kufitinisha ni mwenye nyuso mbili anamkabili kila mmoja kwa uso mzuri kumbe hampendelei kheri, ni kama kinyonga anayebadilika rangi kwa hali anayojipendelea nafsi yake. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya watu kama hawa kwa kusema:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: (( إِنْ شَرَّ النَّاسِ ذُو الْوَجْهَيْنِ الَّذِي يَأْتِي هَؤُلاَءِ بِوَجْهٍ وَهَؤُلاَءِ بِوَجْهٍ)) البخاري
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu): kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika watu waovu kabisa ni wenye nyuso mbili ambao wanawaendea kundi la watu kwa uso mmoja na kundi la watu wengine kwa uso mwingine)) [Al-Bukhaariy]
Mtu huyu ni tofauti na Muislamu mkweli mwenye uso mmoja katika hali zote baina ya ndugu zake au rafiki zake, naye ana ulimi mmoja wa ukweli, hasemi ila yanaomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Hukmu ya An-Namiymah:
Ni haraam kama ilivyobainishwa katika Qur-aan na Sunnah na miongoni mwa madhambi makubwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَّهِينٍ﴿١٠﴾
Na wala usimtii kila mwingi wa kuapa, dhalili.
هَمَّازٍ مَّشَّاءٍ بِنَمِيمٍ﴿١١﴾
Mwingi wa kukashifu, mpitaji huku na kule kwa kufitinisha.
مَّنَّاعٍ لِّلْخَيْرِ مُعْتَدٍ أَثِيمٍ﴿١٢﴾
Mwingi wa kuzuia ya kheri, mwenye kutaadi, mwingi wa kutenda dhambi. [Al-Qalam: 10-12]
Athari ya An-Namiymah:
Kupatikana mtafaruku baina ya watu, kuondosha furaha katika nyoyo na badala yake maudhi, kujenga uadui, kuchukiana, kukatiana au kuzuiliana rizki, na huenda ikasabisha hata kuuana.
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ، أن النبي صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((أَلاَ أُنَبِّئُكُمْ مَا الْعَضْهُ هِيَ النَّمِيمَةُ الْقَالَةُ بَيْنَ النَّاسِ)) رواه مسلم
Kutoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesimulia kwamba: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Je, nikujulisheni nini Al-'Adhwhu? Ni An-Namiymah [kuchongeza baina ya watu])) [Muslim]
Adhabu zake:
1-Kuharamishwa Jannah:
عن حذيفة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((لا يَدْخُلُ الجَنَّةَ نَمَّامٌ)) رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Hudhayfah (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mchongezi hataingia Jannah)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
2-Adhabu Kaburini:
عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ، قَالَ مَرَّ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم عَلَى قَبْرَيْنِ فَقَالَ: ((أَمَا إِنَّهُمَا لَيُعَذَّبَانِ وَمَا يُعَذَّبَانِ فِي كَبِيرٍ أَمَّا أَحَدُهُمَا فَكَانَ يَمْشِي بِالنَّمِيمَةِ وَأَمَّا الآخَرُ فَكَانَ لاَ يَسْتَتِرُ مِنْ بَوْلِهِ )) متفق عليه
Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ambaye amesimulia kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyapitia makaburi mawili na akasema: ((Hakika hawa wanaadhibiwa. Wala hawaadhibiwi kwa sababu ya jambo kubwa (la kuwashinda kutekeleza au kujiepusha nalo." Kisha hapo hapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hapana! Bali ni kubwa (dhambi kubwa na adhabu zake)! Mmoja wao alikuwa akipita kwa An-Namiymah (kufitinisha) na mwingine alikuwa hajikingi na mkojo [anapokojoa])) [Al-Bukhaariy na Muslim]